SMZ imeshindwa kutimiza ahadi January 30, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.1 comment so far
Na Salma Said, Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekiri kushindwa kutimiza ahadi zake zilizotoa katika kikao cha baraza la wawakilishi kuwa wananchi hawatalipa maji hadi hapo maji yatakapoweza kutoka bila ya kusita kwa muda wa masaa 24.
Hayo yameelezwa na Waziri na Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansoor Yussuf Himid alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi wa Jimbo la Mkanyageni (CUF) Haji Faki Shaali aliyetaka kujua kwa nini wananchi wanalipishwa maji wakati serikali iliahidi kutowalipisha.
“Ni kweli nikiri hilo la ahadi ya serikali kuwa hatutalipisha hadi pale maji yatakapotoka kwa masaa 24 tuliahidi humu katika kikao cha baraza la wawakilishi wakati tulipoleta mswaada wa maji kwa asilimia kubwa hilo tumeshindwa kulifanikisha lakini naomba wajumbe mfahamu” alisema Waziri Himid.
Alisema wizara yake imewaagiza mamlaka ya maji hivi sasa kupita kila shehia kutoa elimu ya ulipaji wa maji huku kiwango cha shilingi 4,000 kwa mwezi kilichokuwa kililalamikiwa kimeanza kufanyiwa mapitia kutokana na malalamiko ya wananchi.
Alisema wafadhili wasingeweza kuisaidia serikali ya Zanzibar kama isingeweza kuchangia fedha katika miradi ambayo wanataka kusaidiwa.
Alisema Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa kuanzia utaanza na wafanyabiashara wakubwa kuwatia mita za kulipia maji na abaadae watafuatia wananchi wa kawaida kwa kuwa gharama za mita hizo ni kubwa na zinagharimu fedha nyingi.
Akijibu swali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Nungwi (CCM) Ame Ussi Juma aliyetaka kujua ni busara gani inayotumika katika kuwalipisha wananchi maji hali ya kuwa hayatoki katika majumba yao huku hali duni za wananchi zikiwa hazijazingatiwa.
Waziri Himid alisema maji ni muhimu na kama ni huduma inatakiwa alipishwe yule anayoipata tu lakini katika hali ya sasa ya Zanzibar kuwa changamoto kubwa inayoikabili wizara ya amji juu ya kuainisha kwa kina nani anapata huduma hiyo ya nani hapati.
Alisema na jambo hilo linatokana na ukweli kwamba watumiaji wote wa maji wajumbani hawajafungiwa mita, hivyo inapelekea utata wa wanaopata na wasiopata wote kuwa mwenye kundi moja.
Kutokana na hilo alisema mamlaka ndio ikasambaza bili kwa nyumba zote za mkoa wa mjini magharibi ili kutumia fursa hiyo kufanya uchambuzi wa kina juu ya suala hilo.
Hata hivyo alisema sera ya maji ya Zanzibar ambayo ilipitishw ana baraza hilo la waawakilishi imeeleza kwa kina juu ya viwango vya kutahmini nani ameshafikiwa na huduma hiyo na nani bado.
Alisema sera hiyo imeeleza kuwa serikali itafahamu kuwa imeshawahudumia wananchi endapo watakuwa na uwezo wa kupata huduma ya maji sio zaidi ya umbali wa mita 250 kwa vijiji na mita 150 kwa mijini
Alisema kwa nia ya kutowakandamzia wananchi wira ya maji imeamua na kutoa taarifa kwa wananchi kuwa wanaopaswa kulipia huduma hiyo ni wale wneye kupata huduma hiyo na waliokuwa hawajafikiwa na huduma hiyo wasilipe.
Waziri Himid alisema sekta ya huduma za maji ulimwenguni kote zinapotaka kuweka viwango vya malipo zinatakiwa kuzingatia mambo makuu mawili nayo ni kuweza kurejesha gharama za uendeshaji na kurejesha gharama za uchakavu wa miundo mbinu.
Alisema kutokana na hali ya uwezo wa wananchi wa Zanzibar pamoja na ugeni wa kuchangia huduma hiyo kwa muda mrefu wizara ilizingatia zaidi mambo hayo kwa kuchukua tahmini ya sensa ya kipato cha majumbani ya mwaka 2005 inayofanywa kupitia mtakwimu mkuu wa serikali.
Aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo kuwa kwa mujibu wa kipato cha mtu wa kawaida kwa mwezi kina uwezo wa kulipa shilingi 3,750 kwa huduma ya maji tu, ambapo kwa mujibu wa kima cha chini cha mshahara wa mfanyakazi wa serikali sio zaidi ya silimia 5 ya kipato cha mwezi ndio kinachoweza kulipia huduma hiyo amabzo ni shilingi 4,000 na wizara hiyo ilifikia kutoza fedha hizo chini ya misingi hiyo.
