jump to navigation

Shujaa Nabwa anapambana, tumuunge mkono January 23, 2007

Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.
add a comment
Na Mohammed Ghassani
Kwa wiki ya pili sasa, mwandishi mkongwe wa habari nchini Tanzania, Ali Mohammed Ali (Nabwa), amelazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, mjini Zanzibar, akiugua ugonjwa wa pumzi unaosababishwa na mapafu kujaa maji. Hali yake inakwenda ikibadilika baina ya mbaya kidogo na nzuri kiasi.

Nabwa ni mwandishi wa kudumu wa gazeti hili katika safu yake, Tafakuri za Mzee Nabwa, ambamo amekuwa akichangiana uzoefu wa historia ya maisha yake na wasomaji wake, ambao lazima tuseme kwamba ni wengi mno. Umahiri wa Nabwa katika uandishi hauhitaji kuongezewa chumvi, na wasomaji wenzangu wa makala zake ni mashahidi wa hilo.

Kwa sisi wengine tunaojaribu kufuata nyayo zake, Nabwa anaendelea kubakia zaidi ya mzee kwetu. Huyu ni mwalimu na kiongozi wetu. Kwamba kila fani ina shujaa wake kwa mujibu wa maeneo yake. Katika eneo letu hili, Nabwa ndiye shujaa wa fani hii ya habari. Wanayemkumbukia zama za Dira Zanzibar, wanaweza kulithibitisha hili pasina shaka.

Wasiolikumbuka, Dira lilikuwa gazeti huru la kila wiki la Zanzibar lililokuwa likiongozwa naye. Mafanikio ya Dira pia hayahitaji kutiliwa chumvi. Lilizoa ufuasi wa kutosha na kutisha. Ulitosha kwa waendeshaji gazeti, lakini ulitisha kwa serikali. Ndani ya kipindi kifupi cha uhai wake, liliweza kuinua, kwa kiasi kikubwa, kiwango cha uelewa na mwamko wa Wazanzibari katika nyanja zote za maisha___ uchumi, siasa, historia na utamaduni.

Tuko tunaokwenda umbali wa kusema kwamba, hata kile kitendo cha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kulisakama gazeti hilo kwa kesi na hatimaye kulifungia na kumpokonya uraia Nabwa, ni katika mafanikio hayo makubwa ya Dira. Kwamba kwa kukataa kwake kuramba buti la watawala, Dira ilikuwa imejipambanua kutoka kundi la vyombo vya habari vinavyochunga maslahi ya mabwana tu, na kujidhihirisha kuwa chombo cha kweli cha kuleta mabadiliko na kinachochea ari ya maendeleo miongoni mwa jamii kama lilivyo jukumu la taaluma hii. Ikajijengea heshima.

Tukitaka kuwa wakweli wa nafsi zetu, basi tuko ambao hadi leo hii tunaendelea kufaidi heshima iliyojengwa kwetu na Dira. Na kwa kusema hivyo, sioni namna ambayo tunaweza kuizungumzia heshima hiyo, bila ya kumtaja na kumnasibisha Ali Nabwa. Binafsi naona fahari kubwa mno kunasibishwa naye. Naona fahari kunasibishwa na mtu ambaye alipambana na kusimamia kilichochapishwa na gazeti hilo hadi ukomo wa jitihada zake. Nampigia saluti mtu ambaye alipambana kwa ajili ya uhuru wangu wa kuandika na kupokea maoni.

Nakumbuka alipolumbana na Jaji Joseph Warioba, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) wakati huo, kuhusiana na madai ya SMZ kwamba Dira ilikuwa ikikiuka maadili ya uandishi wa habari. Ilivyoonekana Jaji Warioba alishaamua kusimama zaidi upande wa SMZ kuliko wa usuluhishi. Na kwa kuwa Nabwa alikuwa na hoja, akachanganya kujiamini kwake na ukali kidogo kuisimamia heshima ya Dira.

