Kama Nabwa umekwenda, Unabwa umetuwachia February 23, 2007
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.add a comment
Na Mohammed Ghassani
15/02/2007
Mwanzoni mwa asubuhi
Dunia inaamka
Malaika wa mauti akashuka
Baba akamkabili kumwambia:
“Nimetumwa na Molao
Mbeleye uhudhurie!”
Kwa sauti ya kupuma
Baba akamuuliza:
“Ni vipi wanangu, nani atawalea
Ni nani wa kuwatunza
Nani atawaongoza
Kupambana mapambano?”
Yule malaika akaamba:
“Uliishi uhai wako
Kwa hima ya kupambana
Ukazaa watoto wako
Kwa hima ya kupambana
Na sasa hivi waenda, wauliza mapambano?
Masikini Ali Nabwa, mja wa kupambana
Hebu tuende kwa Mola
Siku sasa imefika
Urudi ukapumue!”
Baba naye akajibu:
“Kurudi kwa Bwana’ngu,
Sipingi, sipingi katu
Hiyino faradhi yangu
Walakini khofu yangu
Ni hawa vijana wangu
Wataweza mapambano
Wataishi kimapambano
Kisha wafe kimapambano
Kama nifavyo baba yao?”
Basi Nabwa, baba yetu
Kaondoka akikhofu
Lau wanawe twaweza
Kupambana kama yeye
Mbele ya vitisho vile
Mbele ya idhilali ile
Mbele ya gharama zile
Jabir, Ghassani, Salma,
Ali, Jussa, Bimani na Hamza
Wanawe, bila ya yeye, tutaweza?
Tutaweza kusimama kulinda kauli yetu?
Tusiogope lawama wala fitina za watu
Za kuvuliwa uraia, na kupokwa paspoti
Za kuzuiwa riziki kwa kufungiwa milango
Za kugeukwa na hata watu wa karibu
Hivi sisi, wanawe, tutaweza?
Kama tukikoseshwa ajira na pesa ya matumizi
Tukawa twarudi majumbani, paka jikoni kalala
Na kosa letu ni kuwa:
Tumefuata nyayo za baba
Kusema la kweli na lilo la haki
Wanawe tutasubiri na kisha twende pamoja__
Tusigeuze shingo zetu na kumeza matapishi?
Khofu za baba si kwamba
Alituona dhaifu
Lakini dunia hii
Aliona ikichenji
Na mambo yakijipinda
Mbele nyuma; nyuma mbele
Na yeye alitamani azidishe kutufunda
Tuhitimu somo hili
La dhati ya mapambano
Illa sasa amekwenda, akilia:
“Wanangu, Mola, wanangu!”
Naam, ndio sisi wanawe
Katika fani ni yeye aliyetutotoa
Alotuzaa, alotulea, alotukuza
Akatuonesha wapi tusimame na wapi tukae
Wapi tuseme, wapi tunyamae
Na juu ya yote:
Alitufunza heshima na utukufu wa mtu
Kwamba ni kujiamini
Na asojiamini hana utu
Nasi twaona fahari
Kuwa Nabwa baba yetu
Kwamba ndiye mlezi wetu
Kunasibishwa na yeye
Kwetu ni jambo akhasi
Na kiapo chetu ni hiki:
Kama baba kama mwana!
Nabwa, baba, hukujijenga wewe
Uliyojenga ni taasisi
Nitaiita Unabwa
Unabwa ulitufungua midomo
Leo hakuna wa kuifunga
Unabwa ulifungua milango
Ya habari, ya kujieleza na kuelezwa
Wale jamaa wameshindwa kuifunga
Mwangwi wa Dira yako
Ungenasi hadi leo
Ulikuwa taasisi
Na taasisi hudumu!
Basi wewe, baba, fika mbele ya Molao
Jasho ukitiririka
Hilo si jasho la wizi
Ni jasho la kutumika
Kutumikia watuo
Kutumikia faniyo
Kutumia ulezio
Nao ni sisi wanao.
Tungetaka ubakie daima dawamu
Illa madhali mwito wa Mola umeita
Ni shuruti uitikwe
Nawe baba umeuitika
Basi nenda kwa salama
Mithali waja wendao
Wanao ulotuwacha nyuma yako
Usitusikitikie
Tutapambana kijanadume
Na tutakufa tungali watu.