Mafuta ni mali ya Wazanzibari – SMZ January 30, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.add a comment
Na Salma Said, Zanzibar
Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansoor Yussuf Himid amewataka wajumbe wa baraza la wawakilishi kuondosha wasi wasi na wajitayarishe vyema kuipokea ripoti ya Mshauri Mwelekezi kutoka Norway hivi karibuni.
Akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae (CCM) Mahmoud Thabit Kombo aliyetaka kujua ukweli upo wapi baina ya serikali ya muungano kusema hakuna amfuta na serikali ya Zanzibar kusema mafuta yapo.
“Mheshimiwa Spika mimi nataka kujua maana juzi nimemsikia Waziri Mheshimiwa Malima akisema Zanzibar hakuna mafuta huku mheshimiwa waziri Mansoor anatakwambia mafuta yapo na sasa nataka kujau ukweli upo wapi” aliuliza Kombo ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.
Waziri Himid alisema hakuna teknolojia yenye uhakika kwa mia kwa mia inayofahamu kuwa mafuta Zanzibar yapo hayapo isipokuwa mwelekeo wa kupata maguta Zanzibar upon a jambo hilo litajulikana iwapo utafutaji na ushimbaji mafuta utaanza rasmi.
” Hao wanaosema hakuna mie nasema hakuna technology ya 100% lakini ninachoweza kusema ni kuwa uwezekano wa kuwepo mafuta Zanzibar upo na hilo tutalijua zaidi tukianza kuchimba sasa ikiwa tutapata kinibu, geloni au pipa hayo yatakuwa ni maumuzi ya wazanzibari kama mafuta kidogo tutajipaka na kama gesi kidogo basi tutanusa, kule Tundauwa Pemba mafuta yanakuja yenyewe ” alisema Himid.
aliwataka wajumbe wa baraza la wawakilishi na wananchi kwa ujumla kuacha kubabaishwa na taarifa mbali mbali zinazotolewa na watu pamoja na vyombo vya habari kuhusu mafuta na uwezekano wa kupatikana visiwani hapa.
“Ninachoomba kwa sasa wajumbe mjiandae kuipokea ripoti ya mshauri mwelekezi na kumshauri mwelekezi atakapotoa ripoti yake ninaamini wajumbe wana ushauri mzuri na wa hoja nzuri sana tuna wataalamu wengi hapa tafiti zinaonesha kwamba upo uwezekano wa kupatikana kwa mafuta kwa mujibu wa mazingira ya jiografia ya bahari yetu” alisisitiza Waziri huyo.
Alisema hatma ya suala la mafuta na gesi pamoja na mgawanyo wake utajulikana katika kikao cha baraza la wawakilishi kijacho ambapo suala la mafuta litajadiliwa kwa kina ili kila mzanzibari ajione amewakilishwa katika kikao hicho ambacho kitaamua maamuzi yenye maslahi na wazanzibari wote kiuchumi.
Aliwataka wajumbe wa baraza la wawakilishi kujiandaa na majadiliano hayo kwa kujenga misingi ya hoja katika suala hilo muhimu kwa maslahi ya taifa na kizazi kijacho.
Akijibu swali la msingi lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani (CCM) Ali Suleiman Ali aliyetaka kujua serikali imejiandaa vipi katika suala zima la kudhibiti uharibifu wa mazingira wakati wa uchumbaji wa mafuta ukiwadia.
Waziri Himid alisema katika mikataba, suala la mazingira limepewa umuhimu wake kama kampuni itaharibu mazingira itapaswa kutoa fidia kwa uharibifu huo.
Alisema kampuni haipaswi kulipa uharibifu wa amzingira pake yake lakini pia zinatakiwa kulipa fidia za uharibifu wa mazao, uhamishaji wa watu katika maeneo yao ya asili na uharibifu wa miundo mbinu
Akijibu swali la kuwaandaa vijana kupata ajira katika uchimbaji wa mafuta Waziri huyo alisema wizara imeandaa mikakati madhubuti ya kusomesha vijana kwa kuwapeleka katika vyuo mbali mbali ndnai na nje ya Tanzania hasa kwa kuwa makampuni yote ya utafutaji wa amfuta katika mikataba yao kipo kipengele cha mafunzo.
Alisema mkataba wa antrim wa mwaka wa 1997 ulikubali kutoa dola za kimarekani 50,000 kwa mwaka na kuna baadhi ya makampuni amabyo yamepewa lesini Tanzania Bara yamefikia hadi dola za kimarekani 100,000 kwa mwaka ambapo uchimbaji ukianza fedha kama hizo zitasaidia kuwapatia mafunzo vijana.
