Skip to content

Pole, Polepole!

Kwa asiyekuwa mweledi, Bwana Humphrey Polepole ni mpigadebe mzuri, ni mpambaji mjuzi na dalali anayeweza kumuuzia mtu jaa [jalala] kwa jina la kasri ya mtindo wa Mediterranean. Wazanzibari tumemsikia katibu huyo wa itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) anavyonadi kwamba wanakusudia kuiletea Zanzibar maendeleo ya mwendokasi chini ya mgombea wao, Bwana Hussein Mwinyi, endapo atachaguliwa kuwa rais wa Zanzibar.

Kifungu cha 23 cha Katiba ya Zanzibar kinamuwajibisha kila Mzanzibari kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa Zanzibar.  Wajibu huu utatekelezeka tu, endapo wananchi wa Zanzibar watakuwa na viongozi waliowachagua kwa kuwaamini, kuwakubali na kuwa na uwezo wa kuwawajibisha.

Na Othman Masoud Othman

Viongozi ambao watawekwa madarakani kwa ghilba za uchaguzi, matumizi ya nguvu za dola, upotoshaji na kwa malengo yasiyokuwa na udhati wa maendeleo ya kweli ya Zanzibar, hawawezi kutimiza wajibu wao wa kikatiba niliotangulia kuutaja wala hawatoweza kuwawezesha Wazanzibari kutimiza wajibu wao huo

Binafsi yangu sina mashaka na shauku ya mgombea wa akina Polepole kwa maendeleo ya Zanzibar. Lakini mashaka yangu ya msingi, na ambayo naamini anayo kila Mzanzibari mweledi na mwenye shauku ya maendeleo ya Zanzibar, ni juu ya uwezo wake wa kutimiza shauku yake hiyo.

Mashaka ya msimamo wa mgombea wa CCM juu ya maslahi ya Zanzibar

Mashaka hayo yamejengwa, kwanza, na msingi wa akhlaki ya kiuongozi ya mgombea huyo tokea alipopata fursa ya kushika nyadhifa kadhaa za kiserikali na kisiasa.  Katika mazingira ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepitia katika figisufigisu na mivutano mingi ya maslahi ya pande mbili za Muungano na pia juu ya mustakbali wa uongozi wa kitaifa, hasa katika masuala ya ufisadi uliokubuhu. Katika mazingira ya udhalimu wa kijahilia ambao umefanyika Tanzania Bara na Zanzibar wakati yeye akiwa Waziri wa Ulinzi. Katika mazingira ya uendeshaji wa Bunge la Katiba na hatimaye yeye mwenyewe kupiga kura ya kuunga mkono Katiba Inayopendekezwa, ambayo ingeiangamiza Zanzibar kabisa.

Katika mazingira yote hayo, hatujawahi kumsikia akitoa maoni yake, msimamo wake wala hisia zake, isipokuwa kimya kilichoshiba wadhifa. Wazanzibari wasiokuwa na mashaka ni wale tu wenye itikadi kuwa siasa ni kunafikiana – “Mnafiki naye akunafiki, maisha yaendelee!”  Ndio maana wazee wakatupa wasia kuwa: “Sikiliza kwa makini zaidi yale yasiyosemwa!” Yasiyosemwa ndio dhamira ya kweli. Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Margareth Thatcher, aliwahi kusema kwamba yeye aliamua kugombea wadhifa huo kwa sababu wanaume wa Uingereza wana tabia ya kutosema yasiyosemwa na usiposema yasiyosemwa huwezi kuitoa nchi katika mkwamo.

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Kila mtu alitegemea Rais John Magufuli angekuwa rais wa namna gani. Kwa bahati mbaya tu, nadhani, amesahau katika upishi wake. Badala ya kutia chumvi, ameweka magadi. Ndio maana chakula chake hakiliki. Sijui nani anaweza kusema mgombea wa akina Polepole atakuwa rais wa namna gani. Miaka 10 iliyopita imewapa Wazanzibari somo la uzamivu kuwa ukichaguwa mgombea wa kimya utaishia kuguna. Wazanzibari wameitakidi katika subira, lakini bahati mbaya, wamejionea wenyewe kuwa Subira wa zama hizi havuti tena kheri, labda anavuta bangi!!!

