Skip to content

Khalifa Hatfar: Kibaraka wa Marekani au mwokozi wa Libya?

MMOJA wa wapashaji wangu wakuu wa habari za Libya nilipokuwa mhariri wa gazeti la Africa Analysis jijini London alikuwa mtu ambaye aliponipigia simu kwa mara ya mwanzo alijitambulisha kwa jina la “Abdallah”.  Alikataa kunambia jina lake la pili.

Nilikuwa nikizungumza naye mara nyingi kwa simu alipokuwa na habari za kunipa au nilipokuwa na maswali ya kumuuliza. Mara chache tukionana uso kwa macho.  Miaka nenda miaka rudi sijapata kumshikilia anitajie majina yake kamili.

Nikijuwa kwamba kwa vile alikuwa mpinzani kutoka Libya lazima alikuwa anachukua hadhari yasije yakamfika yaliyowafika wapinzani wengine wa kiongozi wa Libya, Muammar Qadhafi.  Nikikumbuka ya alasiri ya Ijumaa ya Aprili 11, 1980, pale Yusuf Hassan, mtangazaji wa BBC, ambaye kwa sasa ni mbunge wa Kamukunji, Nairobi, Kenya, aliponipigia simu ofisini mwangu na kunipa pole.

Siku hizo nilikuwa mhariri wa Afrika na Mashariki ya Kati kwenye jarida la Index on Censorship. Nilimuuliza Yusuf pole za nini? Akanijibu: “Kwani hujasikia? Rafiki yako Ramadan amepigwa risasi punde hivi msikitini na amekufa.”

Ramadan alikuwa ni Mohammed Mustafa Ramadan, mtangazaji wa Idhaa ya Kiarabu ya BBC aliyekuwa mpinzani wa Qadhafi. Alipigwa risasi na kuuliwa baada ya sala ya Ijumaa alipokuwa anatoka msikiti mkuu wa London ulio Regents Park. Ingawa alikuwa rafiki na mtani wangu sikujuwa kwamba alikuwa kitisho kikubwa hivyo kwa watawala wa Libya kiasi cha kuwafanya wamtoe roho.

Nikiyakumbuka mauaji ya Ramadan nilimwachia “Abdallah” aendelee kuwa “Abdallah” mpaka siku moja miaka kadhaa baada ya kujuana aliponambia: “Leo ntakwambia. Jina langu si Abdallah. Jina langu ni Ashur Shamis”.

Baadaye baada ya kuulizauliza na kuunganisha hili na lile, ndipo nilipotambua kwamba Ashur alikuwa zaidi ya mpinzani wa kawaida dhidi ya Qadhafi. Alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa vuguvugu la National Salvation Front (NSF) lililokuwa likijiandaa kumpindua Qadhafi.

Vuguvugu hilo lilikuwa na jeshi lililokuwa likiongozwa na Khalifa Haftar, huyuhuyu Khalifa Haftar, kichwa mchungu, ambaye sasa amejibandika cheo cha Field Marshal na aliyekuwa akileta upya vurugu Libya tangu Aprili 3 mwaka huu majeshi yake yalipoanza mashambulizi yakiulenga mji mkuu wa Tripoli.

Lengo lake ni kuuteka mji wa Tripoli na kuing’oa serikali ya waziri mkuu Fayez al Sarraj yenye kutambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Sijapata kukutana na Haftar. Waliowahi kukutana naye wanasema kwamba anaonyesha kuwa ni mtu mpole. Mmojawao amesema kwamba amekaa kama mwalimu wa skuli mstaafu licha ya sifa yake ya ukatili na ubabe.

Takriban wote waliokutana naye karibuni wanasema kwamba mwenyewe anajiona kuwa ni pekee anayeweza kuiokoa Libya.  Amewaambia aliokutana nao kwamba kila aliyezungumza naye Libya alimwambia kwamba wanataka mtu wa kuwaokoa na mtu wenyewe ni yeye.

Swali ambalo wengi nje ya Libya wanajiuliza ni: ni nani hasa huyu Khalifa Haftar?

Wasifu wake unaonyesha kuwa si mtu wa kuchezewa. Ulimi wake tu unazichapa lugha zisizopungua tano: Kiarabu, Kiingereza, Kirussi, Kitaliana na Kifaransa.  Hivi sasa akiwa na miaka 76 aliingia jeshini akiwa kijana kabisa na alishiriki katika mapinduzi ya Al Fateh yaliyoongozwa na Qadhafi na yaliyompindua Mfalme Idris pamoja na aila ya kifalme ya al Sanussi katika 1969. Wapinduzi hao vijana waliupindua ufalme bila ya kuua mtu wala kumwaga damu.