Wanao, baba, wanao
Twakupa ahadi hii:
Tutakufa tungali watu
Hatujageuka nguruwe
Hatutakufa nyamamwitu
Azaaye na wanawe
Tutakufa tukumbukwe
Kama ukumbukwavyo wewe
Kwa heshima, kwa staha na kwa jina
Tutakufa na Unabwa!
Alitaka afe hivi…. February 23, 2007
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.add a comment
Na Mohammed Ghassani
15/02/2007
Ali Nabwa alitaka:
Zama za kufa zikija___
Zije angali yu mtu, hajageuka nguruwe
Hajakuwa nyama mwitu, azaaye na wanawe
Zije bado ana utu, akiondoka aliliwe
Hishima iwe pamoja naye
Navyo ndivyo ‘livyokufa___
Sote twalia kwa yeye!
Ali Nabwa alitaka:
Mauti yakimf’ata:
Yamf’ate mapambanoni, apigania nchiye
Yasimfate chumbani, kapakata miguuye
Afe kikondoo kwani, naye ni simba mwenyewe?
Simba hufa kwenye vita
Na ndivyo alivyokufa___
Jemedari na shujaa!
Ali Nabwa alitaka:
Siku yake ikifika_____
Ifike angali chumvi, mithali umuhimuwe
Wamuhitaji wajuvi, wahisi waondokewe
Asife kifo uchimvi, hata tanga ‘siekewe
Kufa huko hakutaka
Naye hakufa ja hivyo_____
Amekufa akihitajiwa!
Ali Nabwa alitaka:
Safari yake ‘kijiri____
Ijiri hayu fakiri, kwamba sanda akopewe
Bali hakutaka kufa tajiri, utajiri kwake kiwe
Hakutaka afe na matajuri, bali na deni asiwe
Deni si mwenza mzuri
Naye hakufa mdaiwa_____
Labda makala zake!
Ali Nabwa alitaka:
Pumzi ikimuhama____
Imuhame sijidani, mauti yamchukuwe
‘Simuhame matungini, kilabuni wala kwenye msewe
Alitaka afe muumini, msala chozi utowe
Uliliye ulitima
Naye amekufa hivyo____
Akiwa mchaji Mungu!
Ali Nabwa alitaka:
Buku lake likifungwa____
Asiwe katika madhalimu, wa viumbe vya Molawe
Lifungwe watu wangali na hamu, wakitaka lifunuliwe
Afe na wake utamu, ufavyo muwa ufuwe
Asife nikisimangwa
Na Nabwa kafa na hadhi____
Na utukufu na jaha!
Ali Nabwa hayu nasi! February 23, 2007
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.add a comment
Ali Nabwa katoweka, na sote tumezeeka
Na wale walomcheka, leo damu watapika
Aibu imewafika, kwa yote yalotendeka.
Na kweli itapofika, roho zao kukatika
Pasiwepo pa kushika, hata haya kutundika
Sumu yao watapika, watafute pa kuwika.
Kwa urongo kupachika, leo watajizika
Ficha fichu papatika, kukataa za hakika
Allah! Allah! Rabbana, tunusuru abdika.
Msiba umetufika, na hasara kuibuka
Sote waja wa Hakika, kwa urithi kujitwika
Wake Mola tamweka, Malaika kuitika!
Ameen.
Wakatabahu,
Salim H. HIMIDI/Bwanatosha,
Paris, France,
18/02/2007.
Ufuasi usikiuke uhalisi February 12, 2007
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Politics.add a comment
Na Mohammed Ghassani
Wakati mazungumzo ya kuisaka suluhu ya kudumu Zanzibar yakiendelea baina ya timu za majadiliano kutoka vyama cha CCM na CUF, kuna mambo machache tunayopaswa kukumbushana kwa nia safi ya kujenga mustakbali mwema.Hili la nia safi ni mojawapo na, nasisitiza, lifahamike vyema kwa nia safi pia. Zanzibar ni yetu sote, na ni mahala pekee kwa sisi, tunaojitambua na kujitambulisha kuwa Wazanzibari, tunapoweza kupaita petu. Na hili neno petu lenyewe lina maana ya ndani zaidi kuliko linavyoonekana. Linahitaji nia safi kwelikweli kulifahamu na kulifahamisha. Waingereza huita home, kwa kulitafautisha na house. Wana msemo kwamba a house is built of bricks and stone, but home is built by love alone.