Mashaka ya itikadi na uendeshaji wa Muungano

Mashaka ya pili juu ya mgombea wa akina Polepole ni juu ya itikadi ya kisiasa na uendeshaji wa utawala katika Jamhuri ya Muungano.  Wakati fulani mnamo mwaka 2014, waziri mwandamizi na mwanasiasa mwenye dhamana kubwa wa Tanzania Bara, Bwana William Lukuvi, aliwahi kutoa tamko takatifu la ushahidi wa itikadi hiyo akiwa Kanisani.  Naamini hakukusudia.  Kiherehere cha mdomo wake tu kiliisaliti dhamira iliyofichwa moyoni.

Itikadi hiyo ndiyo iliyoipelekea Zanzibar hadi leo kuwa katika madhila ya kukosa uhuru na maendeleo. Madhila ya kukosa sauti ya kuamua hata namna ya kutumia rasilimali zake.  Madhila ya kukosa fursa ya hata kukopa kutoka kwa aliyekuonea huruma na akataka kukukwamua.  Madhila ya kukosa fursa ya kuamua nani awe imamu katika ibada ya kujiletea maendeleo yao.

Kwa dhati kabisa, simuoni mgombea wa akina Polepole kuwa na uwezo wa kukabili changamoto hizo. Ndio maana inabidi kurudi kwa Polepole kumuomba awajibu Wazanzibari masuala ya msingi.  Maana yeye anayejinadi kuwa ataleta maendeleo, ndiye kikwazo cha mwanzo cha mgombea wao.

Maswali ya Wazanzibari kwa CCM

Kwa hivyo, kabla ya Polepole hajaja kuwauzia ghilba ya maendeleo, ni vyema awaambie Wazanzibari wameshindwa nini kuiletea Zanzibar maendeleo tokea 1977 wakati Chama chao kilipoanzishwa hadi leo? Cha muhimu zaidi, awajibu Wazanzibari angalau Masuala 7 yafuatayo kati ya masuala zaidi ya 700 ambayo Wazanzibari wanayo kwa akina Polepole:

