Mkataba upitiwe kuondoa kero za Muungano August 16, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.1 comment so far
Joseph Mihangwa
SIKU chache kabla ya uhuru wa Tanganyika, wakati wa chakula cha mchana mjini Dar es Salaam, Rais wa kwanza, Mwalimu Nyerere, alinukuliwa akisema maneno yafuatayo juu ya Zanzibar: “Kama ningeweze kukivuta kisiwa kile mpaka katikati ya Bahari ya Hindi, ningefanya hivyo. Kwa kweli sitanii; nina wasiwasi kitatuletea matatizo makubwa sana huko mbeleni”.
Ingawa Mwalimu hakufafanua alimaanisha nini kwa maneno hayo, lakini inafahamika kihistoria kwamba, Zanzibar, licha ya udogo wake, siku zote ilionekana korofi mno kwa watu wa bara kuliko ilivyostahili hata ukatungwa ule usemi kwamba, “Zumari likipigwa Unguja, Afrika Mashariki yote lazima icheze”; au kwamba “Zanzibar inapopiga chafya, Bara hupata mafua”.
Miaka minne baadaye tangu Mwalimu atamke maneno hayo, Tanganyika na Zanzibar ziliungana kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, 1964 chini ya Mkataba wa Kimataifa ujulikanao kama “Hati ya Muungano” [Articles of Union], uliotiwa sahihi na marais wa nchi hizo mbili – Mwalimu Nyerere na Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964.
Ingawa Muungano huu ulielezwa kuwa wa hiari [jambo ambalo linapingwa na baadhi ya watu], ukorofi wa Zanzibar ulizidi kumwandama Nyerere huku akituhumiwa kuongoza mkakati wa siri, kwa Zanzibar kumezwa na Tanganyika kiasi cha kumkatisha tamaa.
Kuna wakati Rais Karume aliwahi kumwambia Mwalimu kuwa Muungano [huo] ni kama koti tu; mtu akiona linambana ana hiari ya kulivua wakati wowote, kwa maana kwamba muungano huo sio ndoa ya kudumu inayowafanya wanandoa kuwa mwili mmoja.
Naye Mwalimu, katika hali ya kukata tamaa, mwaka 1969 alisema: “Kama watu wa Zanzibar wakiona kwamba Muungano hauwafaidii kitu, na kama kweli watu wa Zanzibar wanaona hivyo, mimi siwezi hata kidogo kuwaua wananchi wa Zanzibar. Kama waliingia katika Muungano kwa hiari yao, wanaweza pia kujitenga kwa hiari yao. Hatukuishinda Zanzibar vitani….”
Hii inathibitisha kwamba Mwalimu hakulazimisha Muungano kuendelea, kama inavyodhaniwa na Wazanzibari wengi. Nao Wazanzibari, licha ya kupewa mwanya wa kujiengua kama waliona inafaa kufanya hivyo, waliona ni ngoma nzito, lakini wakaendeleza ukorofi usio na maana, kama tutakavyoona baadaye.
Pengine ni kwa msimamo huo wa Nyerere na ukorofi wa Zanzibar, kwamba gazeti la The Economist la Uingereza lilidai katika makala yake yenye kichwa cha habari “Hatari za Nyerere”, kwamba “Nyerere alimudu nusu tu ya kazi [ya kumeza] ya chatu; alifanikiwa kuimeza Zanzibar, lakini hakuzivunja nguvu zake [ukorofi] kwanza. Kwamba mnyama huyo, mzima – mzima angali anayeyushwa tumboni na uchungu wa mateke yake unaonekana ndani kabisa ya siasa za Tanganyika na unaweza ukaua”.
Maneno haya, yanayoelezea baadhi ya matatizo ya Muungano wetu, yangali hai na yenye nguvu hadi leo; ambapo uchungu wa mateke ya Zanzibari ni dhahiri na unatishia kuvunja Muungano.
Mapema mwaka 2004, Zanzibar ilitoa teke la kituko cha kudai na kujipatia bendera yake ya Taifa, Wimbo na Nembo ya Taifa. Serikali ya Muungano ikashindwa kuhimili teke hilo na Zanzibar ikajitangazia ufalme.
Kana kwamba hayo hayakukidhi ufalme huo, mwaka uliofuata, Zanzibar ikadai na kujichukulia hadhi ya kuiwakilisha kama nchi katika Shirikisho la Mpira barani Afrika [CAF], wakati huo huo ikaendelea kudai kujiunga kama nchi, katika Shirikisho tarajiwa la kisiasa Afrika Mashariki [EAF].