Ushereheshe kadiri uwezavyo msemo huu, ndivyo utakavyoyakuta mapenzi yetu yalivyo kwa mpendwa Mama yetu, Zanzibar. Kwetu hatuna mbadala kwaye. Pengine popote katika sayari hii ya Mungu Muumba, hatupahisi. Kupahisi, nakusudia, ni kupatia moyoni, kupavaa na kupaamini. Popote tuwapo, pasipokuwa Zanzibar, twajihisi kwamba tu wageni na watu wa kupita tu. Ni kwa Zanzibar tu, ndiko tujitambulishako na tujifakharishako. Namna hiyo ndivyo tumpendavyo Mama yetu!
Kwetu sisi, hakuna chochote tukipendeleacho zaidi ya kupaona petu pametulia, watu wetu wameshikana mikono kuijenga nchi yao na wenetu wanacheza wakikuwa pamoja kwa mapenzi na mshikamano wa kidugu uliomo ndani ya damu zao, maana sisi, Wazanzibari, wazazi wao, tu wamoja. Hakuna cha thamani zaidi ya hicho.
Basi mpenzi na rafiki yetu ni yule anayesaidia hicho kuwa; na adui na hasimu yetu ni yule anayekizuia kisiwe. Kumpapatikia mtu anayetusaidia kumtukuza Mama yetu, Zanzibar, kwetu ni jambo akhasi. Na vivyo kumpiga pande mtu anayemdhalilisha Mama yetu huyo, kwetu ni jambo la wajibu. Hakuna ubaya kuyatekeleza mawili hayo. Hatuyaoenei aibu.
Na hapa ndipo penye nukta nyengine. Maneno hayatoshi kuelezea matarajio waliyo nayo Wazanzibari, hivi sasa, kuhusiana na khatima ya nchi yao. Kama kuna zawadi yoyote ambayo Rais Jakaya Kikwete amewapatia watu hawa ni jitihada zake za kuanzisha mjadala wa kuelekea suluhu ya kudumu.
Licha ya ukweli kwamba Rais Kikwete alipaswa kuutekeleza wajibu huu kama kiongozi wa watu, lakini wenziwe waliopita kabla yake walikuwa pia viongozi wa watu na hawakusimamia jukumu lao la kiuongozi. Kwa hivyo, yeye anayeutekeleza anastahili sifa na shukrani maalum. Na sisi, Wazanzibari, si wachache wa shukrani. Hali tukitambua kuwa Rais Kikwete hatufanyii ihsani katika hili, lakini pia sisi si wizi wa fadhila. Tunamthamini kama kiongozi na rafiki wa kweli kwetu. Kwa jitihada hizi, anastahili heshima hiyo.
Maana twajuwa kwamba, ikiwa Zanzibar yetu itazidi kutopea kwenye ubaya zaidi ya hapa ilipo sasa, yeye atajeruhika heshima yake kama kiongozi wa nchi tu, lakini hatapoteza zaidi ya hapo. Kinyume chake, tutakaopoteza mengi ni sisi, Wazanzibari___ heshima, mali, roho na, juu ya yote, mustakabli na jaala ya watoto wetu.
Kumbe Rais Kikwete angeliweza kujivalisha miwani ya kiza na kujitia pambani, akajifanya haoni wala haisikii Zanzibar ikizama shimoni, akamaliza kipindi chake cha uongozi, akastaafu na akaiacha nchi yetu ikiwa mbovu zaidi ya vile alivyoikuta. Kwani, kama hilo lingejiri, la ajabu hasa lingelikuwa lipi? Kwani sio siye tuliozowea kusalitiwa na kudharauliwa ndani ya Jamhuri hii ya Muungano?
Sio siye tuliozoea kuachwa katikati ya vilio na taharuki, mithali ya madude yasiyo thamani, huku viongozi wa juu tuwaliliao wakigeuza shingo zao au hata wakithubutu kutukejeli? Kwani sio siye tuonekwao watu-mwitu mbele ya watu-wastaarabu wenye hatamu za nchi hii? Pasingelikuwa na la ajabu, kwa hivyo, japo lawama na shutuma zisingekwisha mpaka siku ya ufufuo! Na kwani nani kasema kuwa lawama na shutuma zinazuia pishi za wakubwa kujaa?
Ndivyo alivyotufanya mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, na pishi yake haikupungua hata kibaba. Alitukuta wabovu, tumeoza, twanuka. Na ingawa tulikuwa raia wake, tulioishi kwenye vipande vya ardhi vinavyotambuliwa kwamba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo yeye alikuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wake, yayumkini hakututambua hivyo. Na kama alitutambua, basi ndiyo hivyo hakutuhisi.
