Skip to content

Uzalendo ni kutetea maamuzi ya umma, sio ya kidikteta

Kwa hili la Mfuko wa Ushirikiano kwa Changamoto za Mileni wa Marekani (MCC) na wahisani wengine kujitoa katika kuisaidia Jamhiri ya Muungano wa Tanzania, tusimtafute mchawi ni nani. Uchawi tumejifanyia wenyewe kwani wao walishatoa indhari na mapema ambazo kama tungekua na nia thabiti ya kuzifanyia kazi – hasa kwenye uchaguzi wa Zanzibar na utumiaji mbaya wa Sheria za Makosa ya Mitandao – basi tusingefika hapa tulipo leo hii.

Ni kweli kuwa ni jambo baya kukosa misaada na kuwekewa vikwazo vyengine vya kiuchumi, lakini ni jambo baya zaidi pale maamuzi ya Wazanzibari walio wengi yanapopuuzwa na kulazimisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kishinde kwa hali yoyote ile hata ikafikia kuikanyaga Katiba na sheria zetu wenyewe.

Kinachosikitisha zaidi ni kuwa wananchi wa tabaka la chini ndio walengwa hasa wa hiyo misaada ya wahisani. Anayekaa na akapuuza hili la MCC na la nchi nyengine kujitoa kuisaidia Tanzania, basi ama ni wale ambao hawalipi kodi au ni watumiaji wa hizo kodi za wananchi kwa manufaa yao na familia zao. Watakaoathirika katika haya ni wananchi wa chini, na sio viongozi pamoja na familia zao.

Na Dhamir Ramz
Na Dhamir Ramz

Tujifunze kuwa na uzalendo kwa nchi na sio kuuhusisha uzalendo huo na ulafi wa madaraka ya kisiasa na matakwa binafsi, kwa sababu matokeo yake ni mfano wa haya ambayo yanatokea sasa hivi. Tutake tusitake, bado Tanzania inahitaji kushirikiana na mataifa mengine kwenye kuwaletea wananchi wake maendeleo. Tusijidanganye kwa dhana ya kujitegemea wenyewe, kwa kuwa bado hatuna nia thabiti ya kufanya hivyo kwa vile karibu mfumo mzima wa uongozi umekosa uzalendo wa kulitumikia taifa na badala yake wengi wanatizama matakwa yao binafsi.

Uzalendo hasa ni kuwa na mapenzi ya kweli kwa nchi, na hilo linahusika moja kwa moja na kukubali mabadiliko na kuachiana uongozi kwa kupitia njia za kidemokrasia. Uzalendo hasa sio ubabaishaji, bao la mkono au kuimba “Mapinduzi Daima” na “Muungano Wetu” kwa gharama ya kukiuka haki za kimsingi za raia kujiamulia hatima ya taifa lao. Uzalendo wa kweli ukiwepo utapelekea umoja na uzalendo kwa wananchi na tutaona kasi ya maendeleo inaongezeka kwa vile kutakuwa na ushindani wa kisera kwa vyama vinavyoshika hatamu za nchi, na itapelekea kwa wale wanaoshindwa kuja na ubunifu wa sera zilizo bora zaidi za kuendeleza nchi hii.

Tuwe na wigo wa kuheshimu maamuzi ya wananchi, hasa katika chaguzi. Kufanya hivyo ni kutupeleka katika misingi bora na imara ya demokrasia na kujenga uzalendo wa kujituma kwa kila raia. Siasa za vitisho na kunyang’anya haki za watu zimepitwa na wakati. Tujiulize tutatokaje na mkwamo huu ambao ni matokeo ya kuibeza demokrasia na utumiaji mbaya wa Sheria ikiwemo kuwalenga watu wa kundi fulani pamoja kudhibiti uhuru wa kujieleza?

Historia itatuandika kwa mujibu wa matendo yetu. Anayefanya wema ataandikwa kwa wema wake na anayefanya ubaya ataandikwa kwa ubaya wake. Na pia, utaifa wetu, hata ukifutwa katika ramani ya dunia, utabakia na kudumu katika nyoyo zetu. Anayetetea uzalendo lakini akafumbia macho uhuru na haki ya watu kuamua hatma ya taifa lao ni katika wale ambao historia itawaandika kwa wino mweusi, ishara ya kiza cha matendo yake.

Mungu ibariki Zanzibar na watu wake, Mungu ibariki Tanzania iondokane na siasa chafu na misukosuko ya kitaifa.

Categories

HABARI

Tags

, , ,

Leave a Reply