Skip to content

Kujibakisha madarakani kwa nguvu za dola hakutaisaidia Z’bar

Katika gazeti la Mwananchi toleo la Jumatatu, tarehe 1 Februari 2016, kumechapishwa makala yenye kichwa cha habari: “Shein awaonya wanaofikiria kuleta fujo Zanzibar”, ambapo mwandishi wa makala hiyo, Raymond Kaminyoge, anaandika kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amewatahadharisha wanaojiandaa kuleta vurugu visiwani humo kwamba wasije kuilaumu Serikali kwa hatua itakazochukua dhidi yao.

Akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho kwenye uzinduzi wa sherehe za miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika Kisiwandui Zanzibar jana, Dk Shein alisema: “Tutailinda amani kwa gharama zozote na tutamdhibiti yeyote atakayeleta vurugu… niliambiwa kuna watu wanataka kuleta vurugu, nasema walete hizo vurugu kama wana ubavu.” Alisema CCM itaendelea kutawala Zanzibar licha ya vibaraka wa ndani kutumika kutaka kukiondoa chama hicho madarakani.

Na Muhammad Yussuf
Na Muhammad Yussuf

“Mtaiona hivihivi CCM ikiendelea kutawala licha ya majaribio ya vibaraka kutaka kuing’oa, kwenye nchi nyingi vibaraka wamefanikiwa kuviondoa vyama vilivyoleta ukombozi, lakini kwa Zanzibar mtaiona hivihivi,” alisema, akiwahamasisha wananchi kujitokeza kwenye uchaguzi wa marudio Machi 20.

Kusema kweli, hii ni kauli inayosikitisha sana kutoka kwa kiongozi mkuu wa nchi. Nasema hivi kwa sababu hivi wale maelfu kwa maelfu ya Wazanzibari waliokipigia kura chama cha CUF walikuwa ni vibaraka? Hivi vyama vingapi vilivyoleta uhuru Barani Afrika vimeshaondolewa madarakani mpaka hivi sasa? Ni vingi sana; na walioviondoa kwa njia za kidemokrasia hawakuwa vibaraka, isipokuwa walikuwa ni wazalendo waliotaka mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ya kweli katika nchi zao. Na hapana shaka yoyote ile kuwa hivyo vyama vikongwe vilivyobakia madarakani navyo vitaondolewa tu kwa sababu wananchi wameshachoka navyo; na kwa kuwa havina tena mvutio hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa vimeshindwa kulinda na kutetea maslahi ya wananchi. Ni suala la muda tu; kama si leo, kesho; kwani hakuna kitakachodumu maisha!

Kwa hivyo, kujibakisha madarakani kwa mabavu au nguvu za dola, hakutasaidia kitu; kwani njia pekee ya usalama na amani na yenye kukipatia chama ushindi wa uhakika na wa kishindo katika chaguzi zinazoendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia, haki, usawa na utawala bora, ni uwezo wa chama husika kuvutia nyoyo, hisia na imani za wananchi. Waswahili wanasema hivi: “Nyimbo nzuri humtoa nyoka pangoni”, badala ya vitisho vya kutumia nguvu za Dola.

Kusema kweli, kama nguvu za Dola zingelikuwa zinatosha kuziweka serikali zisizotakiwa madarakani daima milele, basi aliyekuwa Shah wa Iran, Mohammad Reza Palahvi; au Hosni Mubarak, aliyekuwa Rais wa Misri; au Laurent Gbagdo, aliyekuwa Rais wa Cote d’Ivoire; au aliyekuwa Rais wa Burkina Faso, Blaise Campaore; au Rais wa zamani wa Tunisia, Abdulaziz Ben Ally; au Muammar Gaddafi, aliyekuwa kiongozi wa Libya; na wengine wengi; wote hawa wangelikuwa bado wako madarakani hadi hii leo; kwani pamoja na kutumia nguvu nyingi za kupita kiasi za Dola dhidi ya wananchi wao, bado wameondolewa kwa nguvu za umma.

Kwa kujikumbusha tu, miongoni mwa viongozi hao, kulikuwa na wale waliozikimbia nchi zao kwa hiyari yao baada ya kuona kuwa hali ya kisiasa inawageukia; na wengine waliuawa kikatili kabisa kutokana na kung’ang’ania kwao madaraka hadi mwisho. Mwisho wa siku, wote waliondoka madarakani na huku wakiacha maisha katika nchi walizokuwa wakizitawala kwa mabavu yanaendelea kama kawaida; tena bila ya uongozi wao. Na hapa ninakumbushwa na Aya moja ya Qurani inayosema hivi:

“Walayazidu dhalimina illa khassara”.

Sadakta.

Leave a Reply