Skip to content

ZEC kamalizeni kujumuisha matokeo, mumtangaze mshindi – Maalim Seif

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alisema katika vikao vya kuutafutia ufumbuzi mkwamo wa kisiasa Zanzibar vilivyokuwa vikifanyika Ikulu chini ya uenyekiti wa Dkt. Ali Mohamed Shein, kuanzia tarehe 09 Novemba, 2015 walikubaliana kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) haifai tena kuendesha uchaguzi na kujadiliana juu ya namna ya kupata Tume nyengine inayoweza kufanya kazi hiyo.

Hivyo ameelezea kushangazwa na kitendo cha serikali kupitia CCM kuukubali “uamuzi batili wa ZEC wa kutaka kuendesha uchaguzi wa marudio”, akisema hatua hiyo imedhihirisha kuwa viongozi hao hawakuwa na nia njema kwenye mazungumzo hayo yaliyofanyika mara tisa na baadaye kuvunjika bila ya kupatikana muafaka.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi wa CUF Mkoa wa Dar es Salaam katika ofisi kuu za Chama hicho Buguruni Dar es Salaam, ikiwa ni mfululizo wa vikao vyake vya kuzungumza na viongozi wa Chama hicho ngazi wa Wilaya na Majimbo, yenye lengo la kuwaeleza juu ya maafumuzi yaliyofanywa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF ya kutoshiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar.

 Baadhi ya viongozi wa CUF Mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, Ofisi Kuu za Chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi wa CUF Mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, Ofisi Kuu za Chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam.

 

Alisisitiza kuwa kitendo cha kufuta uchaguzi uliokamilika na kutangaza tarehe  nyengine ya marudio ni batili, na kwamba hakuna msingi wowote wa kurejewa kwa uchaguzi huo, kwani “waangalizi wote wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi waliridhishwa na uchaguzi huo kwamba ulifanyika kwa amani, huru na haki”, na kwamba ana matumaini kuwa wataendelea na msimamo wao huo hadi haki ya wananchi wa Zanzibar itakapopatikana.

Katika hatua nyengine, Maalim Seif alimshutumu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Fransis Mutungi, kwa kuunga mkono hoja dhaifu ya ZEC ya kutaka kurejewa kwa uchaguzi wa Zanzibar.

“Kama anaweza kutenda haki asingekubali matokeo ya Urais na Wabunge kwa upande wa Zanzibar, kwa vile uchaguzi huo ulikwenda sambamba na ule wa Zanzibar na kuwashirikisha wapiga kura hao hao, daftari hilo hilo na vituo hivyo hivyo vya kupigia kura”, alisema Maalim Seif.

Kiongozi huyo aliitaka CCM kukubaliana na misingi ya demokrasia ya vyama vingi, na kama hakiwezi ni bora kurejesha mfumo wa chama kimoja. “Msimamo wa CUF ni kwamba hakitambui kufutwa kwa uchaguzi. Tume ya Uchaguzi ikamilishe zoezi la kujumuisha kura kwa majimbo yaliyobakia na hatimaye kumtanga mshindi wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015.”

Aidha Maalim Seif alisema Chama cha Mapinduzi na viongozi wake wamepoteza dira baada ya kutoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kutokana na kubakwa kwa demokrasia Tanzania na hasa Zanzibar.

“Serikali kutaka mabalozi wa nchi za nje na wawakilishi wa Jumuiya za kimataifa wasizungumze na viongozi wa vyama vya upinzini isipokuwa kwa ruhusa ya Wizara ya Mambo ya nje ni kitendo cha aibu.”

Wakati huo huo, Maalim Seif aliwaonya baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaoendeleza makundi ndani ya chama, na kwamba iwapo wataendelea na tabia hiyo watachukuliwa hatua. “Huu ni wakati wa viongozi kuwaunganisha wanachama na wananchi kuwa kitu kimoja na sio kuwagawa kwa misingi ya makundi ya watu wachache.”

Imeandikwa na Hassan Hamad.

Categories

HABARI

Tags

, , ,

Leave a Reply