Hata kabla ya Dira kufungiwa, wengi wetu tulishajuwa kuwa hilo lingelitokezea tu. Tabia ya serikali yetu ya ukosefu wa ustahmilivu kwa hoja inayokinzana na mtazamo wake, haikuwa kitu cha ajabu. Mara nyingi, nakumbuka, tulikuwa tunajadiliana kabla ya kuchapa habari au makala ambayo tulishaiona kwamba ingeliigusa mishipa ya fahamu ya watawala. Lakini inapotokea tumekubaliana, ni Nabwa aliyekuwa akisema, “Mimi ndiye Mhariri Mtendaji. Ichapwe, liwalo naliwe!” Akatupa nguvu, tukasimama na kuingia mzigoni.

Huyu ndiye Nabwa aliyelala kitandani sasa katika wodi ya wagonjwa mahututi. Hadi SMZ ilipoamua kulifungia gazeti la Dira, ilikuwa ‘imeshaipata fresh’ na haikuwa tena na fahari ya kujigamba kumiliki habari zote za nchi hii. Tayari milango ya habari ilikwishafunguka, na tangu hapo haijapata kufungika tena. Ni Nabwa na Dira ndio waliokuwa wameifungua milango hiyo. Fahari iliyoje!

Hata sasa ambapo amekuwa na safu ya kudumu katika gazeti hili, ule mwangwi wa sauti za milango kufunguka unaendelea kusikika. Binafsi, mara nyingi napokea salamu za kumsifu Nabwa kwa simulizi zake zilizomo kwenye safu hiyo. Inafahamika kwamba, kuna wasomaji wengi ambao, baada ya kununua tu gazeti hili, hukimbilia kusoma ukurasa wa nne, kwenye Siku Moja Itakuwa Kweli, kabla ya hata kusoma ukurasa wa kwanza.

Naamini uongozi wa gazeti hili unapata heshima kuona kwamba miongoni mwa vitu vinavyolifanya gazeti hili la Fahamu Mwananchi kuwa hasa Fahamu ni yeye, Ali Nabwa. Fahamu nalo, kama lilivyokuwa Dira, linazidi kupata ufuasi kila kukicha na, miongoni mwa sababu nyengine zote, ni kwa kuwa muna Nabwa. Nabwa amekuwa kama ishara ya habari na mawasiliano katika nchi hii, na hasa Zanzibar ambako ameamua kuikita mantiki ya uandishi wake. Ni majaaliwa yake Mungu kwamba ishara hii hivi sasa imelala kitandani Mnazi Mmoja ikipambana na maradhi.

Kitu kimoja cha ziada, ambacho pengine hakijuilikani na wengi wetu, ni kwamba Nabwa anaamini mno juu ya kuwasiliana na watu. Ukimya na upweke si katika misamiati anayoipendelea maishani mwake ingawa, kwa mujibu wa simulizi zake, kuna mara nyingi alizolazimishwa kuwa katika hali hiyo na mfumo. Hata hivyo, hajapata kuuruhusu ukimya na upweke umlemee. Hata katika siku hizi za karibuni ambapo maradhi yamekuwa yakimpa tabu na akawa hawezi kuandika moja kwa moja kwa mkono wake, basi bado huagiza mtu aende na kompyuta nyumbani kwake ili amkaririe naye aandike.

Najua kuwa hakuna kitu kinachomkera Nabwa kama gazeti kutoka hali yeye hayupo kwenye safu yake. Ni mtu anayekerwa na hali ya kutokuwasiliana, incommunicado. Anataka kuwasiliana na kuendelea kuwasiliana hata pale kitandani alipo. Anataka kuendeleza mapambano na kuuvuja upweke na ukimya uliomo kwenye maradhi. Alifanya hivyo hata alipokuwa amefungwa jela pale Keko na Mwalimu Julius Nyerere. Aliwasiliana na wafungwa wenzake kwa ishara na hata kwa miguno na mipigo ya viambaza. Huyu ndiye Ali Nabwa aliye kwenye chumba cha wagonjwa mahututi akipambana na jaala yake.