Wajumbe wa baraza la wawakilishi wa pande mbili za CCM na CUF waliingana kwa pamoja na kutaka suala la mafuta na gesi kuondoshwa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Zanzibar yajiuza vyema January 30, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.1 comment so far
Na Salma Said, Zanzibar
Serikali ya Mapindizi Zanzibar (SMZ) imesema Zanzibar imenufaika sana katika kujitangaza kwa wawekezaji katika sekta ya utalii na ushirikiano kwa nchi na mashirika mbali mbali ya misaada ya kimataifa duniani.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma wakati akijibu swali aliloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni (CCM) Salmin Awadh Salmin aliyetaka kujua ikiwa Zanzibar ni sehemu moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatumiaje wizara ya mambo ya nje katika kutekeleza shughuli zake za kiutendaji hasa zile za kiuchumi.
Waziri huyo alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatumia wizara ya mambo ya nje ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kufanikisha mambo kadhaa ya kimataifa ikiwa ni pamoja na safari za nchi za nje za viongozi wakuu wan chi za nje wanaotembelea Zanzibar.
“Mheshimiwa Spika ni dhahiri Zanzibar iemnufaika sana katika kujitangaza kwa wawekezaji na hasa sekta ya utalii na ushirikiano kwa nchi na mashirika mbali mbali ya misaada ya kimataifa amabyo ni dhahiri maendeleo makubwa yamefikiwa kupitia misaada tuliyoipata kutoka kwao” alisema Waziri Juma.
Juma alisema katika kuimarisha mshikamano wa muungano tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu katika kila ofisi za ubalozi kuwepo Mzanzibari kwa lengo la kuimarisha wizara hiyo kuwa na sura ya muungano.
“Jambo hilo tumelizungumza na tunakusudia kulizungumza zaidi katika kikao cha kujadili kero za muungano kitakachofanyika mwezi wa Aprili kwa ajili ya kufanyiwa kazi zaidi lakini wizara hiyo lazima iwe na mzanzibari kwa kuwa wizara hiii ni ya muungano” alisema Juma.
Alisema wamekubaliana kimsingi kwamba kila katika ofisi za ubalozi wa Tanzania ziliopo nje ya nchi kuwepo Mzanzibar kwa ajili ya kufuatilia masuala mbali mbali yenye maslahi ya Zanzibar.
Hamza alisema wizara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa ni wizara ya muungano hivyo ushiriki wa Zanzibar unahitajika katika wizara hiyo.
Alisema kwa sasa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ipo katika mchakato mkubwa wa kutafuta vijana wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi hizo katika ofisi za ubalozi.
”Suala la mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa ni moja ya wizara inayolalamikiwa katika kero za muungano…..yapo mafanikio makubwa katika kulipatia ufumbuzi tatizo hilo nab ado tunaendelea kujadiliana nao lakini tutafika pahala kila mmoja aridhike” alisema Juma.
Waziri Kiongozi ataka kufagia barabara January 30, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.add a comment
Na Salma Said, Zanzibar
Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Shamsi Vuai Nahodha ameahidi kushirikiana na watendaji wa Baraza la Manispaa kusimamia kufanyika kwa usafi katika manispaa ya mji wa Zanzibar kutokana na uchafu ulio kithiri katika mitaa mbali mbali Mjini hapa.
Nahodha amelazimika kuchukua uamuzi huyo kutokana na kubaini wafanyakazi wa baraza la mji wamekuwa dhaifu katika kutekeleza majukumu yao ya kufanya usafi katika maeneo mbali mbali ya mji pamoja na barabara za mjini kuwa chafu mno.
Kauli hiyo aliitoa wakati akitoa ufafanuzi wa kina kufuatia swali la msingi lililoulizwa Mwakilishi wa Jimbo la Nungwi (CCM) Ame Ussi Juma aliyetaka kujua serikali inashughulikia vipi suala zima la uchafu wa mji hasa barabara zilizojaa michanga amabzo kwa kiasi kikubwa zinaharibu miundo mbinu hiyo.
“Namuagiza Waziri wangu wiki ijayo tutalishungulikia suala la usafi wa mji kwa kugawa kazi sisi na wafanyakazi wa baraza la manispaa na ninaona bora mimi mwenyewe nitasimamia kazi hiyo tuone kama hatutaweza…..” alisema Nahodha.
Nahodha alisema tatizo kubwa la uchafu wa mji wa Zanzibar linatokana na manispaa ya mji kutokuwa makini na sio tatizo la vitendea kazi kama ilivyoelezwa na baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilishi.
“Nahisi tatizo kubwa linalotukabili sio suala la vitendea kazi ni ufanisi wa kazi yenyewe na kutimiza wajibu wetu kwa sababu nchi yetu masikini suala la kununua gari ya mamilioni hatuna lakini kama tutafanya usafi kwa huu umasikini wetu wa kutumia mifagio na hasa kwa nchi yetu ndogo basi tutaweza kuweka mji wetu safi lakini tatizo ni wafanyakazi kutimiza majukumu yao” alisisitiza Nahodha.