Hivi karibuni, Zanzibar imezua kizaazaa kingine cha kuliondoa suala la maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa, kutoka kwenye mambo ya Muungano, na Serikali ya Muungano imeshindwa kukemea hatua hiyo ya Baraza la Wawakilishi [Bunge] la Zanzibar ya kuvunja Katiba.
Na katika kuonyesha kwamba Serikali ya Muungano haina uhakika au kutouamini muundo wa sasa wa Muungano, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameliambia Bunge hivi karibuni kwamba, njia pekee ya kumaliza kero za Muungano ni kwa nchi hizi mbili kuunda Serikali moja makini bila kuelezea aina ya muundo wa sasa, udhaifu wake na kwa nini Serikali haijachukua hatua kurekebisha mapungufu ya Muungano.
Kigugumizi hiki cha nini? Hadi lini tutavumilia mateke makali ya Zanzibar tumboni?
Hati ya Muungano ndiyo msingi na mhimili mkuu wa Serikali ya Muungano. Hati hii ni sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Serikali ya Mapinduzi na haiwezi kubadilishwa, kuongezwa au kupunguzwa nje ya kusudio la awali la wale waliotia sahihi mkataba huo na kuridhiwa na mabunge ya nchi hizi mbili.
Suala la mafuta ni kati ya mambo 12 mapya ya Muungano ambayo hayakuwamo katika mambo 11 asilia. Kwa maoni ya wengi ni kwamba mambo hayo yameongezwa kinyemela bila kuzingatia Mkataba wa Muungano, na kufanya idadi ya mambo ya Muungano kufikia 23!
Hapo ndipo ilipo hoja ya Wazanzibari kwamba, nchi yao inazidi kunyofolewa viungo vyake na Serikali ya Muungano wakati inachotakiwa kuchangia ndani ya Muungano ni mambo 11 tu ya mwanzo, kwa mujibu wa Mkataba.
Kuna ukweli ndani ya hoja hii, kama tu tutaamua kuheshimu Mkataba wa Muungano. Ndiyo maana Serikali ya Muungano inashikwa kigugumizi kila mara Zanzibar inapojinyakulia mambo yaliyoingizwa kinyemela katika Katiba ya sasa ya Muungano, nje ya yale ya mwanzo.
Kwa jinsi tunavyowafahamu wenzetu wa Visiwani, tusifikiri kwamba wataishia na bendera ya Taifa na suala la mafuta pekee; bali tuna hakika wataendelea kudai kurejeshewa au kujinyakulia mambo yote 11 yaliyobaki, na Serikali ya Muungano isiwafanye kitu.
Ukweli uko wazi; kwamba Tanganyika na Zanzibar zilipoungana kwa mambo 11 tu, Sheria za nchi hizo ziliendelea kuwa na nguvu kwa mambo yote yasiyo ya Muungano, [ibara ya 4 na 5 Mkataba wa Muungano], na kwamba Serikali za Tanganyika na Zanzibar hazikufutika, wala haikuelekezwa kwamba zifutike [Tazama ibara 25 (i) Katiba ya Muda, ya 1965].
Kwa mujibu wa ibara 6 (a) na (b) ya Mkataba wa Muungano, kutakuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye atasaidiwa na Makamu wa Rais wawili, mmoja kutoka Zanzibar ambaye ndiye Rais wa Zanzibar, na mwingine kutoka Tanganyika, pamoja na mawaziri na maofisa wengine wa serikali atakaoteua kutoka serikali za Tanganyika na Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais ndiye Msaidizi wa Rais wa Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano nchini Zanzibar, na ndiye pia mwakilishi wa Serikali ya Zanzibar katika Bunge la Muungano.
Makamu wa Pili wa Rais ndiye Msaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mambo 11 ya Muungano upande wa Tanganyika, na pia ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali katika Bunge la Muungano. [Angalia ibara ya 3 (a) – (b) Mkataba wa Muungano; na ibara 13 Katiba ya 1965].