Kama yeye aliyepo kitandani anapambana hivyo, sisi tulio nje tuna jukumu gani? Kwanza tuna jukumu la kibinaadamu. Kwamba huyu ni mja mwenzetu aliyepatwa na masaibu kama ambavyo yangelimpata yeyote kati yetu. Ugonjwa ni kinyume tu cha uzima, na vyote viwili ni dhati kuhusu maisha. Tunapaswa kumuombea kwa Mungu ampe afya ya haraka ili arudi nyumbani kuunganika na familia yake kuyafurahia maisha. Msaada huu uwe ni wa hali na mali. Hali ya kiuchumi ni mbaya kwetu sote, lakini penye dharura kama hii, waungwana huchangizana ili kukidhi haja.

Pili, tuna wajibu kama wanahabari wenzake. Kuwa mwanahabari hakumaanishi mwandishi wa habari tu, bali wote ambao mfumo wa habari unawahusu, na hao ni wengi. Tunapaswa kumuunga mkono katika mapambano haya. Tuwasiliane naye, maana sote tunajuwa kuwa pamoja na kuvuta hewa, uhai wa mwanaadamu huhuishwa na kuwasiliana. Pasipo mawasiliano, maisha huwa chapwa, yakakosa ladha na yasiwe na thamani.

Alipo Nabwa ni kitandani hospitalini___ mahala pakimya, papweke na palitima. Si mahala pa kukaa hata sekunde chache kwa mtu mwenye furaha na afya. Tuwasiliane naye, auhisi umoja na mshikamano wetu. Ayaone mapenzi na huruma zetu kwake. Ajuwe kuwa, hata kama yuko peke yake humo chumbani kimwili, kiakili na kiroho sisi sote tuko naye.

Tusisahau kwamba, Nabwa amekuwa akiwasiliana nasi siku zote kuuondoa ukimya na upweke wetu. Tangu akiwa kwenye Dira kisha An-Nur na sasa Fahamu, huyu ni mtu ambaye hajapata kuacha kuwa karimu kwetu, akitunywesha maji ya fikira kutoka kisima chake kisichokauka cha kumbukizi. Kwamba amekuwa akitufanya tuione dunia ya miaka 50 nyuma kana kwamba iko mbele ya macho yetu hivi sasa. Kwamba amekuwa nasi kutufumbua macho kuhusiana na historia yetu, akiupambanua ukweli kutoka giza la uongo.

Nabwa anapambana. Tumsaidie katika mapambano hayo kwa kuwasiliana naye na kuwasiliana na Mungu Muumba wetu.

Miaka 43 ya Mapinduzi: Kweli Zanzibar iko huru? January 23, 2007

Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.
add a comment

Mohammed Ghassani

Kwa mara nyengine tena, katika hisabu za uhai wangu, Mapinduzi ya 1964 yanaadhimishwa huku Zanzibar ikiwa kwenye lindi la umasikini wa mali na hali. Haidhuru maneno matamu na takwimu kubwa kubwa za kukuwa kwa uchumi ambazo watawala wanataka tuziamini, lakini mifano hai inaonesha kwamba Zanzibar inarudi kinyumenyume.

Nipige mfano mmoja mdogo wa taashira. Mwishoni mwa mwezi Septemba 2006 niliondoka Zanzibar kuja hapa Dar es Salaam kwa masomo, nikiacha mnara wa jengo la Beit-el-Ajab umewekewa miti kwa ajili ya matengenezo. Ni juzi tu, baada ya miezi mitatu na kitu ndiyo nimerudi nyumbani kwa mapumziko. Unajua kitu cha mwanzo kukishuhudia ni nini? Ile miti nimeikuta pale pale na jengo liko vile vile___ ishara kwamba Zanzibar yangu ilikuwa imekwama kwa miezi yote hiyo.

