jump to navigation

Hapana, Mkapa hukuwa Rais mzuri December 24, 2006

Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.
add a comment
Na Mohammed Khelef Ghassani

Nianze kwa kipande cha ushairi cha rafiki yangu, There Stands a Looser:

I may be the one when I loose
But you remain the same always
Neither you nor I____
Can deny the consequences
Nor can we tune otherwise
But____
As these counted minutes finish our day
Our children shall rise and say:
“Look, hey! There stands a looser”
And believe you me;
That looser wont be I

Ndiyo, there stands a looser. Tahriri ya wiki iliyopita ya gazeti la Fahamu Mwananchi ilikuwa inazungumzia kauli ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kwamba, pamoja na kasoro ndogo ndogo za kibinaadamu, alijitahidi kuiongoza nchi kwa amani na upendo na kwamba anapaswa kumshukuru Mungu kwa kumlinda.

Makala hii haiendi mbali na tahriri hiyo. Hoja ni ile ile: Mkapa hakuiongoza vyema nchi hii. Na ufuatao ni uthibitisho kwamba, kama kuna chochote chema ambacho Mkapa aliifanyia nchi hii, basi ni vile kuondoka kwake madarakani muda wake ulipofika kwa kutokuwa na ndoto ya kubadilisha katiba na kuendelea kubakia kama wafanyavyo wenzake.

Kwa mara ya kwanza, Mkapa aliyeingia madarakani kwa mgongo wa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliyedhani kwamba mwanafunzi wake huyo ataendeleza kile alichokiamini yeye (Mwalimu), alikuwa na staili ya aina yake ya uongozi (utawala?). Kwa mfano, zile siku za unyemi wa fungate yake madarakani, alikuwa akihubiri mno kaulimbiu ya “Ukweli na Uwazi”. Alikuwa akitaka nchi imuamini kwamba yeye ndiye hasa yule Mr. Clean wa Mwalimu Nyerere kwa kuwa mkali mno dhidi ya rushwa. Basi akianza fungate hiyo kwa kutaja mali zake alizokuwa nazo, kisha akawashawishi mawaziri wake, akina Waziri Mkuu Fredrick Sumaye, wafanye vivyo.

Hakuishia hapo. Akawataka wananchi wamuamini kwamba yeye ni mpambanaji kwelikweli dhidi ya ufisadi na rushwa kwa hivyo akawaomba wamtajie majina ya watu wanaowajuwa kuwa ni wala rushwa. Akaunda pia Tume ya Jaji Warioba kulihakiki suala lenyewe lote. Si unajuwa kuwa serikali iliyomtangulia ya Mzee Ali Hassan Mwinyi (Babu Ruksa) ilikuwa ‘imeminyiwa’ na wafadhili kwa madai ya kuwa kwake ovyo mbele ya ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi ulioota mizizi? Sasa otea nini kilitokea baada ya hashuo lote hilo?

Kwanza, baada ya kupelekewa majina ya ‘wala rushwa’ katika serikali yake, aling’aka kama mbogo kwamba watu wana wivu wa kike na, badala ya kuangalia maendeleo yao, wanaendekeza choyo cha kuona kila mwenye mali basi ameipata kwa rushwa. Akasema kwamba watu wasimpelekee majina tu, bali wampelekee ushahidi, hali anajuwa fika kwamba katika kutoa na kupokea rushwa kila jitihada huchukuliwa kuhakikisha kuwa hakuna nyayo za ushahidi inayoachwa. Kama ilivyo dini, rushwa ni imani. Ama uamini kama ipo au la.

Pili, ile taarifa ya Tume ya Jaji Warioba ikaishia kapuni (na kwa taarifa ni kwamba hii si tume pekee ya Mkapa ambayo ilimalizikia kiaina tu). Ikachapwa, bila ya shaka, katika magazeti, lakini mambo yakaenda taratibu mno. Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKURU) aliyoiunda ikawa ni showcase nyengine. Lilikuwa jibwa kubwa la kutisha lakini lilikuwa kibogoyo kisicho meno ya kutosha. Lawama ni kwamba, limepewa koti kubwa kuliko umbile lake. Huyo ndiye Mkapa kwenye rushwa.

Kihoro kilichomuingia Mwalimu Nyerere kwa kuangushwa na chaguo lake, naamini, kilisaidia kuzisogeza siku zake haraka kuelekea kuzimu. Si mchezo mtu wa heshima kama yeye kunyanyuka katika umri ule kuzunguka nchi nzima na kumnadi mtu wake, kisha mtu huyo akaja kumwangusha mwangusho wa kioo____ ulio vigumu kuungika tena. Mwalimu Nyerere hakuunga tena tangu Mkapa alipoanza kuyatekeleza madaraka yake.

Kisha kuna mkasa kama ule wa akina Jenerali Twaha Ulimwengu ambaye, licha ya kuwa mpiga debe wake mkubwa katika siku za kampeni, alipoanza kumuona anakwenda njia siyo naye kumsema kwa hilo, mara akatangazwa si raia. Nisisahau kwamba sakata la uraia wa Mzee wangu, Ali Nabwa, lilianza katika siku za mwisho mwisho za utawala wa Mkapa na kwa hakika alilijua vyema, lakini akaondoka na kuliacha kama lilivyo.

Kuna mauaji ya Mwembechai ya mwaka 1997. Shaka kwamba alikuwa ‘mdini’ wa kutupwa zilianza kujengeka hapa. Maana pamoja na serikali yake kufanya ilivyowafanyia waumini wa Kiislam ndani ya msikiti, bado alikataa kabisa kuunda tume ya uchunguzi wa sakata lile. Na hata alipotokea msomi mmoja, Dk. Hamza Njozi, kuandika kile hasa kilichotokea katika kitabu chake cha The Mwembechai Killings, serikali yake ilikipiga marufuku kitabu hicho.