Kilicho wazi hapa ni kwamba, kuteuliwa kwa Mwalim
u Nyerere kama Rais wa kwanza wa Muungano mwaka 1964, bila kuachia nafasi ya urais wa Tanganyika kulimfanya awe Rais wa Jamhuri ya Muungano na pia Rais wa Tanganyika ambayo haikufa; ingawa hapakuwa na kizuizi kwa Rais mwingine au Waziri Mkuu kuchaguliwa kuongoza Serikali ya Tanganyika, na Nyerere akabakia Rais wa Muungano pekee [Angalia ibara ya 12 Katiba ya muda, 1965].
Haikuwa sahihi kwa Kamati iliyoteuliwa kupendekeza Katiba ya 1977 kukiuka matakwa hayo ya Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano ya 1964, ambao ndio mhimili mkuu wa Kikatiba kwa Muungano na Serikali zake mbili na ambao hauwezi kubadilishwa na mtu au chombo chochote cha Serikali.
Vivyo hivyo, uteuzi wa Tume iliyoteuliwa kupendekeza Katiba ya 1977 inayotumika sasa haukuzingatia ibara ya 7 (b) ya Mkataba wa Muungano iliyotaka iteuliwe Tume itakayoteuliwa itokane na maridhiano kati ya Rais wa Zanzibar na Rais wa Muungano, jambo ambalo halikufanyika; badala yake Tume hiyo iliteuliwa kwa misingi ya vyama vya siasa vya TANU na ASP wakati mambo ya vyama vya siasa hayakuwa ya Muungano.
Tunaamini kwamba, muundo wa Muungano wenye serikali tatu ndio uliokusudiwa. Ndiyo maana Mkataba wa Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muda ya Muungano ya 1965, ziliendelea kutambua kuwapo kwa Sheria na Serikali za Tanganyika na Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano tu wakati na baada ya siku ya Muungano. Mabadiliko yaliyofuata, ama kupitia Amri za Rais [Presidential Decrees] au Katiba ya 1977, kwa heshima zote, yanakiuka Mkataba wa Muungano.
Haya ndiyo yaliyokuwa mawazo ya mwanzo ya Waasisi wa Muungano wetu kwani, Juni 5, 1963, mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar, viongozi wa Kenya, Tanganyika na Uganda walikutana mjini Nairobi kuzungumzia uundaji wa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki [EAF] ambapo wazo kuu lilikuwa ni kuunda Serikali ya Shirikisho kwa mambo kadhaa tu kwa kuanzia, na nchi hizo kuendelea kusimamia mambo yake mengine.
Kufuatia Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, na kufuatia Kenya na Uganda kughairi wazo hilo, Tanganyika na Zanzibar ziliamua kuungana kwa mfumo na muundo ule ule uliokusudiwa na EAF kama hatua moja kuelekea EAF.
Hili linathibitishwa pia na Balozi wa Marekani Visiwani Zanzibar, Frank Carluci; ambaye katika simu yake ya maandishi kwenda Washington, Aprili 23, 1964, siku moja tu baada ya kutiwa sahihi kwa Mkataba wa Muungano, aliripoti akisema: “Karume ametia sahihi Mkataba wa Muungano akiamini kwamba ni wa kuunda Shirikisho lenye serikali tatu”.
Mwalimu anaonekana kushabikia pia muundo huo. Katika makala yake ndefu kwenye gazeti la Africa Forum [Vol. 1, No. 1 la 1965] alisema: “Mfumo bora wa Muungano [wowote] ni ule wa Shirikisho wenye kuwa na Serikali ya Muungano na Serikali za nchi zinazoungana, kila moja ikibakia na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano”.
Mawazo haya ya Mwalimu yamesisitizwa tena katika kitabu chake “Uhuru na Umoja” [Freedom and Unity”, ukurasa wa 300 – 304. Kama ni kweli Nyerere aliyaasi mawazo yake ya awali juu ya muundo huu, basi ni bahati mbaya, kwani kwa kufanya hivyo mzimu wa mawazo hayo uliendelea kumtesa kwa kiapo chake cha kutokubali kugeuka “jiwe”; na ndivyo hivyo mateke ya Zanzibar yatakavyoendelea kutuumiza kwa kung’ang’ania muundo tofauti usiotekelezeka..
Baada ya kung’atuka urais mwaka 1985, Mwalimu alikuwa wazi kwa hili pale alipokiri kwamba, muundo wa sasa unafaa ujadiliwe, kuondoa utata, hata kama yeye alikwishatoa msimamo wake.
Kati ya wajumbe 11 wa Tume ya Jaji Nyalali ya kupendekeza mabadiliko ya Katiba kutoka Bara, tisa walitaka Shirikisho na wawili tu ndio waliotaka muundo wa sasa uendelee.
