jump to navigation

Uchumi

WAZANZIBARI NA MAFUTA YAO, WATANGANYIKA NA MADINI YAO!!

Licha ya kuwa suala la uchumi si la Muungano, lakini zile nyenzo zote za kuusimamia na kuuendesha uchumi huo zimehodhiwa na kudhibitiwa na Serikali ya Muungano – kodi, mikopo, biashara ya nje, uwekezaji, na sasa hata hili suala la uwezekano wa kuwepo kwa nishati ya mafuta. Ni wazi basi, kwamba kama Wazanzibari hawakujikaza, itafika siku Zanzibar itakuwa haina tena lake wala chake. Msimamo ufuatao, uliotolewa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ni muhimu kwa khatima ya Zanzibar na lazima tuunge mkono…

SAID ALI MBAROUK, CUF GANDO

SAID ALI MBAROUK

“TPDC (Shirika la Maendeleo ya Mafuta la Tanzania), chombo ambacho kilianzishwa mwaka 1969 kikiwa si chombo cha Muungano na mpaka hivi leo hakijawa chombo cha Muungano, lisijishugulishe kabisa na masuala ya mafuta Zanzibar. Badala yake, Zanzibar nayo ianzishe kampuni yake iitwe Zanzibar Petroleum Development Corporation (ZPDC). Hii (ZPDC) ijishughulishe na utoaji wa leseni na usajili wa makampuni na shughuli nzima ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta kwa Zanzibar. Utaratibu utafanywa ionekane kwamba kampuni yetu ZPDC inashirikiana na TPDC katika ama masuala ya kimataifa au masuala mengine, lakini bado Zanzibar iwe na kamandi ya kutosha katika masuala mazima ya mafuta. ” – Said Ali Mbarouk

RASHID SEIF SULEIMAN, CUF ZIWANI

“…Hata misguiding inatokea. Bahati mbaya siye tumepewa muda mdogo, lakini mimi nimetazama humu kwenye ile ripoti ya Antrim, imeandikwa kuwa TPDC ni kitengo cha Muungano. Iko wapi TPDC (kwenye Mambo ya Muungano?), lakini kwenye ripoti imeandikwa. Kwa hivyo kuna mambo mengi, kama tutayapitia, yametajwa kuwa ni ya Muungano wala si ya Muungano. Na ile lugha ilitomika vile vile katika kurekebisha TPDC, hata kama tungekuwa twataka (hilo la TPDC na mafuta kuwa jambo la Muungano, tuseme), lakini haiwezekani to employ, to change to nini… Kitu kama hichi ambacho si cha Muungano, lazima utumie neno lenye uzito unaofaa – restructuring. Sisi tunasema, kama mafuta yapo ni yetu, kama hayapo basi. Tunasamehe!” - Rashid Seif Suleiman

ZAKIA OMAR JUMA, CUF VITI MAALUM

“….Suala la mafuta si suala la Muungano, kwanza. Na katika masuala haya, Articles of Union ni International Agreement ambayo kiilivyo Mkataba huu ni mkubwa kuliko hiyo Katiba ya Jamhuri ambayo imeambiwa isitiwe mkono au katiba nyengine yoyote katika nchi husika kwa ule Mkataba wake. Kwa hivyo, ninaamini kabisa ingelikuwa ni vyema ukaangaliwa ule Mkataba – ambao bado unawekwa siri, sijui kwa sababu zipi – akapewa huyo mshauri, akajuwa kwamba hayo mambo yenyewe yakoje katika suala hili, ili akaona kazi yake inarahisika vipi. Kama mfano ambao Mhe. Rashid ameutoa, huwezi kwenda mahala pana foundation imejengwa ya nyumba pengine very simple, ukaambiwa ujenge sky scraper. Huo usalama utakuweko wapi?” – Zakia Omar Juma

HAJI FAKI SHAALI

HAJI FAKI SHAALI

“Sasa suala linakuja: hapa ndipo hadaa ilipotumika katika Muungano. Katika Muungano wa 1964 ulipofanyika, ilichukuliwa ile Katiba ya Tanganyika ikarekebishwa ili kutoa nafasi kwa Zanzibar nayo kuwemo. Sasa nadhani hii ni wrong. Miye nadhani, kama hata hayo makubaliano yatakuwepo, basi sheria iandikwe upya na sio ukachukua sheria ya upande mmoja, ukairekebisha ifanye kazi pande mbili. That is wrong!” – Haji Faki Shaali

SOUD YUSUF MGENI

SOUD YUSUF MGENI

“Sasa katika nchi hii, hakuna mtu wala chombo chenye mamlaka ya kubadilisha Mkataba wa Muungano. Makubaliano ya Muungano ni makubaliano ya nchi mbili. Wanaobadilisha ni wale wale ambao waliounda Mkataba wa Muungano. Si chombo. Bunge la Jamhuri ya Muungano, kisheria, halina mamkala ya kubadilisha Articles of Union. Baraza la Wawakilishi halina mamlaka ya kubadilisha Articles of Union. Articles of Union hubadilishwa na wale wale ambao walianzisha Articles of Union, nchi mbili Tanganyika na Zanzibar. Kwa hivyo, mambo yote yale ambayo Bunge lilichukuwa mamlaka ambayo si yake ya kuingiza mambo katika Articles of Union kuwa ni ya Muungano, mimi nasema yale yote ni batili na hatuyakubali.” – Soud Yussuf Mgeni

 