Ingawa Haftar alikuwa mdogo wake Qadhafi kwa mwaka, Qadhafi aliwahi kusema kwamba Haftar alikuwa kama mtoto wake.  Haftar alisomea mambo ya kijeshi kwanza kwao Libya katika Chuo cha Kijeshi cha Benghazi ambako ndiko alikofunzwa Qadhafi pia.  Baadaye Haftar alipelekwa kwa masomo zaidi katika Muungano wa Sovieti na Misri.

Kwa muda mrefu Haftar alikuwa mtu wa karibu sana na Qadhafi. Ni yeye aliyepewa dhamana ya kuyaongoza majeshi ya Libya yaliyopelekwa Misri 1973 kusaidia kulikomboa eneo la Sinai lililokuwa limeshikiliwa na Israel. Baadaye Haftar aliteuliwa na Qadhafi awe mkuu wa majeshi ya Libya.

Usuhuba wa Haftar na Qadhafi ulianza kuharibika baada ya Qadhafi kumpeleka Kanali Haftar Chad 1986 kwenda kuwaongoza wanajeshi wa Libya katika vita baina ya Chad na Libya. Haftar aliingia mtegoni waliotegewa na majeshi ya Chad kwa msaada wa Marekani. Yeye na wanajeshi wake wasiopungua 700 walitekwa.

Qadhafi alivimba kwa hasira. Akamkanya na kumtema Haftar pamoja na wanajeshi wake. Lililomkera na kumtia ghadhabu ni kwamba Haftar na mateka wenzake wa vita walikuwa waache mapigano kwa vile Qadhafi alikuwa amekwishatia saini makubaliano ya kuyaondoa majeshi ya Libya kutoka Chad. Kuendelea kwa Haftar na wanajeshi wake kuwako Chad kuliyavunja makubaliano hayo.

Baada ya kushikiliwa wakiwa mateka wa vita Qadhafi alishikilia kuwa Haftar na wanajeshi wake warudishwe Libya. Marekani ilikataa na badala yake ikawapeleka Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo).  Huko nusu yao walitaka kurudi Libya lakini Haftar na baadhi ya wanajeshi wengine wakaamua kujiunga na vuguvugu la NSF la kina Ashur Shamis.

Vuguvugu hilo likiungwa mkono na Marekani na lilikuwa na lengo la kumpindua Qadhafi. Juni 1988 Haftar alitangaza kwamba vuguvugu lao limeunda jeshi chini ya uongozi wake. Nadhani fikra ya kutaka kuwa mtawala wa Libya ilimwingia akilini tangu wakati huo.

Marekani iliposita kuipa Zaire msaada wa fedha Rais Mobutu Sese Seko wa Zaire aliwafukuza wanajeshi waliosalia wa Haftar na akawapeleka Kenya walikoruhusiwa kuishi kwa muda.

Mwaka 1990 Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, lilifanya mpango wa kuwaingiza Marekani Haftar pamoja na wanajeshi wake wapatao 300 wakiwa wakimbizi. Kufikia 1996 Haftar alishiriki katika njama ya kumpindua Qadhafi kwa kuchochea uasi katika milima ya mashariki mwa Libya lakini jaribio hilo halikufanikiwa.

Haftar akarudi Washington, Marekani, alikokuwa akiishi na alikopewa uraia wa nchi hiyo. Baadaye alihamia Virginia karibu na makao makuu ya CIA.

Haftar aliyaunga mkono majaribio kadhaa ya kutaka kumpindua na kumuua Qadhafi lakini mara zote majaribio hayo yalishindwa.  Baadaye Haftar aliziacha siasa za upinzani na alianza kusikilizana tena na Qadhafi ingawa hakurudi kwao.

Shamis amewahi kusema kwamba akimuona Haftar akiishi vizuri akiwa Washington lakini hakujua akipata wapi fedha. Uvumi uliopo ni kwamba akifadhiliwa na shirika la CIA lililokuwa likimtumia.

Haftar alirudi Libya 2011 kwenda kuyaunga mapinduzi yaliyomtoa Qadhafi madarakani akifikiria kuwa ataibuka kuwa mkuu wa majeshi ya Libya mpya. Hilo halikuwa. Alipewa cheo cha uluteni jenerali lakini alikuwa wa tatu katika uongozi wa jeshi. Alinuna akafunga virago na kurudi Marekani akisema kwamba anakwenda “kucheza na wajukuu” zake.