Na kati ya wajumbe 11 wa tume hiyo kutoka Zanzibar, saba walitaka muundo wa sasa uendelee lakini ufanyiwe marekebisho, watatu walitaka Shirikisho na mmoja hakuwa na msimamo.
Vivyo hivyo, hoja iliyoshindwa ya kikundi cha Wabunge 55 wa Bunge la Muungano (maarufu kama G55) ya kutaka kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika mwaka 1993, ni ushahidi mwingine kwamba muundo wa sasa una matatizo.
Pia kwamba haueleweki na umepotoshwa kwa maslahi ya kisiasa, kiasi kwamba matatizo yake, ambayo kusema kweli ni ya kikatiba, tunajaribu kuyatatua kwa njia za kisiasa badala ya Kikatiba. Kwa hiyo tunajaribu kutibu mara kwa mara dalili za ugonjwa badala ya kutibu ugonjwa wenyewe.
Wala pendekezo la Waziri Mkuu Pinda la kutaka kuundwa kwa serikali moja alilolitoa bungeni hivi karibuni, na ambalo limepokelewa kwa hasira kali na Wazanzibari wengi, si suluhisho sahihi kwa kero za Muungano.
Si suluhisho kwa sababu linataka kufanyika mjadala mpya wa Muungano, tofauti na uliokusudiwa.
Kama isingekuwa ubinafsi wa wanasiasa wetu wanaonufaika na mgogoro huu wa kisiasa kwa upotoshaji na utekelezaji mbaya wa Muungano, suluhisho pekee la kero hizi lingekuwa ni kupitia upya Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano kuona kilichokusudiwa ndani ya Hati hizo na kukitii na kukiheshimu kwa ukamilifu.
Tutavumilia mpaka lini mateke haya machungu ya Wanzanzibar?
CCM, CUF Pemba kimeeleweka vitambulisho August 16, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.add a comment
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), Ofisi ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi, zimekubaliana kubadili utaratibu wa uandikishaji wa vitambulisho na sasa utafanyika shehia kwa shehia na kwa tarehe maalumu kuanzia Jumatatu ijayo.
Hatua hiyo inatokana na utaratibu wa awali ambao uliwalazimu wananchi baada ya kuchukua fomu katika shehia zao kufika ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ambako walikuwa wakipata vitambulisho hivyo.
Akizungumza jana mjini hapa, Ofisa Tawala wa Wilaya ya Wete, Khamis Juma Silima, alisema makubaliano hayo yalifikiwa juzi kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa CUF, Khalifa Mohammed Issa na Kaimu Katibu wa CUF wa Wilaya, Haidary Ali Abdallah.
Wengine waliohudhuria ni Katibu wa CCM wa Wilaya, Said Abdallah Suluhu na Mhazini wa CCM, Ramadhan Issa Kipaya na Mkuu wa Idara ya Vitambulisho Pemba, Hamad Shamata Hamad.
Watakaohusika kujiandikisha ni wenye vyeti vya kuzaliwa, na wakishapata vitambulisho hivyo watajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambalo uandikishaji wake umesitishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutokana na vurugu zilizojitokeza wakati wa uandikishaji.
Kulingana na ratiba hiyo, inaonesha kuwa Jumatano na Jumanne wiki ijayo uandikishaji utafanyika shehia za Kambini na Kiuyu Minungwini, wakati siku mbili zinazofuata itakuwa Kiuyu Kigongoni na Ole. Agosti 21 na 22 itakuwa Mjini Ole na Kangani, wakati siku mbili baadaye itakuwa Piki na Mzambarauni Takao, huku Agosti 26 na 27 itakuwa Mtambwe Kusini na Kaskazini.
Agosti 28 na 29 itakuwa Kisiwani na Limbani na Agosti 31 na Septemba mosi itakuwa Jadida na Kipangani, wakati Septemba 2 na 3, itakuwa Pandani na Selemu na siku mbili zitakazofuata itakuwa Utaani na Bopwe. Kwa mujibu wa ratiba, Septemba 7 na 8 itakuwa Kizimbani na Fundo, siku mbili zitakazofuata, itakuwa Gando na Ukunjwi, huku Junguni na Mchangamdogo ikiwa ni Septemba 11 na 12.
