Bandari mpya iwe fursa ya kukuza uchumi wa Zanzibar November 23, 2008
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.add a comment
Na Ally Saleh
19 November, 2008
HABARI njema zilivuma wiki hii zikisema kuwa baada ya subira ya muda mrefu hatimaye bandari ya Zanzibar imekamilika na kuwa iko njiani kuanza kazi kwa kiwango chake kikamilifu.
Kila Mzanzibari atafurahia habari hii maana kila mtu anajua kuwa kitovu cha uchumi wa Zanzibar ni bandari na mchango wake tunaweza kusema haumithiliki kuanzia zama hizo hadi leo.
Kwa wengi wasiojua bandari ya Zanzibar ilikuwa na umuhimu mkubwa katika eneo hili la Bahari ya Hindi kwa kuwa ilikuwa ni kituo kikubwa cha kutia nanga meli zilizokuwa zikitoka chini ya Afrika kutokea Marekani na juu ya Afrika kutoka Asia na hata Ulaya.
Zanzibar ilikuwa ikitawala ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki kutoka chini ya Somalia mpaka Sofala, Mozambique, ilihitaji bandari yenye uwezo na haiba.
Mwaka 1892 ilitangazwa nia ya kuifanya Zanzibar Bandari Huru wazo ambalo halikuwahi kutimizwa kikamilifu na hata baada ya nia hiyo kusisitizwa upya katika miaka ya hivi karibuni basi bado imekuwa ni ndoto.
Kwa maumbile yake ya visiwa bandari ina nafasi maalum katika uchumi, hilo halina shaka yoyote ile. Na kwa hivyo uhai na uzima wa bandari unamgusa kila mtu hapa kwetu.
Ndio maana bandari ilipokuwa inaugua uchumi wa Zanzibar na watu wake walikuwa wanaugua. Ndio maana wakati mivutano ya kisiasa ilipokuwa ikirindima na kukawiza ufadhili wa mradi huo uchumi wa Zanzibar uliumwa nawatu wake waliumwa.
Na pia wakati mvutano uliotokea kuhusu aina ya ujenzi wa bandari hiyo, uchumi wa Zanzibar uliumwa na watu wake waliugua.
Lakini wengi tumekuwa tunajiuliza katika mazingira tuliyonayo au ambayo tunalazimishwa kuishi nayo ni rahisi kiasi gani ujenzi mpya wa bandari hiyo kuwa na faida kwa uchumi wa Zanzibar?
Hapa ni maana mbili. Moja ni ile ya mfumo mzima unaozunguka suala la faida ya ushuru unaoweza kutokana na harakati za bandari hiyo kuingiza na kutoa bidhaa, ambalo hili liko nje ya uwezo au utawala wa Serikali ya Zanzibar kwa upande fulani.
Na maana ya pili ni uwezo ulio ndani wa menejimenti ya bandari hiyo kusimamia na kuwa tayari kivifaa na kitaalamu ili kazi za bandari hiyo ziwe na natija ambayo umma wa Kizanzibari unatarajia kimapato na kiajira?
Kwa sasa bandari ya Zanzibar inafanya kazi katika hali ya ushindani mkubwa. Ushindani nje ya Tanzania dhidi ya bandari ya Mombasa na upinzani ndani ya Tanzania dhidi ya bandari ya Tanga lakini hasa Dar es Salaam na hatua zikianza kuchukuliwa kuiwezesha zaidi ile ya Mtwara.
Hata dhana ya kuwa na bandari huru inapanuliwa pia. Taarifa zinasema Kigoma inasukumwa iwe na hadhi hiyo na hivi karibuni tumeambiwa pia Dodoma pia inaweza kufanywa kuwa na hadhi hiyo ili kushika biashara inayokwenda katika nchi jirani ambazo kwa jumla ni tisa na vunge kubwa la kibiashara kwa Tanzania, lakini fursa hiyo ikiwa bado haijarutumiwa vyema au kikamilifu.
