Skip to content

La mchanga na uovyo wa Muhongo

Rais wa nchi aliyechaguliwa kidemokrasia hawezi kukubalika kwa watu wote anaowaongoza,  ni lazima uwepo upinzani toka upande wa pili. Ikitokea rais akakubalika kwa watu wote kitu demokrasia kitakuwa kimejiua chenyewe. Maana demokrasia ni kama imo kwenye uumbaji wa Mwenyezi Mungu, ndiyo maana aliuachia uasi uwepo dhidi yake wakawa ndio hao wanaoitwa mashetani. Mungu aliumba demokrasia!
 
Nalisema hilo kutokana na kilichojitokeza juma lililopita ambapo Rais Magufuli alikabidhiwa ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza suala la mchanga unaosafirishwa kupelekwa ugaibuni. Jambo hilo lilikuwa likituchanganya sana baadhi yetu, jinsi watu wenye akili timamu wanavyoweza kugharamia mchanga toka Tanzania na kuusafirisha kwenda mabara mengine bila mchanga huo kuwa na kitu chochote cha maana.
 
Wapo baadhi ya watu waliokuwa wakijaribu kulitetea zoezi hilo ambalo limekuja kuonekana kuwa ni zoezi haramu, ama kwa kutokujua au ikiwa ni mbinu ya kuulinda ufisadi mkubwa dhidi ya nchi yetu, wakilitolea maelezo ya kitaalamu kuonesha kwamba lilipaswa kuwepo.
 
Ripoti iliyotolewa na Kamati iliyoundwa na rais ikiwahusisha wasomi na wataalamu waliobobea katika masuala ya madini imeonesha, bila  hisia zozote za kisiasa, kwamba nchi ilikuwa ikiibiwa pesa ambayo inapotajwa ni yule tu mwenye roho ya chuma anayeweza kukosa kububujikwa na machozi!
 
Kumbe nchi yetu, kama alivyosema rais, ilipaswa kuwa inazifadhili nchi nyingine hata zile tunazoziita nchi wafadhili wetu. Tunaogelea kwenye umasikini unaonuka wakati wanaotufadhili wakiupata kwetu utajiri walionao! Hilo ni jambo la kumtoa machozi kila mwananchi aliye na akili timamu.
 
Kwahiyo kwa hapa, bila kujali mambo ya itikadi za kisiasa, nataka nimpongeze Rais Magufuli kwa kuliona hilo, ujambazi ambao nchi yetu imekuwa ikifanyiwa kwa muda wote huo huku yenyewe ikaki masikini, na kulifanyia kazi.
 
Lakini ikumbukwe kwamba kwa kipindi chote tangu upinzani urudi hapa nchini umekuwa ukilisema jambo hilo, lakini ukibezwa na wale wanaoona kwamba kuubeza upinzani ndilo jukumu lao kuu hata kama kwa kufanya hivyo ni kulinyonga taifa lao!
 
Rais Magufuli, akiwa amenuia kabisa kujitenga na hao wanaoweka mbele masuala ya kiitikadi wakiwa wameyaweka nyuma majaliwa ya nchi yao, ameonesha alivyoguswa na wizi huo kiasi cha machozi kumlengalenga, kwa waliomuangalia wakati anakilaani kitendo hicho cha ujambazi ambao nchi imekuwa ikifanyiwa kwa kipindi chote cha kuusafirisha mchanga wenye madini kwenda ughaibuni.
 
Kwa jinsi rais alivyochukia na kuamua kuwatimua kazi mara moja wote wanaohusika na suala hilo imejionesha wazi kwamba amedhamiria kutanguliza uzalendo kwa nchi yake huku masuala ya itikadi za kisiasa akiwa ameyaweka nyuma kama sio kuyasahau kabisa.
 
Mfano tuliona namna alivyoeleza kiungwana katika kutengua uteuzi wa waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Kasema kwamba huyo ni rafiki yake na anampenda sana, vilevile tunajua kwamba ni kada mwenzake katika chama tawala, lakini akasema kwamba kwa suala hilo ilibidi profesa huyo ajipime kama anafaa kuendelea kuwa kwenye nafasi hiyo. Uzalendo mbele urafiki baadaye.
 