Nasema hakutuhisi kwa kuwa, kwenye ubovu na uoza wetu huo, Mkapa aliishi nasi kwa miaka kumi ya utawala wake, lakini hakushugulika na kuoza na kuharibika kwetu. Kubwa alilolifanya Rais huyu, alipotuona tunavunda, ilikuwa ni kufumba pua yake, na sio kuuondosha uovu na uoza uliokuwepo. Hata tuliponyayuwa mikono ya kutaka msaada, alijibu kwa kuongeza wanajeshi na silaha nzito nzito. Akaondoka akituwacha na ubovu wetu, husemi ila mateso yetu ndiyo iliyokuwa starehe yake na kudhalilika kwetu ndizo andasa zake. Tabaani, alikuwa anastaaladhi vikubwa mno nafsini mwake pindi akiarifiwa na watu wake namna tulivyoadhibika ndani ya mikono ya serikali yake.
Basi nasema, naye Rais Kikwete angeliweza, chembilecho wasanii wa Zanzibar, kwa raha zake, kuja kustaafu na kumalizia muda wake Chalinze, kama anavyoumalizia mwenzake sasa kwenye hekalu la Lushoto, huku akiiwacha Zanzibar na Wazanzibari kwenye mateso ya kuchukiza kwa kisingizio cha kulinda historia ya Mapinduzi na kudumisha Muungano. Lakini inavyoonekana, hadi sasa, Rais Kikwete ameamua kutokuyadharau mateso yetu. Ameamua kutokuufanya udhalilifu na dhiki zetu kuwa andasa zake. Ameamua kutukubali na kutuhisi kwamba sisi ni raia wake.
Ndipo kwa hilo, inapokuja nukta hii ya kumalizia: kwamba kuna haja ya kumsaidia Rais Kikwete ili naye atusaidie. Hilfen Sie hilfen, wasemavyo Wajerumani. Na miongoni mwa yale machache ambayo sisi wengine tunaweza kumsaidia Rais Kikwete ni kumkumbusha kwamba, uhalisi wa tatizo la Zanzibar ni zaidi ya mifano apigayo kila mara anapozungumzia huu anaouita mpasuko.
Nimemsikia mara mbili tatu akipiga mifano ya mpasuko wa Zanzibar kwa kutaja hatua zilizokuwa zinachukuliwa na wananchi kuwasusia wenzao ambao wana imani tafauti za kisiasa. Mara mbili za mwanzo ni katika mikutano yake aliyoifanya mwanzoni mwa mwaka jana Pemba na Unguja akiwashukuru wananchi wa visiwa hivyo kwa uchaguzi uliomuingiza yeye madarakani. Mara nyengine ni majuzi katika mazungumzo yake na wahariri wa vyombo vya habari.
Mifano anayopiga Rais Kikwete ni kama ule wa anayevuusha watu kwa kidau baina ya Mkoani na Kisiwapanza (Pemba) kutokuwapa huduma hiyo wale wanaowaona kuwa wapinzani wao kisiasa. Ama katibu mmoja wa CCM ambaye aliachiwa maiti ya mzazi wake na majirani zake, ambao kwa vyovyote vile watakuwa ni wana-CUF. Au watu kuacha kumfuata imamu katika sala kwa kuwa si mwenzao.
Sasa, inawezekana kabisa kwamba, hii ndiyo mifano pekee aijuwayo Rais Kikwete katika kuuelezea uzito wa mpasuko wa Zanzibar. Yayumkini ndiyo mifano apewayo na watu wake wa karibu waliomzunguka. Na ni mifano ambayo ni ya kweli. Lakini, ukweli wa uwepo wa mifano hii hautoshi kulielezea tatizo lenyewe lilivyo. Ukweli huu, badala yake, unaonesha kuna kitu chengine cha ziada na, kwa hivyo, chenye kutoa mifano mingi zaidi.
Nakusudia kusema kuwa, mpasuko wa kisiasa Zanzibar hauelezeki tu kwa kisa cha Katibu wa CCM kususiwa maiti ya mzazi wake na majirani zake, ambao ni wana-CUF, bali pia kinaelezeka kwa Katibu huyo kutangulia kwenda kutia fitina Polisi ili majirani zake hao waje wakamatwe, wapigwe, wateswe na kisha waswekwe ndani ambako wasingeliweza kutoka hadi kwa kutoa kiasi kikubwa cha pesa, vyenginevyo wabambikiziwe kesi za kubuni!