Mbali ya Zanzibar kutengezewa zengwe la ushindani lakini pia kuna suala zima la mfumo wa kodi. Hapa kuna “Ziraili” wa uchumi wa Zanzibar, yaani Mamlaka ya Kodi ya Tanzania (TRA). Kwa hali ilivyo sasa na mipango tunayosikia inazidi kutayarishwa, mikono ya taasisi hiyo itazidi kutopea katika roho ya uchumi wa Zanzibar.
Wengi tunajua jinsi wafanyabiashara kadhaa walivyoamua kuisusa bandari ya Zanzibar na kuhamishia uingizaji wa biashara zao moja kwa moja bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa wanatozwa mara mbili kwa kisingizio cha Zanzibar wanatozwa kiwango kidogo cha kodi.
Sote tunajua athari ya hili. Iwapo wafanyabiashara watapeleka bidhaa zao moja kwa moja Dar es salam ni wazi kuwa TRA itapata kodi yake, lakini itakuwa ni hasara ya Zanzibar maana Bodi ya Mapato ya Zanzibar itakosa kukusanya kodi za ndani na hivyo kutia pengo katika makusanyo ya Zanzibar na kuathiri bajeti na uchumi.
Kwa juhudi zozote zitazofanywa kuimarisha bandari ya Zanzibar kwa maana ya kuongeza uwezo wake wa kupokea na kutoa bidhaa, lakini hilo halitokuwa na baada iwapo Serikali ya Zanzibar haitochukua hatua madhubuti kabisa itayohakikisha kuwa mfumo mzima wa kodi unapitiwa upya kwa kudai kutizamwa upya sheria iliyounda Mamlaka ya Mapato ya Tanzania TRA.
Kwa upande wa pili, kama nilivyotangulia kusema ni uwezo na ubunifu wa menejimenti ya ndani kusimamia operesheni za bandari hiyo ambayo bado hadi leo inavutia kiasi kikubwa cha mizigo kinachoingia hapa, lakini kwa baadhi yetu inatia shaka iwapo tunatumia uwezo wa bandari hiyo kikamilifu.
Lazima tukubali ukweli kuwa hizi ni zama mpya. Ni mpya kisayansi na kiteknolojia na ni mpya kifikra na kibunifu.
Na kwa hivyo ni lazima bodi yenye kusimamia taasisi kama ya bandari ambayo inameza yote mawili ya sayansi na teknolojia na fikra upya na ubunifu ionyeshe sura kama hiyo.
Leo tena si wakati wa kuwachagua “Pandu na Jecha,” kuingia katika bodi kama hizo kwa kulipa hisani za kisiasa au kutafutiana nafasi za ulaji.
Pili ni muhimu kuwa na menejimenti ambayo inajua nini inakifanya. Menejimenti ambayo inaweza kumudu kila hatua ya operesheni zinazohusika katika bandari hiyo.
Kuweza kuwa na mipango na taratibu za kitaalamu na sio kazi kufanywa kwa njia ya kukikisa na kubahatisha. Kazi zisitolewe kwa hisia za kisiasa na vyeo vitolewe kwa uwezo.
Bandari kwa sasa, ni jambo ambalo sio siri, ina uhaba mkubwa wa vifaa vya kupakulia mizigo. Hii ni dhambi kubwa katika bandari yoyote ile duniani.
Siri ya bandari nzuri ni vifaa vya kupakulia ambavyo sio tu vinahakikisha usalama lakini pia vinahakikisha uharaka wa mizigo kushushwa na ndio siri ya mafanikio ya bandari yoyote ile iwe ni Singapore, Mombasa au Zanzibar.
Kila mwenye meli na mzigo anataka shehena yake ishuke haraka, kwa salama na ihifadhiwe pahala pema. Mzigo ukishuka kwa haraka unaokoa muda wa meli kukaabandarini au nangani kwa muda mrefu, lakini hali hiyo siyo ilivyo bandari ya hapa Zanzibar.