Hii ni ishara tu, si kila kitu kuhusu Zanzibar. Lakini huo ndio muakisiko wa hali ilivyo nyumbani. Kunarudi nyuma. Hali ni tafauti na Tanganyika ambako, nionavyo, kunakwenda mbele. Ishara nyingi zinasema hivyo___ tangu majengo hadi pirika za maisha. Si halali kusema kwamba hali ni nzuri sana (juzi imetangazwa kuwa ya 47 kati ya nchi 50 masikini duniani), lakini ikiwa wawili hawa ni wagonjwa, basi Zanzibar yuko kwenye sakaratil-mauti na Tanganyika anaweza angalau kujikongoja. Hivyo ndivyo miaka 43 ya Mapinduzi ilivyomfanya Mama yangu, Zanzibar___ mgonjwa zaidi kuliko ilivyomkuta.

Na huo ndio uhuru wetu, Wazanzibari, uliotokana na Mapinduzi hayo. Uhuru wa kuwa na skuli na vyuo visivyo elimu, hospitali zisizo matibabu, mifereji isiyo maji, maduka ya vyakula na masoko ya vitoweo lakini wengi wanashinda na njaa. Kila Mzanzibari, kama mwanaadamu mwengine, hutamani kusoma asiwe wajinga, atibiwe asife maradhi, ale asilale na njaa na, kindharia, watawala wanamwambia ana ‘uhuru’ wa hayo, bali kiuhalisia ‘hayuko huru’ kuyapata!
Kuwa huru ni kuwa na nyenzo na uwezo; na ndicho kilichopiganiwa na wazee wetu walipopambana kumkomboa mkwezi na mkulima wa Zanzibar. Ikiwa walimwaga damu yao kuikomboa nchi, basi ilikuwa ni kwa kumvua Mzanzibari minyororoni mwa dhiki na dhuluma kwa kubadilisha staili ya utawala na sio kubadilisha sura za watawala tu.

Waliofanya Mapinduzi, inaelekea, walichoshwa kuona watu wachache tu, waliokuwa na mahusiano na utawala, ndio pekee waliokuwa na fursa ya kuufaidi utajiri wa nchi, huku wengi wakibakia kuteseka ndani ya nchi yao. Ni akina akrabiina tu, tunavyoambiwa, waliokuwa wananufaika na kila jambo zuri___ matibabu, elimu, makaazi na maisha ya kiwango cha juu___ wakati makabwela wakiteseka kwa njaa, maradhi na ujinga.

Basi wazee wakadai uhuru. Walipoupata, wakaona haujatosha, wakafanya mapinduzi ‘kuwakomboa’ zaidi Wazanzibari wawe huru, kwa maana ya kupata haki zao, kuwa nazo na kuzimiliki, maana hizo ndizo nyenzo za kuyastawisha maisha. Ikiwa kuna uhalali wowote wa mapinduzi yale, basi ni huo.

Lakini hata baada miaka hii 43 ya mapinduzi hayo, tunajuwa kuwa tumesalitiwa. Yule mkwezi na mkulima aliyelengwa kukombolewa, hajakomboka. Bado anadhalilika vile vile. Ule uhuru wa kweli uliokusudiwa awe nao Mzanzibari, haujapatikana.

Kilichopatikana, badala yake, ni mabadiliko ya sura za watawala na mstari mwekundu wa mfarakano. Hilo ndilo linalotufanya tuamini kuwa bado Zanzibar, kama nchi, haijawa huru__ haijawa na uwezo na nyenzo za kupata, kuwa nacho na kukimiliki. Uhuru wa kweli uliopiganiwa na wazee wetu sio tulionao. Mapinduzi tunayoyasherehekea leo, hayabebi tena ile azma yake yaliyolengwa.

Yale yale yaliyotakiwa yaondoke miaka 43 nyuma, ndiyo yaliyopo sasa, tena kutokana na mabadiliko ya wakati na ongezeko la mahitaji, yapo kwa kiwango cha kutisha. Na ikiwa hivyo ndivyo, ni msamiati gani wa kuhalalisha kujiita kwetu huru?

Nitoe mifano. Wakati Zanzibar inapata uhuru wake mwaka 1963, hamani ya dola ya Kimarekani ikiwa ni shilingi saba, ilikuwa inaingiza kiasi ya shilingi milioni mbili kwa mwaka kwa kusafirisha samaki wakavu Tanganyika. Kwa sasa, hiyo ingelikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni tatu.