Mpasuko huu haulezeki tu kwa kisa cha mwenye dau Kisiwa Panza kukataa kumchukuwa Sheha wa Shehia yake, bali pia unaelezeka zaidi kwa Sheha huyo kuwakaribisha vijana wa makambi ya Janjaweed katika shehia yake ili kuja kuchoma moto majumba ya watoto na wajukuu wa mwenye kidau, na kuwaibia mali zao. Ndivyo ulivyokuwa mfano wa kijiji cha Kianga katika siku za uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mkoa wa Mjini Magharibi.
Mpasuko wa Zanzibar hauelezeki tu kwa familia moja kukataa kuiozesha mtoto wao katika familia nyengine, bali unaelezeka zaidi kwa kufahamu kuwa hiyo familia iliyokataliwa kuoa, iliwahi kuwawekea pingamizi ya kuandikishwa kuwa wapiga kura wanafamilia ambao sasa wanataka ukwe nao, kwa madai kwamba hawajatimiza muda wa kuishi katika eneo lao ilhali kwa miaka 20 mutawaliya wamekuwa wakiombana chumvi na moto mlango kwa mlango. Kichekesho ni kuwa, hata huyo mtoto anayeposwa, ambaye sasa ana miaka 21, alizaliwa katika nyumba hiyo hiyo na mama mkwe mtarajiwa ndiye aliyekuwa mkunga!
Mpasuko wa kisiasa wa Unguja na Pemba hauelezeki kwa mfano tu wa kukataa kununua na kuuza kwa mtu anayedhaniwa kuwa ni kijana wa Janjawidi na vikosi vya SMZ, bali unaelezeka zaidi kwa mifano ya hasara kubwa ya mali, damu na heshima iliyosababishwa na vijana hao kwa hao ambao leo wanakataa kununua na kuuza kwao. Ndiyo mifano ya duka la Sana Express kuchomwa moto pale Lumumba Unguja ambapo zaidi ya mali ya milioni 500 iliteketezwa. Ndiyo mifano ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa Mzee Hamad Salum na Muhunzi Juma wa Jang’ombe. Ndiyo mifano ya kubakwa kwa mke wa mwalimu wa skuli ya Dole. Ndiyo mifano ya watu wa Kinuni kukamatwa na hawa tuwaitao Polisi wetu wakitoka msikitini na kwenda kupigwa, na hadi kufikia upeo wa kunyweshwa mikojo yao. Ndiyo mifano ya watu hao kuvamiwa katika mistari ya kujiandikisha kuwa wapiga kura wakakatwa kwa mapanga vichwani na kufundwa kwa nondo.
Kwa maneno machache, na kwa dhamira nzuri, tumsaidie Rais Kikwete kwamba wale waliouliwa ndugu zao, wakabakiwa watoto na wake zao, wakawachiwa mayatima na vizuka, wakavunjiwa nyumba na kuchomewa moto mali zao, wakaswekwa ndani kwenye mateso na idhilali hizo zilizoepuka kabisa mipaka ya ubinaadamu, ndiyo hao ambao waliamua kuwagomea wale wote wanaoamini kwamba walishiriki kwa njia moja ama nyengine katika unyama huo waliotendewa.
Kibinaadamu watu hawa wangeliweza kulipiza visasi kwa yale waliyotendewa. Hiyo ingelichukiza, lakini bado ingefahamika. Lakini, kwa ubinaadamu huo huo, wakaamua kutokunyanyua mkono kuwarudi wadhalilishaji wao, bali kutokushirikiana nao tu. Hizi huitwa politics of non-cooperation, siasa za kupiga pande. Tanzania iliifanya hiyo, wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, dhidi ya Afrika Kusini kupingana na utawala wa kibaguzi. Ni matawi miongoni mwa matawi ya siasa za kupigania haki kwa njia ya amani, nonviolence politics.
Kama hili si halali katika ujenzi wa Zanzibar mpya, ni sawa. Lakini kwamba lilitumika, kama Civilian Based Operations (CBO), harakati za kiraia, dhidi ya Military Based Operations (MBO), harakati za kijeshi, zilizokuwa zikifanywa na serikali, kwa hakika lilikuwa jambo ndilo.