Kulingana na ratiba hiyo, Maziwani na Kojani A itakuwa Septemba 14 na 15, ambapo siku mbili zitakazofuata, itakuwa Kiungoni na Pembeni, ambapo Shengejuu na Mpambani itakuwa Septemba 18 na 19 na shughuli hiyo itahitimishwa Septemba 25 na 26 kwa shehia za Chwale na Kinyikani.
Hata hivyo licha ya ratiba hiyo, bado jana kulionekana baadhi ya wananchi wakiwa katika makundi wengine waking’ang’ania kutaka wapewe vitambulisho hivyo kwenye ofisi hiyo hiyo ya Mkuu wa Wilaya.
Utaratibu wa awali ingawa ulikuwa mzuri, lakini ulipata upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CUF waliodai una usumbufu mkubwa na kuzua zogo, kwamba baadhi ya wananchi wananyimwa fomu za kuandikishwa hasa wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa.
Hata hivyo Jumanne wiki hii, akizungumza katika mkutano na viongozi wa kisiasa, masheha na baadhi ya watendaji wa Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohammed Juma Ame, aliwataka wasio na vyeti vya kuzaliwa waende mahakamani waape na kupewa fomu za kuandikishwa.
Uandikishaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi ulianza mwaka 2005, lakini baadhi ya wananchi walikuwa hawajitokezi kuchukua fomu kwa vile masuala ya Serikali yamekuwa hayapewi kipaumbele kisiwani hapa na hayaungwi mkono.
Pemba asilimia kubwa ni wafuasi wa CUF. Lakini baada ya kutolewa tamko kwamba wasio na vitambulisho hawataingia kwenye Daftari, sasa mwamko umekuwa mkubwa, kila mtu akitaka kujiandikisha na kusababisha vurugu katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya, ambazo ndizo zinatoa vitambulisho, wakati shehia zinatoa fomu za kupata vitambulisho hivyo.
SMZ yakasirishwa na utafiti ulioonyesha Seif kinara Z`bar August 16, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.4 comments
Kampuni ya Utafiti ya Synovate Steadman imepewa wiki mbili na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iwe imeomba radhi kwa hatua yake ya kudai kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ndiye anayekubalika zaidi kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa 2010.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alisema kampuni hiyo imefanya kitendo cha utapeli cha kuidanganya SMZ.
Alisema kampuni hiyo iliwasilisha ombi la kufanya utafiti katika barua yake ya Mei 18, mwaka huu kuhusu hali ya uchumi na utamaduni Tanzania na kupewa kibali na ofisi yake.
Alisema kampuni hiyo ambayo imesajiliwa Tanzania na kupewa namba ya usajili 32692, imefanya kinyume chake kwa kwenda kuandika mambo ya siasa na kuonyesha kuwa Hamad anaongoza kwa kukubaliwa na wananchi kwa asilimia 28 na kuwaacha wanasiasa wengine wa CCM.
Ripoti ya kampuni hiyo, ilielezwa kwamba Hamad anaongoza akifuatiwa na Dk. Mohammed Gharib Bilal mwenye alama 24, Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha alama sita na Dk. Ali Mohammed Shein alama mbili.
“Serikali inaipa muda wa wiki mbili kuomba radhi kupitia vyombo vile vile vilivyotumika kupotosha, vinginevyo haitapewa kibali kingine chochote kufanya shughuli zake Zanzibar,”, alisema Hamza.
Kwa uapnde wa Jamhuri ya Muungano utafiti huo ulionyesha Rais Kikwete anakubalika zaidi na ana nafasi kubwa ya kutetea nafasi ya urais akifuatiwa na Mwenyekiti wa Chadema , Freeman Mbowe namba tatu ikishikwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Hamza alisema mazingira ya Zanzibar ni tofauti na Tanzania Bara, kwa vile Zanzibar ni nchi ndogo na wananchi asilimia 60 damu zao zimejaa siasa, hivyo utafiti huo ulipaswa kuwa wa kina na kusimama kwenye mizani ya ukweli.
Alieleza kwamba uhuru wa kutoa maoni unaotolewa na serikali unapaswa utumike vizuri na sio kuwapotosha wananchi na kwamba tayari SMZ imepokea maombi mengine ya kampuni hiyo ya kutaka ifanye utafiti mwingine wa mawasiliano, lakini alisema bila ya kutekeleza agizo hilo haitapatiwa ruhusa.