Mbali ya kuhakikisha kwake kuwepo kwa nafasi za kazi zisizopunguwa 500 kwa mradi huo tu, pato hili pia lilihakikisha kujitanua kwa Zanzibar kiuchumi. Miaka 43 baada ya Mapinduzi, sio tu kwamba Zanzibar haina tena inachozalisha kuiuzia Tanganyika, bali yenyewe inategemea yazalishwayo huku. Huko hakuitwi kwenda mbele. Ni kurudi nyuma. Na huo sio uhuru uliopiganiwa.

Hadi Mapinduzi yanafanyika, nchi pekee za Kiafrika zilizolingana na Zanzibar kwa pato kubwa la taifa zilikuwa Ghana na Afrika Kusini. Wakati huo, Zanzibar ilikuwa inatowa misaada ya chakula na pesa kwa nchi nyingine ulimwenguni, kama vile Yemen. Leo Zanzibar ya miaka 43 ya Mapinduzi ni sehemu fukara kabisa duniani. Wazee wetu hawakupinduwa ili tuje tuwe masikini!
Zanzibar haikuwa na uchache wa wataalamu. Ni aibu kuwa miaka 43 baada ya Mapinduzi, bado tunaagizia wataalamu wa sheria, kwa mfano, kutoka nje ya nchi, ilhali hadi Mapinduzi hayo, ni Sudan tu katika Kusini nzima ya Jangwa la Sahara iliyokaribiana nasi kwa wataalamu wa kutosha, na wa ziada, wa kizalendo. Ikiwa tumerudi nyuma kiasi chote hiki, ni fedheha kujiita huru.

Katika huduma za kijamii, hali ni mbovu hivyo hivyo. Miongoni mwa maazimio ya Mapinduzi ni kuwapatia wakulima na wakwezi makazi bora, huduma nzuri kwa wazee wasiojiweza, elimu bora zaidi, chakula cha kutosha na matibabu yanayomstahikia mwanaadamu. Huko nyuma, tunaambiwa, watu wengi walishindwa kuyapata hayo kwa kuwa, hata kama walikuwa na uhuru nayo, hawakuwa na uwezo wa kuyagharamikia.

Matokeo yake, watoto wengi wa kimaskini wakaishia kuwa wajinga kwa kutokumudu kwenda skuli. Watu wengi wakawa wanalala na njaa, au kwa ‘kugongeana mwiko’, katika vibanda vyao vya makuti, na hata wengine wakawa wanakufa kwa kukosa matibabu. Wachache waliokaribiana na watawala au waliojiweza kifedha, ndio walioyafaidi maisha.

Leo, miaka 43 baada ya Mapinduzi, kuna yapi Zanzibar? Si mfano wa yale yaliyotokea kabla ya miaka ya ’60? Wale wale watoto wa makabwela, waliozungukwa na skuli, wanakosa elimu bora kwa kuwa hawana uwezo wa kulipia. Skuli za serikali zipo, lakini zimefuiya na mfumo mzima wa elimu umeporomoka. Kupata elimu nzuri kunalazimu kulipia masomo ya ziada au kusoma katika skuli za binafsi, ndani na, au, nje ya Zanzibar. Na kwa kuwa hayo yote yanamaanisha pesa, na pesa ni adimu kwa wakulima na wakwezi, basi elimu bora haipatikani kwao!

Badala yake ni watoto wa wakubwa na wenye pesa zao, ndio wanaoipata hiyo elimu bora. Wengi husomeshwa nje ya nchi na wachache wanaosoma Zanzibar ni katika zile zinazoitwa international schools, ambako pesa za walipa kodi huyeyushwa kila mwezi.

Mwishowe, kwa kuwa kuipata kazi kunategemea kisomo mtu alichonacho, basi watakaokuja kupata kazi (ikiwa zipo) watakuwa ni hao hao waliopata elimu bora. Mtoto wa mkulima na mkwezi atarudi kule kule kwenye pingu na jembe la mzazi wake.