Nihitimishe kwamba, inawezekana, kwa nia ile ile safi niliyoitaja mwanzoni, Rais Kikwete hataji mifano hii ya upande wa pili katika kuuelezea uzito wa mpasuko, kwa kuwa hajawahi kuelezwa hali halisi. Inawezekana pia, kwa nia hiyo hiyo safi, alikuwa ameshaelezwa, lakini kwa kuwajuwa CCM wenzake wa Zanzibar walivyo, hataki kuwatahayarisha kadamnasi. Yote mawili yanaeleweka. Husnu dhanna, tusemavyo Wazanzibari.
Kwa nini tunahama kwetu kukimbilia Ughaibuni? February 12, 2007
Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.add a comment
Ni bahati mbaya kwamba, huko Ulaya nako hawatakiwi (au kwa usahihi zaidi hawatakiwi hivyo walivyo). Kwa hivyo, wanarudishwa kwanza katika nchi ya Kiafrika ili wakachujwe na ikibidi kuchukuliwa, wawe wachache sana ambao watakuwa na faida ya wazi wazi na ya moja kwa moja kwa Ulaya. Na hii inaeleweka.
Makala hii, pamoja na ijayo, itazungumzia sababu za Waafrika kuhama kwao na kupendekeza baadhi ya njia za kufuatwa. Tuanze kwanza na sababu ya ndani ya bara letu, na tuanze pia kwa tabaka la hawa tuwaitao ‘wasomi’.
Katika A Man Of the People, Chinua Achebe anamnukuu Chief Nanga, mwanasiasa asiye na uelewa mkubwa wa mambo lakini aliyefanikiwa kupanda kisiasa kiujanjaujanja tu, akimuambia Odili, msomi aliyekuwa ndio kwanza ametoka chuo kikuu: “It doesn’t matter what you know, but whom you know!” Sio ukijuwacho, bali umjuwaye.
Hii ndiyo khulka ya kawaida kwa Afrika nzima. Baada ya kuwa nchi imeshatumia fedha na muda mwingi kumsomesha kijana wake, msomi huyu hurudi nyumbani kuja kukumbana na udhalilifu kama huu. Chote kile alichokisoma chuoni, huwa si mali kitu. “Hawezi kuishi maisha ya kitabuni katika uhalisia.”
Huu ni ukweli unaomtesa msomi huyu kiuchumi, kijamii na kisaikolojia. Hujikuta mgeni kwenye jamii yake mwenyewe aliyozaliwa. Kama mwanaadamu, angelitamani kuishi waishivyo watu, angalau kwa kupata mahitaji muhimu ya maisha. Kama mwanajamii, angelihitaji awe mshiriki katika shughuli za kijamii kwa kuwasaidia watu wake. Na kama msomi, angelihitaji kupata utambulisho wake kutoka jamii hiyo kwa stahiki yake. Angelitaka aheshimiwe, angalau kwa maana nyepesi tu.
Lakini anajikuta hana fursa yoyote ya kuutumia usomi wake kuyapata hayo, maana hapa sio nini anakijuwa bali ni nani ahli yake katika system, ndiye atakayeweza kumsaidia angalau apate kijisehemu cha kutarazaki, mkono uende kinywani. Anatakiwa asahau kabisa mchango wake kwa watu, asifikirie heshima yake, apuuze elimu yake. Tusi gani kwa msomi wetu! Ni tusi hili ambalo ni miongoni mwa sababu za kukimbilia Ughaibuni, ambako kuna uwezekano wa kuyapata anayoyakosa kwao.
Binafsi, hadi hivi karibuni tu, nilikuwa nimefungika na mawazo kuwa msomi anayeihama nchi yake na kwenda kufanya kazi kwengine huwa ni mpungufu wa uzalendo kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha kwao. Nilipingana na kisingizo hiki, maana niliona ni kukimbia tatizo ambako hakusaidii utatuzi wake. Kama ni shida zilizopo petu, hapa ndipo pao, kwa nini wasingelikaa tukashirikiana pamoja kupambana nazo? Kwa nini wasikae kusaidia kuleta mabadiliko?
Hesabu yangu ilikuwa ni kiwango cha faida wanachokizalishia nchi wanazofanyia kazi. Ingelikuwa wapi leo Afrika, ikiwa faida hiyo ingelikuwa inazalishiwa hapa? Kwa mfano, vijana wangapi wa Kizungu kwa mwaka humaliza digrii zao kwa kusomeshwa na wasomi wetu? Au miradi mingapi huiandika kwa mwezi na kuzalisha mamilioni ya dollar na euro katika kutekelezwa kwake?