Haftar alirudi tena Libya Februari 2014. Hivi sasa kuna serikali mbili nchini humo. Kuna ile ya Tripoli yenye kutambuliwa na Umoja wa Mataifa ambayo Haftar anataka kuipindua. Na kuna iliyo Tobruk, mashariki mwa nchi hiyo, yenye kuongozwa na Jeshi la Kitaifa la Libya likiwa chini ya Haftar.

Mwanzoni hiyo ya Tobruk ndiyo iliyokuwa ikitambuliwa kimataifa mpaka palipopatikana Maridhiano ya Kisiasa ya Libya mnamo 2015.

Libya ilianza kusambaratika tangu Qadhafi auliwe Oktoba 20, 2011. Kuwako kwa serikali mbili zenye kuhasimiana kumezidi kuichafua nchi hiyo yenye majeshi mingine kadhaa ya mgambo, baadhi yao yakiiwakilisha mitandao ya kigaidi.

Haftar anaishtumu serikali ya Tripoli kuwa imejaa magaidi na amekuwa akidai kwamba lengo lake ni kuwapiga vita magaidi wote wenye kufuata mielekeo mikali ya Kiislamu kama vile wafuasi wa Dola ya Kiislamu (Islamic State) au Al Qa‘eda.  Amekuwa akishtumu kwamba wote wenye kuingiza dini katika siasa ni magaidi wakiwa pamoja n ahata wafuasi wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu (Jami’yat al Ikhwan al Muslimin).

Huwa anasahau au labda anajisahaulisha kwamba wengi wenye kumuunga yeye mkono ni watu wenye  kufuata misimamo ya Kisalafi ya vuguvugu la Madkhali, lenye kuingiza dini katika siasa. Vuguvugu hilo linajikita juu ya maandishi ya mwanachuoni wa Kisalafi Rabee al Madkhali wa huko Saudi Arabia.

Kwa sasa Haftar anaungwa mkono na Saudi Arabia, Misri,  Muungano wa Falma za Kiarabu (UAE), Urussi, Ufaransa na hivi karibuni Rais Donald Trump wa Marekani amejitokeza hadharani kumuunga mkono.

Trump ameubadili msimamo wa awali wa Marekani tangu ianze duru hii ya pili ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe huko Libya.  Hapo mwanzo sera rasmi ya Marekani ilikuwa kuwa na hadhari na Haftar.

Februari 7 mwaka huu, kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani katika Afrika (AFRICOM), Jenerali Thomas Waldhauser, aliishambulia Urussi kwa kujiingiza katika mzozo wa Libya upande wa Haftar.  Kuna ushahidi kwamba Urussi na Ufaransa zimekuwa zikimpelekea Haftar wanajeshi wa kukodi na washauri wa kijeshi huko Benghazi. Imekuwa pia ikimsaidia kwa kumpelekea vifaru ya kijeshi, mizinga, ndege za droni na marisawa.

Kuna ushahidi kwamba mshauri mmoja mkuu wa Rais Vladimir Putin wa Urussi, Yevgeny Prigozhin, anayejulikana kwa lakabu ya “mpishi wa Putin” amekuwa akihusika katika kadhia ya kumsaidia Haftar. Kuna kampuni moja ya Kirussi inayosemekana kumsaidia Haftar kwa kumtengenezea sarafu ili kuisaidia kifedha sehemu ya Libya Mashariki.

Urussi, Ufaransa na Marekani ni wazi kuwa zinayarandia mafuta ya Libya. Visima kadhaa vya mafuta mashariki na kusini mwa nchi vimo mikononi mwa wanajeshi wa Haftar.

Kwa upande wao, Saudi Arabia, UAE na Misri hazitaki pawepo serikali ya kidemokrasia ya mwelekeo kama wa Udugu wa Kiislamu nchini Libya. Zinahisi kuwa serikali aina hiyo itawapa funzo baya wananchi wao.

Haftar anataka madaraka tu ya kuwa kiongozi mbabe wa nchi yake. Nafikiri huo uchu wake wa madaraka ndio utaomuangamiza.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ahmed Rajab na kuchapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 24 Aprili 2019. Mwandishi anapatikana kwa baruapepe:aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Leave a Reply