Mzigo ukishuka haraka pia ni nafuu kwa mwenye shehena maana mzunguko wake wa fedha unazidishwa kasi yake na mzigo ukihifadhiwa palipo pazuri ndipo sifa ya bandari inapokuja juu na watu wengi zaidi kutaka kuitumia.
Sasa hivi kazi zinazopatikana bandarini kwetu hazitoshi umma unaosubiri kibarua ambao hufika kila siku maeneo ya bandarini. Juhudi lazima ichukuliwe kuwezesha ajira zaidi kutengenezwa kuweza kuwasaidia watu zaidi na njia pekee ya kufanya hivyo ni kuongeza ufanisi ili mizigo mingi zaidi iweze kushushwa kwa siku, kwa wiki na kwa mwezi.
Ingawa kuimarika kwa vifaa kutamaanisha watu wachache wataopata kazi ya kibega, lakini pia itamaanisha fursa nyingi zaidi za watu wengine kupata kazi kwa maana ya kuongezeka kiwango cha mizigo itakayokuwa inapakuliwa kwa siku, kwa wiki na kwa mwezi.
Tusisahau pia kumalizika kwa ukarabati wa bandari hiyo kutaongeza pia idadi ya wasafiri wanaopita katika bandari hiyo na hivyo kuchangia katika sekta ya utalii wa nje na wa ndani mbali ya kuwa abiria nao pia hufanya biashara na sekta hiyo pia kuweza kuimarika.
Makala hii madhumuni yake ni kukumbusha kuwa tusifurahi kwa kuwa ukarabati wa bandari hiyo umeweza kukamilika. Lakini tufurahi zaidi kuwa bandari hiyo itakuwa na fursa bora zaidi ya kukuza uchumi wa Zanzibar kwa kuongeza mapato serikalini na kupatia ajira zaidi wananchi.
Lakini kwa hali ilivyo sasa haitii moyo sana. Lazima Zanzibar ipiganie kuleta mabadiliko katika sheria ya TRA kuvua minyororo ya “utumwa mpya wa kiuchumi”.
Ila zaidi yake bandari ya Zanzibar inahitaji msukumo mpya, fikra mpya na hasa vifaa vipya bila ya vitu hivyo tutakuwa tumekarabatiwa bandari lakini tutabakia pale pale pa kijungumeko.
Wasiliana na mwandishi wa makala hii kupitia simu +255 777 430 022, au tembelea www.eternaltourszanzibar.net, http://jumbamaro.blogspot.com
SUZA 4th Graduation Ceremony November 13, 2008
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.1 comment so far
- The State University of Zanzibar (SUZA) wishes to announce the names of prospective graduands for the 4th Graduation Ceremony to be held on Saturday 29th November, 2008 at 03.00 p.m at Victoria Garden, Mnazi Mmoja.
- The Chancellor of the State University of Zanzibar and the President of Zanzibar, His Excellency Dr. Amani Abeid Karume will confer the University awards.
- Graduands are requested to attend the rehearsal on Thursday 27th November, 2008 starting at 8.00 a.m. Those who will fail to attend the rehearsal will be awarded their awards in absentia.
- For the occasion, every graduand will have to rent a graduation robe by paying non-refundable Tshs. 10,000/-. Robes will be available from Monday 24th November, 2008 at the SUZA Procurement Office, Vuga Campus.
- Graduands are required to make their own travel and accommodation arrangements and the State University of Zanzibar is not liable to reimburse any expenses.