Wakati huu wa kusherehekea miaka hii 43 ya Mapinduzi, pita mitaani kwa makabwela ushuhudie hali ilivyo. Pita Miembeni, Mikunguni, Jang’ombe, na Sogea, uone maandamano ya madumu ya maji. Pita vijijini kwetu ushuhudie hali ya watu walio ‘huru’. Pita Mtende, Kojani, Kiuyu na Marumbi usikie harufu ya njaa ikikunukia puani mwako.

Lakini kejeli ilioje, huko Mazizini na mwenginemo muchache, watu wanakula na kumwaga katika madebe ya taka. Huko kunasherehekewa hasa miaka 43 ya Mapinduzi na uhuru wa mkulima na mkwezi. Huko ndiko uhuru na ukombozi ulikofika!

Hebu nenda jumba la wazee Sebleni, pale karibu na uwanja wa Amani, ukamuone huyo mkulima na mkwezi ‘alivyokombolewa’. Mzee wa miaka 70 amechakaa na kuchafuka kama lilivyo jengo lenyewe, anajikokota kwenda kutafuta makozi ya kupikia hadi karibu ya Mwera. Serikali iliyomvundika mule, imeshindwa kumtunza kikweli na, badala yake, anadhalilika. Miaka 43 iliyopita, huyu alikuwa ni mtafutaji uhuru, alikuwa mpiganiaji ukombozi; na sasa ni dhambi kumuita yeye kuwa ni raia huru!

Hebu tembelea hospitali zetu, zile tulizoahidiwa huduma bora na bure. Wakwezi na wakulima hawapatiwi muda wa kuangaliwa sawasawa na madaktari kwa kuwa hawana pesa za kuhonga. Na hata wakishaangaliwa kwa hayo macho matupu, hakuna dawa. Wao, wakulima na wakwezi, wanatakiwa kununuwa dawa za zaidi ya elfu tano, pato lao la mwezi mzima. Huo ndio uhuru walioupigania?

Wakati huo huo, huku wao wakiteseka kwa maradhi bila ya dawa, fedha nyingi zinatumika kuwatibu nje wale walio na fursa katika utawala, hata kama maradhi hayo yangeliweza kutibiwa hapa hapa kwa pesa kidogo au bure kabisa. Watakatifu hawa wanajuwa namna ya kuufaidi uhuru na ‘wako huru’ kufanya hivyo. Wana nguvu, uwezo na nyenzo za kuutumia uhuru wao. Wao ndio ‘waliokombolewa’ na Mapinduzi ya 1964.

Marehemu Jaramogi Oginga Odinga wa Kenya aliwahi kuandika kitabu na kukiita Not yet Uhuru, akimaanisha kuwa hata baada ya mkoloni wa Kiengereza kuondoka, bado Kenya haikuwa huru, maana waliochukuwa madaraka baada yake, walijigeuza wakoloni weusi na wakaila nchi yao wenyewe. Walikuwa wanaitawala nchi kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha ya umma, ufisadi na utumizi mbaya wa madaraka. Walikuwa wanaifakamia keki ya uhuru kwa matonge.

Nachelea kusema kwamba hali i vivyo kwa Zanzibar. Waliochukuwa madaraka baada ya Mapinduzi wameigeuza nchi hii kuwa shamba lao, mali yao na vizazi vyao. Wao peke yao ndiyo wameojihalalishia kuila keki ya Mapinduzi kwa staili wanayoitaka wenyewe. Wao peke yao ndio wanaopata makazi mazuri na ya kuridhisha, maji salama na safi, matibabu bure na bora, elimu ya kiwango cha juu na ya manufaa, chakula kizuri na cha kutosha, na mavazi ya kuvaa na kujipamba. Sisi, watoto wa wakwezi na wakulima, tungali kule kule walikokuwa wazazi wetu miaka 43 iliyopita. Kwetu, ni not yet uhuru!