Ajali ya meli: Maalim Seif azitaka mamlaka ziwajibike May 30, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.trackback
Na Salma Said, Zanzibar
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amezitaka mamlaka za usafirishaji na mawasiliano chini zilizo chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwajibika ili kuipa heshima serikali ya Amani Karume mbele ya umma kutokana na uzembe uliopelekea kutokea kwa ajali ya Meli ya MV Fatihi jana usiku kisiwani Unguja.
Kwa kauli hii, bila shaka, Maalim Seif anamgusa moja kwa moja Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa SMZ, Machano Othman Said, akimtaka aanze kujiuzulu wadhifa wake akifuatiwa na maafisa wengine katika mamlaka husika.
Maalim Seif ametoa tamko hili leo mara baada ya kutembelea eneo la ajali na kupata maelezo mafupi toka kwa maofisa wa Shirika la Bandari la Zanzibar, akiwemo Mustafa Jumbe ambaye ni mkurugenzi wa shirika hilo.
Maalim Seif amesema ni jambo la kusikitisha kuona hata taarifa za usafirishaji abiria zikiwa hazifahamiki wala idadi ya abiria waliokuwemo ikikanganya akili na zaidi meli hiyo inaaminika ilikuwa mbovu.
Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema siku chache zilizopita meli hiyo ilikuwa ikitoka Pemba na kulazimika kushusha abiria bandari ndogo ya mkokotoni kabla ya kutia nanga katika bandari ya Maalindi na hadi sasa haijaelezwa wazi kama tatizo lilikuwa nini na kisha ianze kubeba tena abiria.
“Vyombo vilivyo husika vilichukua hatua gani ya kuhakikisha meli hii sasa ni nzima na inafaa kuchukua tena abiria na kusafiri majini,tuna mashaka pengine mamlaka husika hazikuchukua hatua sahihi.”
Aidha ameilalamikia hatua ya meli hiyo kupata ajali ikiwa bandarini lakini zikakosekana juhudi za haraka za kitaalam za kuokoa maisha ya abiria na mizigo yao na mamlaka zinazohusika kutojaribu kunusuru hali hiyo ya taharuki.
“Hata pale walipotokea wasamaria wema waliokuwa tayari kutaka kujitolea kusaidia kutokana na uzoefu walionao walikatazwa na hivyo kuchukua muda wa takriban saa nane hadi wazamiaji kutoka kikosi cha KMKM kufika bandarani.”
Katibu Mkuu huyo wa CUF amesema hiyo ni hatari katika nchi na jamii ingetazamia sana kuwepo kwa kikosi kilichoandaliwa vyema kimafunzo kwa masjanga ya uokoaji hapo bandarini kusaidia kulihami janga hilo .
“Tunaiotoka serikali kwanza ichukue hatu za dharura ili kuhakikisha hakuna mtu aliyebaki, na kama kuna maiti zipatikane na familia zao wakazike, mamlaka zinazosimamia usafiri ziwajibike na usalama wa vyombo ufahamike kabla ya kuanza safari katika kubeba abiria na mizigo.”
Aliongeza kusema kuwa kuyafumbia macho masuala kama hayo wakati wake umepita na sasa ni lazima wanaohusika wawajibike ili kujenga nidhamu ya uwajibikaji kutokana na dhamana walizobebeshwa na serikali.
Hata hivyo, Maalim Seif alisema Serikali ya Muungano pia ilitakiwa iweze kusaidia kutoa misaada yao, lakini hakuna dalili za serikali hiyo kushiriki katika uokoaji huo.
Wakati akiondoka bandarini, Rais Karume aliulizwa serikali yake inachukua juhudi zipi alisema hata wapinzani nao ni sehemu ya serikali hivyo haiyumkini kuuliza serikali inachkua hatua gani kwa sasa.
“Serikali ina mamlaka zake. Majumuisho wake ndiyo unapata serikali. Kila mtu ni serikali hata wewe mwandishi ni serikali. Hata hawa wapinzani.” (huku akimuonyesha kidole chake Maalim Seif kuwa ni sehemu ya serikali).
Rais Karume na Maalim Seif, wote, kwa nyakati tofauti, walitoa salamu za pole kwa wafiwa na kuwatakia majeruhi wote katika ajali hiyo wapate uzima haraka ili washiriki katika kazi za kimaendeleo.
assalam aleykum
napenda kutoka tanzia kwa raia wenzangu wa afrika ya mashariki kwa janga hili na huu ni mtihani kutoka kwa rabbi,ila wazee wamesema YASINI NI DAWA HELA NAMBIO UWE NAZO hii nikimaanisha kuwa kuna watu wazembe inabidi wawajibikie kwani hili pia :uzembe: umechangia katika hili.
tuwe pole kwa hili ndigu zangu.