Bendera kama ishara ya unchi wa Zanzibar November 12, 2008
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.1 comment so far
Na Mohammed Khelef Ghassani
12 Novemba, 2008
Peter Kisumo, mbunge kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), alisema katika kikao cha Bunge la Bajeti la mwaka huu, 2008/2009, kwamba Zanzibar kuwa na bendera haimaanishi kuwa Zanzibar ni nchi, kwani bendera hiyo ni sawa na ile ya klabu ya mpira ya Yanga. Bila ya shaka, kauli hii ilitukera Wazanzibari na kuamini kwamba tumedhalilishwa. Licha ya kusema maneno hayo katika Bunge na sisi kudai kwamba aombe radhi na achukuliwe hatua kwa kuikosea adabu Zanzibar, hakuna chochote kilichofanywa hadi sasa, na hakuna dalili kama kitu hicho kitafanywa.
Sisi Wazanzibari hatuoni ikiwa kuna la kubishania ikiwa Zanzibar ni nchi ama la, maana ni kinyume cha mantiki kuuliza ikiwa jua linatoka mashariki ama la. Nakusudia kuwa ukweli haubishaniwi, yanayobishaniwa ni maoni ya mtu binafsi. Kwetu si suala la maoni ya mtu binafsi kwamba Zanzibar ni nchi, bali ni ukweli ulio wazi na usiopingika.
Makala hii, hata hivyo, haijikiti sana huko, bali inakusudia kuonesha historia ya bendera nchini Zanzibar kwa miaka 44 iliyopita na ikiwa historia hiyo inamaanisha lolote kwa hadhi na heshima ya Zanzibar.
Tarehe 10 Disemba, 1963 Zanzibar ilipata uhuru wake kutoka ukoloni wa miaka 73 wa Uingereza. Kuashiria uhuru kamili, Zanzibar ilipandisha bendera yenye mji mwekundu ikiwa na alama ya karafuu mbili katikati. Karafuu limekuwa zao la kibiashara kwa visiwa hivi kwa takriban karne mbili sasa.
Bendera hii ya uhuru ilipepea kwa muda usiozidi mwezi mmoja, kwani Januari 12, 1964 palifanyika mapinduzi yaliyoitangaza Zanzibar kuwa Jamhuri na kupandishwa kwa bendera mpya. Hii ilikuwa na rangi tatu: nyeusi juu, katikati manjano na chini buluu, ambayo nayo ikaja ikachukuliwa nafasi yake na bendera nyengine yenye rangi tatu pia, lakini zikiwa kwa mtiririko huu: buluu juu, nyeusi katikati na kijani chini. Kuondoka kwa bendera moja kwenda nyengine baina ya mbili hizi hakukuchukua muda mrefu. Labda ni chini ya mwezi mmoja.
Mapinduzi ya Januari 1964 nayo yakafuatiwa na Muungano wa Aprili 1964 na Jamhuri ya Tanganyika. Kwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar, Julius Nyerere, alama zote zilizokuwa zikitunika kuitambulisha Jamhuri ya Tanganyika sasa zikaidhinishwa kuitambulisha Jamhuri hiyo mpya iliyotokana na Muungano huu. Kwa hivyo, kuanzia hapo, Zanzibar ikawa nayo inapepea bendera ile ile inayopeperushwa Tanganyika.
Bendera hii inaunganisha karibuni rangi zote ambazo zilitumiwa na bendera mbili za Zanzibar baada ya Mapinduzi (ingawa hiyo haisemi kwamba ilifanyika kwa makusudi ya kuonesha uwepo wa Zanzibar ndani ya Muungano), isipokuwa zimepangwa kwa staili tafauti. Katika muundo wa pembe tatu, juu kuna rangi ya kijani, katikati kuna utepe mweusi unaozungukwa na tepe za kijani na chini kuna rangi buluu. Katika mtandao wa www.swimport.com/flags/unmemberflags.html, ambao una orodha ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na bendera zao, bendera hii ipo kwenye kiungo cha Tanzania – Zanzibar. Hii inaweza, pengine, kuhalalisha ile hoja ya Wazanzibari kwamba Zanzibar bado ni mwanachama wa Umoja huo, kwani haijawahi kujiondoa wala kupeleka ombi la kubadilisha uanachama wake. Hili, hata hivyo, ni suala la mjadala maana ni maoni tu.