Sasa nina shaka na hukumu niliyokuwa nayo kwao. Na ni baada ya kuongoea na baadhi yao, nikiwa na msimamo kwamba wao wanakosea na kwamba nami nina wajibu wa kuwakosoa kama watu wangu. Mmoja ‘aliniondosha njiani’ tu, “Nitarudi.” Lakini mwengine hakuniwachia hivi hivi tu: “Ungeliniuliza kwa nini nimeondoka kwetu na sio kwa nini sirudi kwetu, labda lingelikuwa suali muwafaka zaidi!”
Akanitanabahisha kwamba, si kweli kuwa watu wa aina yake wanaondoka kwao kuzikimbia shida zilizopo, maana ni shida hizo ndizo zilizowalea na kuwasomeha hadi wakafika walipofika. Na pia ni shida hizo walizoapa kupambana nazo katika maisha yao yote ya masomo ili kuipa maana elimu yao katika maisha ya watu wao. Lakini linalowakimbiza ni kuwa ‘hawatakiwi’. Wanakanwa na nchi zao wenyewe, nchi za uzao wao. Na katika wakati huu ambao sisi ndugu zao tunawakana, kuna wenzetu wanaowatafuta kwa udi na uvumba.
Vipi msomi wetu anakanwa katika nchi ya uzao wake? Kwa kuwa hapewi kazi ya mamilioni ya shilingi? Kwa kuwa hapewi gari la kifakhari, wala nyumba nzuri kama wapewavyo wanasiasa? Hapana, hayo si makubwa kiasi ya kwamba akiyakosa anahiyari kupasamehe pao, lakini la muhimu zaidi kwake ni kupewa utambulisho wake na kutambuliwa kama msomi.
Kuna mifano mingi ya wasomi walioamua kurudi kwao, baada ya masomo, ili waje wafanye kazi kwa ajili ya mataifa yao, lakini walipofika wakakumbana na kejeli za wanasiasa visirani, ambao kwao wao msomi ndiye adui nambari moja.
Afrika kuna ugomvi usiokwisha baina ya wanasiasa na wasomi, maana wawili hawa kila siku huyaona mambo kutokea vipembe tafauti. Wakati mmoja huyaona kutokea kipembe cha kisiasa na kutaka kila kitu kifanywe kwa kufuata muono huo, mwengine huyaona kutokea kipembe cha kitaaluma, na haja yake ni kuyafanya mambo kupitia muono huo.
Wakati mwanasiasa anataka mtu amuendeshe, msomi anagoma kuendesheka na, hivyo, anakuwa hatari kwa nguvu za mwanasiasa. Siku zote watu hawa ni Lila na Fila. Henry Peter aliwahi kusema: Education makes people easy to lead, but difficult to drive; easy to govern, but difficult to enslave. Elimu huwafanya watu rahisi kuongozeka, lakini wagumu kuendesheka; rahisi kutawalika, lakini wagumu kuwatia utumwani!
Ubaya wa mambo kwa msomi, ni kuwa yeye huwa hana nguvu za kufanya maamuzi ambayo yatafuatwa hapo hapo. Mwanasiasa anazo nguvu hizo. Akisema mashine ya maji ifunguliwe Lumumba ikafungwe Bwejuu ili Mhishimiwa Sana akapate kufunguwa mradi wa maendeleo huko, jambo hilo litafanyika siku hiyo hiyo hata kama ni kinyume na ushauri na matakwa ya kitaalamu.
Msomi akiinuka kulisemea hilo, huyo anaanza kuonekana ‘mpinga maendeleo’, na mchochezi. Na hayaishii hapo tu, huenda siku kumi zijazo akakuta kibarua kimeshaota majani. Kisa? Kukidhi mahitaji ya kitaaluma badala ya mahitaji ya kisiasa!
Akiepukana na hilo, msomi wetu anakumbana na jengine kutoka system. Kwa mfano, mtu anarudi nyumbani baada ya kumaliza kuchukuwa mafunzo ya Uhandisi huko atokeako, lakini akifika anakabidhiwa chaki akasomeshe Kiingereza kwa wanafumzi wa Darasa la Saba. Mwengine aliyesomea masuala ya kilimo, anapangiwa akawe fundi wa vinu vya maji. Wapi na wapi?
Lakini kwa kuwa wanasiasa wetu wana ugomvi wa kudumu na wasomi hawa, basi si ajabu kuwa wanawafanyia haya kusudi washindwe na wapate la kuwadharaulia. Wawaite maprofesa uchwara, madaktari feki na majina mengine kama hayo ya tashtiti. Hiyo ndiyo mbeleko Afrika inayombebea msomi wake. Atadumuje?