Najua yatajitokeza yale ya kwamba wakati Muhongo anakalia nafasi hiyo tayari mchanga huo wa madini ulishaanza kusombwa na kupelekwa ughaibuni. Kama zipo fikira za aina hiyo inabidi tuwe wawazi kama alivyokuwa rais wetu, kwamba hizo ni fikira za kipumbavu.
 
Sababu mtu hawezi kuwekwa kwenye nafasi ya ulinzi, kuwazuia na kuwakamata wezi, halafu akawaachia wezi waendelee kuiba kwa madai ya kwamba hao kawakuta tayari wanafanya wizi. Tuseme yeye anataka awakamate wezi wapya tu!
 
Tunaweza kuona kwamba Dk. Magufuli ni mpya zaidi katika nafasi yake ya urais kuliko Muhongo kwenye Wizara ya Nishati na Madini. Maana profesa huyo alishakuwa waziri wa wizara hiyo katika kipindi cha awamu ya nne chini ya Dk. Jakaya Kikwete kabla ya kulazimika  kuachia ngazi kwa kashfa nzito.
 
Sasa iweje Magufuli aione kashfa ndani ya wizara hiyo wakati Muhongo aliyeishaikalia wizara hiyo haioni? Hapa moja kwa moja tunaweza kuona kwamba sio tu Muhongo alikuwa akiijua kashfa hiyo bali alidhamiria kuiendeleza na kuikuza baada ya kurudishwa kwa mara ya pili.
 
Fikira zinazonijia ni kwamba si ajabu, kwa ukaidi na kiburi alivyonavyo Muhongo, angeweza kusema kwamba migodi yote ya wawekezaji wa nje ifungwe kusudi ubaki kusombwa mchanga wenye madini na kupelekwa ukachambuliwe kule wanakotoka wawekezaji!
 
Kama alivyosema rais hao ndio wataalamu tuliowasomesha kwa pesa zetu, badala ya kuzirudisha pesa hizo kwa njia ya uzalendo wakihakikisha zinarudi pamoja na faida, wao wanataka hata kile walichokitumia kuipata elimu waliyonayo kiishie kuiangamiza nchi!
 
Nilishaandika nikimlalamikia Profesa Muhongo kuhusu utendaji wake, maana  yeye anajiona ni mtu mwenyewe uelewa wa kila kitu kuliko mtu yeyote mwingine, lakini mara nyingi anayoyafanya yanaonekana kuelekea kusababisha madhara kuliko kile kinachotegemewa toka kwake.
 
Mfano kuna kipindi alilazimisha bwawa la Mtera lisifunguliwe kumwaga maji yanayozidi kipimo kilichowekwa na wataalamu waliolijenga. Wataalamu walisema ilikuwa kidogo bwawa hilo libomoke na kusababisha garika kubwa pamoja na hasara ya kulijenga upya kwa pesa ambazo nchi haikujiandaa nazo kwa sasa.
 
Jambo ninaloweza kumshauri Rais Magufuli asikubali kuvutwa na sifa za udakitari wala uporofesa anapoteua watendaji. Sifa hizo ni za kinadharia zitumikazo madarasani, ni sifa za kwenye makaratasi, wala siyo za kiutendaji. Wapo watu wengi wanaouweza utendaji uliotukuka bila sifa hizo.
 
Profesa ni mwalimu tu, kinadharia, sio lazima awe mtendaji mzuri. Mfano mzuri  wa karibu ni huu wa Profesa Muhongo. Kuna watu walioikalia wizara hiyo ya Nishati na Madini iliyomshinda Muhongo lakini wao wakaiendesha kwa mafanikio makubwa.
TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Prudence Karugendo. Anapatikana kwa anwani ya barua pepe  prudencekarugendo@yahoo.com na simu nambari 0784989512

Leave a Reply