Baada ya Muungano wa Aprili 1964, Zanzibar ilianza kutumia bendera hii ambayo pia ni ya Jamhuri ya Muungano hadi Agosti 2005
Zanzibar imeendelea kutumia bendera ya Jamhuri ya Muungano kama alama yake hadi mwaka 2005, ambapo Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha azimio la kuanzishwa kwa bendera ya Zanzibar, baada ya shinikizo la siku nyingi kutoka kwa Wazanzibari wenyewe. Kwa hivyo kuanzia mwaka huo hadi sasa, bendera ya Zanzibar imekuwa ni tafauti na ile ya Muungano, japo kwa umbile zinafanana sana. Bendera ya sasa ya Zanzibar ina rangi tatu: juu buluu, katikati nyeusi na chini kijani na ndani yake – upande wa kushoto juu – kuna bendera ndogo ya Jamhuri ya Muungano.
Pamoja na kuwa na bendera hii, Zanzibar pia ina bendera ya Rais, ambayo ina mji wa kijani, muhuri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar uliozungushwa kwenye duara lenye maandishi “Rais wa Zanzibar” na juu ya muhuri pameweka herufi “R” inayosimama kwa neno Rais.
Kama nilivyosema, Zanzibar pia ina muhuri wake ambao una michoro ya visiwa vya Unguja na Pemba, bahari, miti ya mnazi na mkarafuu na umeegemea kwenye panga na shoka. Huu ni tafauti na muhuri wa Adam na Hawa, ambao mwanzoni ulikuwa ukitumika na Serikali ya Tanganyika kabla ya kuhamishiwa kwenye Serikali ya Muungano.
Bila ya kutaja, bila ya shaka, kwamba wimbo wa Taifa wa Zanzibar ni tafauti sana na ule wimbo mrefu wa Taifa wa Jamhuri ya Muungano, ambao nao kama ilivyokuwa kwa alama nyengine za Muungano, ulikuwa wimbo wa Jamhuri ya Tanganyika. Wimbo wa Taifa wa Zanzibar ni mfupi:
“Mungu amtubarikia
Unguja na Pemba yote
Sote tunashangiria
Jamhuri kutuletea.”
“Jamhuri” ndilo neno lililomo kwenye Wimbo wa Taifa wa Zanzibar. Tunahitajika kusema zaidi ya hapa?
Kwa maelezo ya ziada kuhusu bendera Zanzibar tembelea www.allstates-flag.com/fotw/flags/tz-zan.html
Tendwa, ni CCM ndiyo ya kujifunzia uchaguzi wa Marekani November 10, 2008
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.add a comment
Na Salim Said Salim
UCHAGUZI wa Marekani umeweka historia mpya kwa taifa hilo ambapo kwa mara ya kwanza, mtu mweusi ataiongoza nchi hiyo. Uchaguzi huu ulikuwa tofauti na chaguzi zilizopita na ndio maana ulivutia watu kila pembe ya dunia. Wengi walitaka kuona kama mtu mweusi, Barrack Obama, angepewa nafasi ya kuiongoza Marekani. Tulichoshuhudia ni kuwa amepewa kura nyingi; tena kwa kishindo cha kweli: sio kwa njia ya wizi, au mizengwe yoyote. Sauti ya umma imeruhusiwa kusikika.
Wamarekani na watu wengi duniani wametaka mabadiliko kutokana na kuchoshwa na siasa za kibabe za Rais George Bush za kuilazimisha dunia iridhie Marekani kuwa polisi wa kimataifa na kuwa na haki ya kuvamia nchi yoyote na pia kutaka nchi zote zitunge na zifuate sheria za Kimarekani kama zile za kupambana na ugaidi.