Hayo ya msomi kupangiwa kazi kinyume kabisa na taaluma yake huenda yakawa madogo, lakini hebu fikiria mtu ambaye amepoteza miaka yake kumi kuchukuwa fani ya udaktari huko nje, anakuja hapa na kuamriwa kupiga deki hospitali, eti ni kumkomoa na usomi wake! Lipi tumfikirie atalifanya msomi huyu?
Lakini adui wa msomi wetu si mwanasiasa tu, hata jamii yenyewe anayokuja kuifayia kazi na kuishi nayo. Wengi wetu huwa tunadhani kupata fursa ya masomo ya juu kumempa fursa nzuri ya kuyatengeneza maisha na hivyo kumpa pia wajibu wa kutusaidia kwa hali na mali.
Kwetu, kuwa na digrii, kwa mfano, kunamaanisha kukunja mapesa na kuja nayo nyumbani. Anaporudi mikono mitupu, msomi huyu huonekana kayasaliti matarajio ya watu wake. Na akitaka ayatimize mahitaji hayo, basi lazima afanye kazi kuwatimizia haja zao. Na kazi ipi atakayoifanya hapa petu kuyakidhi mahitaji ya familia zetu kubwa?
Kwa hali hiyo, msomi wetu huwa amesukumwa ukutani, ambapo hana jinsi ya kung’amuka ila ajitolee muhanga kwa kufanya moja kati ya matatu haya: ama akae kupambana na mfumo kwa kucha na meno, au abadilike kwa mujibu wa mahitaji ya mfumo wenyewe au aikimbie nchi yake ya uzawa
Kila moja kati ya matatu haya yana gharama kubwa sana, na lolote atakalolifanya, hujikuta anajilaumu kwa kutolifanya jengine. Kwa mfano, kuamua kubakia na kuukabili mfumo uliopo ni kujikubalisha kukosa na kupoteza kila kitu. Ni kukubali kujiundia maadui wengi na wenye nguvu kuliko yeye kutoka tabaka la watawala. Anaweza kukosa hata mlo wa siku moja yeye na familia yake na mwisho wa hadithi akafa dhalili na madhulumu. Mifano ya wasomi wa aina hiyo ipo mingi sana.
Chaguo la kujibadilisha na kwenda sambamba na mahitaji ya mfumo uliopo ndilo linalofuatwa na baadhi ya wasomi tulionao nyumbani. Lakini chaguo hili huwa linamsuta msomi anayeheshimu maadili ya taaluma yake. Mfumo wetu, kwa hakika, ni wa kifisadi sana na kuwa fisadi ni kitu alichojifunza na kuamini kuwa ni kiovu. Sasa, kuishi kwa mujibu wa matakwa ya mfumo ni kukubali kuwa fisadi.
Tunao hapa wasomi na digrii zao, lakini ndio hao wala rushwa wakubwa na ambao huhongwa kuitikia Ndio Mzee ili waidhinishe mambo maovu kufanyiwa watu wao kwa jina la taaluma zao na, au, vyeo vyao. Ndio hao waliopitisha miradi ya rada, ndege ya raisi, mikataba ya IPTL na mengineyo lukuki nzima.
Hawa si wasafi na wala hawawezi kusafika madhali wamesimama na wanaishi na wachafu. Hawa ni wasaliti wa taaluma zao, wasaliti wa uelewa wao wenyewe. Wanaweza wasife madhulumu, lakini hawawezi kuepuka kufa madhalimu.
Na, mwisho, yule asiyeweza kuyastahamilia hayo yote hulazimika kupahama pao na kwenda ugenini. Huko ataweza kufanya kazi na kupata visenti vya kuwasaidia watu wake. Huko ataweza kuilinda na kuidumisha heshima yake kitaaluma. Huko kutamuepusha kufa dhalili au kufa dhalimu.
Lakini huko kutamnyima kwao, kunakiapoteza kizazi chake kinachokuja kuwa kigeni kwao pia. Atazaa watoto wasio utambulisho___ Waafrika sio wala Wazungu sio. Ndiyo akina hao tuwaitao Amefricans, Eurofricans au Asifricans. Watandawazi, labda tuwaite hivyo kwa Kiswahili. Na hilo ni poteo kubwa kwa msomi wa kipetu, ambaye kujitowa kwake muhanga kwa staili hii kunamkosesha, yeye na wanawe, titi la mama.