  1. Kwa nini walitumia Jeshi mwaka 2015 kupindua matokeo ya Uchaguzi wa Zanzibar? Na kimewashinda nini kuleta maendeleo ya Zanzibar baada ya Mapinduzi hayo wakati Serikali zote mbili wanazitawala wao?
  2. Kwa nini waliamua kuwasafirisha Masheikh wa Uamsho na kuwafungulia mashtaka Tanzania Bara kwa tuhuma za makosa yaliyofanyika Zanzibar? Kwa nini walifanya hivyo, wakati walijua na walikiri katika vikao kuwa jambo hili ni kinyume na Katiba na Sheria za Zanzibar na hata zile za Tanzania Bara? Na ni kinyume pia na maamuzi na maelekezo ya wazi ya Mahkama Kuu ya Zanzibar na Mahkama ya Rufaa ya Tanzania yaliyotolewa katika maamuzi kadhaa. Utaileteaje Zanzibar maendeleo wakati unaidharau na hutambui hata mamlaka yake ya kikatiba?
  3. Kwa nini walitunga Katiba Inayopendekezwa mwaka 2014, ambayo kwa wazi na dhahiri ilikusudia kuiangamiza Zanzibar, kinyume kabisa na mapendekezo ya Rasimu ya Tume ya Warioba? Na kwa nini walikataa katakata kuingiza mapendekezo ya Zanzibar yaliyokusudia kuinusuru Zanzibar hata katika mfumo wa Serikali Mbili uliopendekezwa na rasimu yao?  Miongoni mwa mapendekezo yaliyokataliwa na akina Polepole, na ambayo yalipendekezwa na Kamati ya Mawaziri wa CCM Zanzibar iliyoongozwa na Balozi Seif Ali Idi, ni pamoja na kuondoa kipengele cha kumpa Rais wa Muungano uwezo wa kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na sehemu na pia lile la kuifanya ardhi kuwa jambo la Muungano.
  4. Kwa nini wamekataa katakata hadi leo kuanzisha Akaunti ya Pamoja ya Fedha kama ilivyoamriwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano tokea mwaka 1984 na utaratibu wake kupendekezwa na Tume ya Pamoja ya Fedha tokea Agosti 2006? Akaunti hii ndio itayoweka uwazi ya mapato na matumizi ya Muungano na kuiwezesha Zanzibar kupata haki yake ya mabilioni ya fedha katika mapato ya Muungano. Limbikizo la deni la fedha hizo, ambalo Zanzibar inaidai Serikali ya Muungano, ni matrilioni ya shilingi. Fedha za deni hili zingetosha kuipaisha Zanzibar kiuchumi bila ya kusubiri ghilba za Polepole.
  5. Kwa nini akina Polepole wameshindwa kuiwezesha Zanzibar kupata mkopo wa dola 200 milioni za Kimarekani kwa ajili ya mradi wa bandari ambazo Dkt. Ali Shein alienda kuziomba mwenyewe kwa Rais wa China na kukubaliwa? Mradi wa bandari ulikuwa miongoni mwa vipaumbele vya Ilani yao. Kilichokwamisha kupatikana fedha za mradi huu ni barua tu kutoka kwao akina Polepole.  Benki ya Exim ya China ilishakubali kutoa fedha hizo.  Zanzibar walipokoseshwa fedha hizo, Wachina hao ndio waliosikitika na sio akina Polepole. Walichokifanya akina Polepole ni kuiambia Zanzibar ifanye upembuzi yakinifu mwengine [feasibility study] kwa vile gharama za ujenzi ni kubwa sana. Kufikia hatua ya Zanzibar kupewa barua hiyo ya kuagizwa kufanya upembuzi yakinifu ilichukuwa zaidi ya miaka mitatu.  Suala la nyongeza hapa ni kuwa utafanyaje upembuzi yakinifu, wakati Zanzibar ilishaingia mkataba na Kampuni ya CHEC na kilichobaki ni kutimiza masharti ya awali [conditions precedent]?.  Moja ya masharti hayo ni kuandaa maelezo yakinifu ya masharti na gharama za mradi [employer’s requirement], ambayo ndio njia sahihi ya kupunguza gharama.
  6. Kwa nini akina Polepole wamekataa katakata kuyatoa mafuta katika mambo ya Muungano ili kuiwezesha Zanzibar kuendeleza rasilimali hiyo kwa viwango na taratibu zinazokubalika kimataifa na kibiashara? Kwa nini, badala yake, wamefanya lile walilozowea la ghilba, kwa eti kuipa Zanzibar ruhusa ya kusimamia sekta ya mafuta na gesi asilia, huku wakitunga sheria ya Bunge kusema kuwa utajiri wote wa mafuta ni mali ya Serikali ya Muungano? Wazanzibari wanaifahamu vyema Serikali ya Muungano hata ikivaa nikabu na juba.  Wanaifahamu hata ikihema tu, sikwambii ikitembea au ikiongea.  Wanaifahamu kwamba ni Serikali ya Tanganyika.  Ndio maana hawajawahi kumsikia Rais wa Serikali hiyo akiitaja Zanzibar na nini wameifanyia katika hotuba yoyote ya kufunga Bunge tokea ya Rais Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na ya hivi juzi ya Rais Magufuli. Kama huamini zitafute. Wazanzibari wamezisoma zote na hawajawahi kuona kitu cha namna hiyo.
  7. Kwa nini akina Polepole wameuwa biashara na kudamirisha uchumi wa Zanzibar kwa kuiwekea vikwazo vya kikodi, vya kibiashara, mfumo wa fedha na kuinyima haki zake ndani ya Muungano? Wakitaka ushahidi wa jambo hili, nawaomba wakodi hata Uwanja wa Amani, Wazanzibari wawaletee mashahidi wa jinsi ya dhulma ya kiuchumi wanavyoifanya.

Wazanzibari wanahitaji majibu ya masuali haya kabla akina Polepole hawajaja kuwauzia ghilba nyengine.  Kimebadilika nini mwaka huu ambacho hakikuwepo miaka iliyopita? Mgombea? Sifa, uwezo au aila yake?

Sababu ya kumpa pole Polepole ni kuwa amesahau ile busara ya wazee: “Sikiliza kwa makini yale yasiyosemwa!”

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Bwana Othman Masoud Othman, ni mwanasheria mkuu wa zamani wa Zanzibar, ambaye kwa sasa anaendelea kufanya shughuli zake binafsi kwenye taaluma yake ya sheria.

2 thoughts on “Pole, Polepole! Leave a comment

  1. Acheni kudanganya watu nyinyi ccm kila mnatuletea hila za uongo mpya eti mkitupa nchi tutafanya Maendeleo uongo mtupu acheni wazanzibari wenyewe waongoze nchi yao na mwinyi arudi kwao mkuranga hana uchungu na Zanzibar basi tumechoka kudanganywa na kudhulumiwa

    Like

  2. Ukombozi utatokea kwenu mara umasikini wa fikra na mali vimetawala sana. Wanaume tumekuwa malaya wa siasa na kuahidiwa vyeo na hela. Kila lakheri Wazanzibar

    Like

Leave a Reply