Alisema wakati manispaa ya mji ikitafuta vifaa na vitendea kazi za uzoaji taka, ni vyema kwanza wakafanya juhudi za makusudi kuhakikisha wanafanya mipango ya kiuongozi ambapo jambo muhimu ni kutekeleza wajibu katika dhamana walizopewa viongozi na wafanyakazi.
Nahodha alisema hivi karibuni baada ya kuzinduwa zoezi la usafi wa mji uliofanywa na wizara yake kumekuwepo mafanikio makubwa ya usafi, hali ambayo inawezekana kama juhudi za makusudi zitachukuliwa kufanyika katika maeneo mengine huku kila sekta ikiiga mfano huo.
Awali Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Suleiman Othman Nyanga alisema ili kulishulighulikia tatizo la kujaa michanga katika barabara za mjini, linaitaji gari maalumu la kisasa kwa kazi hiyo au kuajiri wafagiaji zaidi kutoka 20 waliokuwepo sasa hadi 60.
Alisema kwa sasa baraza la manispaa halina uwezo wa kuyafanya yote hayo ambapo hali ya fedha itakaporuhusu suala hilo litashughulikiwa ipasavyo.
Waziri Nyanga alisema jambo linalokwamisha kuwa na vitendea kazi bora kwa ajili ya usafishaji wa barabara ni ukosefu wa fedha, kutokana na gharama kubwa ya gari la kusafisha pamoja na vifaa vya kufyagilia si chini ya dola za kiamekani 105,000 sawa na fedha za Tanzania 135,000,000 ambapo serikali haiwezi kuzipata kwa sasa.
Uchaguzi Mdogo Magogoni Mei 23 January 30, 2009
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.1 comment so far
Na Salma Said, Zanzibar
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza ratiba ya uchaguzi mdogo jimbo la Magogoni lililowachwa wazi na Mwakilishi wa jimbo hilo aliyefariki dunia mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) Salum Kassim Ali imesema uchaguzi huo umepangwa kufanyika Mei 23 mwaka huu kufuatia kifo cha Mwakilishi wa Jimbo hilo Daud Hassan Daud.
Mkurugenzi huyo alisema awali Tume ilipokea taarifa kutoka kwa ofisi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, kuhusiana na kifo cha mwakilishi huyo aliyefariki dunia Disemba 12 mwaka 2008.
“Tumepokea taarifa ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, yenye kumbukumbu BLW/SP.1/Vol/145 inayojulisha juu nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha Mwakilishi Daud Hassan Daud chini ya kifungu 459 (b) ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 1984…ZEC imeitafakari kwa kina taarifa hiyo,” alisema Kassim.
Mkurugenzi huyo alisema baada ya taarifa hiyo kutoka kwa Spika ilijadiliana kwa kina suala hilo na hatimae Tume imeamua uchaguzi mdogo wa jimbo la Magomeni ufanyike Mei 23 mwaka huu.
“katika kikao chake kilichofanyika jana tarehe 29 2009 tume ya uchaguzi Zanzibar iliitiitafakari kwa kina taarifa hiyo ya spika na masharti ya uchaguzi, 1984 kifungu 45 (b), nachukua nafasi kukikinukuu hicho, endapo uchaguzi mdogo umepangwa kufnayika siku ya uteuzi itakuwa si chini ya miezi minne na si zaidi ya miezi 25 baada ya tukio lililopelekea kufanyika kwa huo uchaguzi mdogo…” alisema Kassim.
Taarifa za ZEC imesema zoezi la uandikishaji wa wapiga kura wapya litafanyika mwezi ujao Februari 28 hadi Machi 2 mwaka huu.
Pia taarifa hiyo imesema kwamba Machi 3 hadi Machi 8 itakuwa kushughulikiwa uhamisho wa wapiga kura na shahada zilizopotea ambapo Mei 3 itakuwa ni siku ya uteuzi wagombea.
Ifikapo Mei 4 itakuwa ni siku ya kusikiliza pingamizi dhidi ya wagombea huku Mei 5 hadi 22 itakuwa ni siku za kampeni kwa vyama vitakavyoshiriki uchaguzi huo mdogo ambapo Mei 23 ndio itakuwa ndio siku yenyewe ya kupiga kura katika jimbo hilo.
Jimbo la uchaguzi la Magogoni limelazimika kufnayika uchaguzi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo Daud Hassan Daud aliyefariki dunia Disemba 19mwaka jana baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa figo.
Uchaguzi wa jimbo la Mgogoni litakuwa na ushindani mkali kati ya vyama viwili vya CCM na CUF kutokana na kuwa jimbo hilo lina ushabiki mkubwa wa vyama hivyo huku nguvu zake zikitaka kukaribiana.