CHANZO: NIPASHE
SMZ sasa yaikemea ulaya August 16, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.add a comment
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeionya Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU) na mabalozi kutoingilia kabisa mambo ya ndani ya visiwa hivyo na kuponda matokeo ya utafiti kuhusu mbio za urais wa Zanzibar mwaka 2010.
EU pamoja na nchi 10 za barani Ulaya na Amerika Kaskazini, zilionya dhidi ya kasoro zilizojitokeza kwenye zoezi la uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kuitaka SMZ kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuondoa kasoro hizo kwa kuwa zinasababisha kukiukwa kwa demokrasia.
“SMZ haiongozwi kwa kumwogopa mtu au kwa shinikizo lolote, ina katiba yake na sheria zinazosimamia masuala mbalimbali na upana mkubwa wa maendeleo ya demokrasia,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alipoongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana.
Waziri huyo alisisitiza kuwa, SMZ ina utawala wake kamili, ikiwa ni pamoja na sheria inayosimamia uchaguzi iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi kama chombo cha kutunga sheria.
“Hatuongozwi na EU wala AU (Umoja wa Afrika). Sisi ni nchi yenye kuheshimu sheria zake na kufuata utawala bora, demokrasia na kuheshimu haki za binadamu. EU wanatakiwa wafanye utafiti wa kutosha huko Pemba kabla ya kutoa shutuma,” alionya.
Alieleza kuwa, mazingira ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura kisiwani Pemba, yanakwamishwa na wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaowachochea wafuasi wao wavunje na kukiuka sheria, jambo ambalo alidai kamwe halitavumiliwa na vyombo vya serikali.
Zoezi hilo lilisitishwa kutokana na wananchi kulipinga wakidai kuondolewa kwa kigezo cha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kuwa ndio sifa kuu ya kuandikishwa kupiga kura. Wananchi wanadai kigezo hicho kinapingana na katiba ya Zanzibar ambayo inamtambua mtu yeyote mwenye nyaraka nyingine zinazomtambulisha kuwa ni Mzanzibari.
Hata hivyo, Waziri Juma alimtupia lawama nyingi katibu mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad na kumtaja kuwa mmoja wa watu waliofanya mikutano ya hadhara ya uchochezi ili kuhatarisha amani katika kisiwa cha Pemba.
“Serikali haitamtazama na kumvumilia mtu yeyote ambaye ataamua kuvunja na kukiuka sheria. Vitambulisho vya ukaazi vinatajwa katika sheria ya uchaguzi, hivyo kila anayetaka kuandikishwa ni lazima awe na sifa ya ukaazi wa miaka mitatu mfululizo,” alisema.
Kuhusu matokeo ya utafiti wa kampuni ya Synovate ambayo yalionyesha kuwa Maalim Seif ndiye anayeweza kumrithi rais wa sasa, Amani Abeid Karume atakapostaafu mwakani na kufuatiwa kwa karibu na Mohamed Gharib Bilal, waziri huyo alipingana na ripoti hiyo.
Alisema Synovate iliwasilisha maombi Ofisi ya Waziri Kiongozi ili ifanye utafiti juu ya masuala ya kiutamaduni na kiuchumi, lakini kwa makusudi imekiuka taratibu na kufanya utafiti wa kisiasa kinyume na ombi lao la msingi.
Waziri Juma alisema, Juni 18 mwaka huu kampuni hiyo iliwasilisha barua ikiomba kufanya utafiti juu ya masuala ya hali ya kiuchumi na kiutamaduni na siyo kutafuta kura ya maoni kuhusu mbio za urais mwaka 2010 na kuupotosha umma.
“SMZ inaitaka kampuni hiyo kuomba radhi kupitia vyombo vya habari kuhusu upotoshaji wa habari uliofanyika kwamba, Seif Sharif Hamad ndiye anayekubalika kwa nafasi ya urais wa Zanzibar,” alisema.
Alisema kwa kukiuka mantiki ya ombi lao la awali katika kuendesha kwao utafiti walioukusudia, ni wazi kampuni hiyo itakuwa imeidanganya serikali, Ofisi ya Waziri Kiongozi na kuupotosha umma.
Alipotakiwa ataje athari zinazoweza kusababishwa na matokeo ya utafiti huo, alisema zimeutikisa mfumo wa siasa za Zanzibar na pia kuwapotezea mwelekeo na matarajio watu wenye kiu ya kuwania urais.