Nchi nyingi za Ulaya, Asia, Arabuni, Amerika ya Kusini na Afrika zilitiwa kitanzi na kuburuzwa na Bush, baadhi yao kwa kuogopa na nyengine bila ya kutambua athari zake. Sasa uchaguzi umemalizika na kinachofanyika ni tathmini na watu katika nchi mbali mbali wanajiuliza wamejifunza nini katika uchaguzi huu wa Rais wa 44 wa Marekani.
Hapa nchini, miongoni mwa waliowataka Watanzania wajifunze baadhi ya mambo kutokana na uchaguzi huu ni Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa. Lakini namna alivyowataka Watanzania kujifunza inatia mashaka na kujiuliza kama Tendwa alielewa alichokisema au alidhani Watanzania ni mbumbumbu na hawana uwezo wa kutofautisha kati ya changa na pevu, mbichi na mbivu, shaba na dhahabu, mto na kitanda au mto na bahari.
Tendwa alimsifu mgombea wa Republican, John McCain, kwa kukubali kushindwa bila ya kinyongo na kuwataka wanasiasa na Watanzania kujenga utamaduni huu wa kukubali matokeo ya uchaguzi kwa vile hali hii inasaidia kuweka mazingira mazuri ya kujipatia maendeleoa baada ya uchaguzi.
Ni wito mzuri, wa hekima na busara ya hali ya juu. Lakini alichofanya Tendwa ni sawa na kutanguliza gari la farasi mbele na kutaka farasi aliyepo nyuma afanye safari ya kuelekea kule kwenye gari lake.
Kama kweli Tendwa alikuwa anatoa maoni yake kutoka moyoni na kwa nia njema, basi alipaswa kuzungumzia mazingira yaliyozunguka uchaguzi wa Marekani na kulinganisha yanayoonekana Tanzania wakati wa uchaguzi.
Angezungumzia hali inavyokuwa wakati wa uandikishaji, wakati wa kampeni, kwenye vituo vya kupiga kura na mazingira yanayoonekana ya wizi wa kura na matokeo kutolewa baada ya wiki nzima hata kwa majimbo madogo kama ya Zanzibar ambayo wapiga kura wake hawazidi 11,000 na baadhi ya majimbo huwa na urefu wa robo kilomita tu.
Tanzania, vyama vya upinzani huwekewa mikwara visifanye mikutano katika baadhi ya sehemu za nchi na hukataliwa kutumia viwanja vya Manispaaa au shule wakati chama tawala CCM hakipati vikwazo hivyo. Makamanda wa polisi wanaokandamiza upinzani hupandishwa vyeo kama tunzo kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Katika uchaguzi wa Marekani, polisi hawakuonekana kutisha watu kwa kubeba silaha karibu na vituo vya kupiga kura au barabarani, lakini Tendwa hakuligusia hili.
Vile vile katika uchaguzi wa Marekani hatukusikia kuwepo vikundi vya vijana vinavyoshambulia vituo na kupiga watu nondo na mapanga kama inavyoonekana Tanzania wakati wa uchaguzi na hasa Zanzibar, na wanaofanya hivi hawakamatwi na kushitakiwa kwa uhalifu huu.
Wamarekani hawakwenda vituo vya kupiga kura na kuambiwa wasubiri karatasi za kura hazipo. Tendwa anajua kuwa ni kawaida Tanzania kwa vifaa vya kupiga kura kufika vituoni masaa sita baada ya muda wa kupiga kura kutarajiwa kuanza au kuokotwa mitaani. Jee haya ni mazingira yanayohakikisha kuwepo uchaguzi huru na haki?
Tendwa ni Msajili wa vyama vya siasa. Kati ya majukumu yake ni kuhakikisha nchi yetu inafanya uchaguzi wa haki na huru kwa kufuata sheria. Mbona hajauliza kwa nini hata mtu mmoja wa watu zaidi ya 5,000 waliorodheshwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa kujiandikisha zaidi ya mara moja hawajashitakiwa na kuwajibishwa kisheria au hata majina yao kuwekwa hadharani?