HAMAD MASOUD HAMAD, CUF OLE

“Kila nchi ilikuwa na ghala yake. Waheshimiwa, waasisi wa Muungano huu, wakachukua mambo kutoka ghala moja ya kila nchi – mambo 11 – wakayaweka katika ghala moja. Mheshimiwa, kutokea hapo kila kinachochukuliwa kutoka ghala moja, ni kutoka ghala ya Zanzibar na linaingizwa katika ghala ya Muungano kiasi ambacho sasa yamefikia mambo 23 wa ushei. Ninavyoona mimi ni kwamba itakuja siku ghala yetu haina kitu kwa sababu kila kinachochukuliwa, kinachukuliwa kutoka kwetu…” – Hamad Masoud Hamad

ABOUBAKAR KHAMIS BAKARY, CUF MGOGONI

“Lakini hata tuseme – na mimi nakataa – kwamba suala na mafuta na gesi ni suala la Muungano. Sasa kama hivyo ndivyo, mbona katika ripoti hizi au ushauri huu tunaopewa, haujazungumzia chochote kuhusu gesi? Na kwa nini hawa wenzetu wakakarupuka tu wakasema sisi tunataka kuwe na mshauri elekezi ambaye atazungumzia mgawanyo wa mapato ya uchimbaji na utafutaji wa mafuta? Ni kwa sababu mafuta haya yanatoka Zanzibar tu lakini kwa gesi ambayo haiko Zanzibar hawashughuliki? Hicho ni kitawi kimoja tu ambacho nahisi kuna ajenda ya siri; na ajenda ya siri yenyewe ni dhahiri kwa sababu ikiwa gesi ambayo karibu tangu 2000 inachimbwa na inatumiwa kwenye viwanda – ripoti niliyonayo ni kwamba takriban viwanda 20 hivi sasa katika Bara wanatumia gesi inayochimbwa katika maeneo mengine. Fedha ambazo zimeshakusanywa ni zaidi ya shilingi bilioni 100. Sasa kama kweli hili ni suala la Muungano, kwa nini hawa wenzetu hawakusema kwamba suala hili nalo liingizwe katika mchakato huu, likazungumziwa suala la mafuta ambayo hata kuanza kuchimbwa hayajachimbwa? – Aboubakar Khamis Bakary

NAJMA KHALFAN JUMA (CUF NAFASI MAALUM)

“Basi miye naomba, wataalamu mumwambie mtaalamu alokuja: Zanzibar hata kama mafuta ni kinibu ni ya Wazanzibari. Waandishi habari waambieni huku katika magazeti ya kesho, kwamba wawakilishi wa Wazanzibari, wa wananchi wa Zanzibar, nchi ya Zanzibar, mafuta yao hawataki, ni ya Wazanzibari kwa ajili yetu tuliopo hivi sasa, watoto wetu wetu walioko nyuma yetu, wajukuu wetu wajao, vitukuu, vilembwe, vinying’inya mpaka Zanzibar itakapokwisha. Wasije wakatugeuza Nigeria, vita vya kila siku. Hatuviwezi wala hatuvitaki. Siye ni wachache na watuwache na utajiri ambao Mwenyezi Mungu atatujaalia.” – Najma Khalfan Juma

Chanzo: http://hakinaumma.wordpress.comTAFADHALI BONYEZA HAPA KUCHANGIA MAONI YAKO. UNASHAURIWA KUANDIKA MADA YA KILE UNACHOKICHANGIA.

Comments

1. MAALIM - July 27, 2008

Uchumi wa Zanzibar ni marehemu na arubaini tayari umeshasomwa huo ndio ukweli.Uchumi ni Bank,Uchumi ni bandari,Uchumi ni anga,Uchumi ni mamlaka ya kukusanya kodi lakini hayo yote – Zamani Tanganyika imeshainyakulia Zanzibar uwezo na mamlaka sasa sijui niseme nini kuhusu uchumi wa mama yetu Zanzibar

2. MAALIM - August 6, 2008

Mimi bado nasema uchumi wa nchi yetu ya JAMHURI YA WATU WA WANZIBAR.Umefikishwa pahala pabaya sana ndani ya dimbwi la umasikini na Tanganyika ingawaje ni umesikini wa kujitakia !!kusudi haimbiwi pole kwa ajuae lakini kwa asie jua huambiwa pole. Mimi nawapa pole Wazanzibari wenzangu hasa walipata fahamu kamili kuanzia 1965/6 kwani miaka hiyo kujia nyuma sitaki niseme neno la zaidi ya ZENJ EMPIRE kiuchumi na kisiasa lakini baada ya hapo mambo yakaanza kwenda shaghala baghala na leo nchi yetu ndio didididi tubwi. Lakini kawaida ya tubwi huwa shahada mara 3 hii ni mara ya 3 na ya 4 huwa ndio tubwi na mshindo yamjaaliwae tena nataka niseme Wazanzibari bado hii ya 4 nayo ni 2010 tukiikosa hapo nchi yetu ya Zanzibar ishaangamia na kutokomea.Tujifunze mara ngapi kwani?

3. atoya - September 16, 2008

uchumi imara hujengwa na miundo mbinu imara,
miundo mbinu imara hujengwa na viongozi imara. haya basi na tujiulize kama uchumi wetu si imara tatizo nnini? miundo mbinu si imara, tatizo nnini? viongozi si imara!!! hili ndo jibu la maswali yote!
hebu tuamke wazanzibari tubadili hawa viongozi ili tubadili na mustakabali wa maisha ya wazanzibari wote.
shime 2010 wasirudi hawa, ata sijui niwaiteje. maana watu ni wasikiao, waonao, na wenye kufikiri. sie twafa njaa wao watwambia uchumi unkua.


Sorry comments are closed for this entry