“Hata naibu katibu mkuu wa CUF, Juma Duni Haji, pengine alikuwa na nia ya kuwania urais ili ashindane na Seif, inawezekana amekatishwa tamaa, lakini pia si msingi wa ombi la kampuni husika, bali kilichofanyika ni hadaa,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Juma alibainisha kuwa, SMZ kamwe haitamkamata Maalim Seif Sharif Hamad na kumweka korokoroni licha ya madai ya kufanya uchochezi wa makusudi, ambao alisema ni kosa la jinai.
Alisema Maalim Seif anachochea wafuasi wake ili wavunje sheria na kusema atazidi kufanya hivyo bila kuchoka kwa kutegemea akamatwe ili apate umaarufu wa kisiasa.
“Hatuna mpango wa kumkamata Maalim Seif na kumfikisha kortini. Yule atamalizika kidogo kidogo mpaka wananchi watampuuza. Ni jamaa yetu; mwenzetu; analipwa masilahi yake na SMZ, hakuna wa kumkamata na kufanya hivyo ni kumjenga,” alisisitiza.
Siasa chafu za urais zaanza Zanzibar August 16, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.add a comment
Na Salma Said, Zanzibar
KINYANG’ANYIRO cha Urais wa Zanzibar kinazidi kupamba moto, baada ya watu wasiojulikana kusambaza vipeperushi kuelezea sifa za mtu anayepaswa kuchaguliwa mwakani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Watu hao ambao walikuwa wakipita mitaani maeneo yenye watu wengi kwa pikipiki, walisambaza vipeperushi hivyo vilivyoeleza sifa saba za ziada za rais mbali na zilizotajwa katika katiba na kanuni za CCM. “Kwa kuwa kumejitokeza dalili za kuonekana vitendo vya makusudi kudhoofisha dhana nzima ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 hivyo tunataka mtu mwenye uchungu na Mapinduzi, atakayelinda na kuyaendeleza,” moja ya vipeperushi hivyo vimesema.
Kingine kimesema “Kwa kuwa kumejitokeza vitendo vya makusudi vya kudhoofisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Tunataka mtu mwenye uchungu na Muungano na atakayelinda na kuuimarisha.” Vipeperushi hivyo vimesema mtu anayepaswa kuwa rais wa Zanzibar anatakiwa kuwa mwenye uwezo wa kukemea na kuwapa adhabu viongozi walio chini yake wakati wanapokiuka maadili na aoneshe uwezo wa kujenga umoja wa Wazanzibari na Tanzania Bara.
“Pia tunahitaji kada ambaye anakijua chama, jumuiya zake na ambaye atakiongoza chama kwa uadilifu na hatakibeza; na mwenye uzoefu wa utendaji kazi ndani ya chama na serikali zake. “Tunataka achukie vitendo vya wizi wa mali ya umma, ubadhirifu na ufisadi, awe amepagawa na roho mtakatifu na asiwe anapagawa na roho mtaka vitu na asiyeonyesha dalili za kulipiza kisasi kwa viongozi waliopita,” vimesema vipeperushi vingine.
Vipeperushi hivyo vimesambazwa kama kampeni za uchaguzi huo zilizokwishaanza chini chini ndani ya CCM ambako baadhi ya watu wameanza kupigana vikumbo kumrithi Rais Amani Karume.
Wanaotajwa kuwania nafasi hiyo kumrithi Rais Karume ni Waziri Kiongozi wa zamani wa Zanzibar, Gharib Mohamed Billal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Kiongozi wa SMZ, Shamsi Vuai Nahodha, na Naibu waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna.
Wengine ni Mohamed Seif Khatib, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Rais (Muungano), Haroun Ali Suleiman, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa SMZ na Mohamed Aboud, Naibu Waziri wa Afrika Mashariki ( SMT ), Hussein Mwinyi waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye ni mtoto wa rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, na mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Ali Karume (ni mdogo wa rais wa sasa).
Wakati huo huo, pamoja na kuionya Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU) na mabalozi kutoingilia mambo ya ndani ya Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeialika Jumuiya hiyo na mabalozi kuzungumza na Rais Amani Abeid Karume. Juzi SMZ iliitaka EU na mabalozi kutoingilia mambo ya ndani ya visiwa hivyo baada ya jumuiya hiyo ya Ulaya na Amerika kuonya kasoro zilizojitokeza kwenye zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura na kuzitaka serikali za pande zote mbili kuhakikisha zinamaliza kasoro hizo.