Hivyo haoni kuwa hali kama hii inachafua uchaguzi na hata kupelekea anayeshindwa kutokubaki matokeo? Au kwa anavyoona Tendwa hii ni kwa vile udanganyifu umeanza kutoa sura kama sehemu ya chaguzi zetu?
Kinachoonekana ni kwa Msajili kuona umuhimu wa watu kukubali matokeo ya uchaguzi, hata pakiwepo mizengwe iliyokuwa wazi. Ni vizuri kwa Tendwa na wenzake katika ofisi yake na wale wa Tume za Uchaguzi wakaelewa kuwa wamekubali dhamana na wanao wajibu wa kuhakikisha wanazitekeleza kwa mujibu wa katiba, sheria za nchi na za uchaguzi.
Yaliyotokea Marekani ni fundisho kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na tume zetu za uchaguzi. Ni lazima tukubali kubadilika na kuruhusu sauti za wananchi ziheshimiwe kupitia masanduku vya kura.
Tendwa, akiwa Msajili wa Vyama vya Siasa, anapaswa kuelewa kuwa amebebeshwa dhamana ambayo kama hawezi kuitekeleza kwa uadilifu basi asijaribu kuupotosha umma kwani mawazo ya hekima na busara huwa na maana pale yule anayeyatoa anapoonekane kwanza anayaamini na anayatoa kutoka moyoni na sio mdomoni.
Tendwa umenena,lakini hujatenda. Wanachotaka Watanzania, Bara na Visiwani, ni kuona unatenda yale unayoyasema katika kusimamia vyama vya siasa.
Muda upo, lakini unakimbia kwa kasi. Juzi hujaweza, jana hukuweza na je leo hutaweza kufanya la maana baada ya kuona uchaguzi wa Marekani ulivyofanyika? Ni vema kwa wewe na wenzako katika ofisi yako kwanza kujifunza misingi ya uchaguzi huru na haki ambao matokeo yake hukubalika bila manung’niko kisha ndio muwe walimu wa kutoa mafunzo ya kuwataka Watanzania wajenge utamaduni wa kukubali matokeo ya uchaguzi.
International Conference on the Future of Zanzibar November 10, 2008
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.add a comment
International Conference on the Future of Zanzibar (13 – 14th December, 2008) Dragon Hall, 17 Stukeley Street, Covent Garden, London, WC2B 5LT
BOOKING FORM
(Conference fee £30.00)
Title: …..………………………..
First name: ……………………..
Surname: ……………………….
Position: ……………………………
Organisation: ………………………….
Address: ………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………
Phone: ……………………………….
Email: ……………………………………….
How would you like to receive your confirmation?
Please circle
- By Email …………………
- By Post ………………………………….
Payment Method:
- By Cheque, payable to: Zanzibar Relief Agency
- By Bank Transfer: If paying by automated transfer a copy of notification MUST be sent.
Account Name: Zanzibar Relief Agency
Acc No.: 83655903,
Sort Code: 20-67-88, Barclays Bank UK
- Invoice: Invoice name and address (if different from above)
………………….……………………………………………………………………….
…………………………………………………………………………………………..
Accommodation:
This conference is non-residential and accommodation is not included in the booking fee.
Please return this completed form to MUWAZA, 23 St Margarets, Barking, Essex, IG117JN, or by email to mustakbalzanzibar@yahoo.co.uk.
Deadline for submission of the forms is 1st December 2008.
Enquiries: Please call the conference team on +4531162592, +447956027027, or email mustakbalzanzibar@yahoo.co.uk.
About us: MUWAZA is non governmental organization aiming at uniting all Zanzibaris wherever they are for the purpose of prospering their lives and development of their country irrespective of their political