Kuna kasheshe la Bulyanhulu ambako madai ya wazi ni kuwapo kwa kaburi la pamoja la watu waliofukiwa mgodini. Sio tu kwamba serikali yake ililikanusha lakini pia ilizuia vyanzo vyovyote vya habari kutoa taarifa hizo kwa ulimwengu. Huyo ndiye Mkapa katika haki za watu.

Kisha kuna hili suala kubwa kabisa la mauaji ya Januari 2001, Zanzibar, ambalo mwenyewe aliwahi kusema eti liliwahi kumkosesha usingizi na karibuni na mwisho wa utawala wake, alipokuwa ziarani Marekani, akasema kwamba linamsononesha katika siku anapomalizia uongozi wa Tanzania.

Mimi, hata katika siku za kuwapo kwake madarakani, niliwahi kutaka tumuite Mkapacratic, msamiati niliotaka umtofautishe na ule wa democratic. Bado ninaamini hivyo hivyo hadi sasa. Kwamba mfumo wake wa utawala ulikuwa ni mkapakrasia na sio wa demokrasia. Sababu yangu ni kwamba, huyu alikuwa akiamini sana juu ya nguvu ya vyombo vya dola katika utawala na sio nguvu ya wananchi. Mdomoni, alikuwa akisema kwamba watu ndio wenye nguvu, katika vitendo alikuwa akionesha kuwa yeye na vyombo vyake vya dola ndio waliokuwa Alfa na Omega wa maamuzi na madaraka.

Ni shakhsia hii ya ukapakrasia ndiyo iliyozaa mauaji yale ya 2001. Ndiyo iliyowafanya dada zetu wabakwe na ndugu zetu waikimbie nchi yao ya uzawa. Mkapa hakuwa aina ya Raisi anayekubali changamoto katika utawala wake. Basi ni hivyo tu.

Ndio maana, licha ya kuwa mbele ya watu wake aliowapenda na kuwahusudu, mataifa ya magharibi, alikuwa akitoa maneno ya kistaarabu na kidemokrasia, alipowageukia wananchi wake alikuwa akitoa ujuba wa kidikteta. Sote tunakumbuka kauli zake za kuapa kutumia nguvu ya dola kuzima nguvu ya umma ikiwa baada ya uchaguzi kuna watu watakaoamua kuandamana kupinga matokeo yatakayotangazwa na tume zake za uchaguzi.

Alikuwa anaonesha msimamo wake kwa Wazanzibari ambao ndio waliokuwa wamefikia maamuzi hayo. Na akautekeleza msimamo huo kwa kuleta Zanzibar wanajeshi na silaha nzito nzito ambao hawakuondoka mitaani hadi lile lengo alilolikusudia limetimizwa. Na ikiwa hivi ndio kuongoza nchi kwa amani na upendo, nahofia kama angelioongoza kwa vurugu na chuki ingelikuwa vipi?

Alimradi mifano ya Mkapa kutuendesha ovyo ni mingi sana tu. Na yote inamuharamishia kustaafu akiamini kwamba alikuwa mtawala mzuri, maana ukweli ni kwamba hakuwa. Hakuwa na uzuri wa kusifiwa, hata kama, inayumkinika sana, wale watu wake aliowapenda na wao kumpenda sana (watawala wa Magharibi) walijitahidi kumjengea sifa hiyo.

Ukweli ni kwamba, mataifa hayo ambayo kitu pekee yanachokijali kwetu ni maslahi yao ya kiuchumi, yalikuwa yamepata kutoka kwa Mkapa kiongozi wanayeweza kumtumilia kwa yao. Ikiwa ‘aliyagawia’ makampuni ya nchi zao eka kwa eka za ardhi yetu, wachimbe madini na wafanye watakavyo, hapakuwa na shida yoyote ikiwa wao watamlipa Mkapa huyo kwa kumsifu. Kwa kumfanya chibui chao.

Kwa mfano, kuna suala la ununuzi wa rada na ndege ya raisi. Hivi sasa polisi ya Uingereza inachunguza kashfa ya ununuzi wa rada hiyo kwa kuwa tangu mwanzo ilishaonekana kwamba kulikuwa na harufu kali ya rushwa.

La ndege ndilo lilitutukanisha nchi nzima. Waziri wake wa Fedha, Basil Mramba, akatwambia ingelikuwa sawa ikiwa hata kama sisi raia tungelikula udongo lakini ndege ya raisi ilikuwa lazima inunuliwe. Na ni kweli, nchi hii inayohisabiwa kuwa miongoni ya zile za mwisho kwa umasikini, ikanunua ndege ya kupanda raisi wake akienda kuomba misaada kwa wale ambao wenyewe hupanda ndege za kawaida kuja kwetu.
Kuna namna alivyomkingia kifua Waziri wake Mkuu, Fredrick Sumaye, ambaye kila kidole cha tuhuma kilikuwa kinamuotesha yeye kwa namna alivyokuwa na miradi ya ajabu ajabu. Akatutukana sote kwamba tuna wivu wa kijinga. Kwamba si kila kiongozi aliyepata mali (hata kwa njia za ajabu?) kwamba amekula rushwa au ameiibia serikali.

Kumbe ilikuwa anajenga kabisa ukuta wa kinga, maana hata naye mwenyewe, kama nilivyosema, aliondoka bila ya kutangaza mali yake aliyoichuma akiwa madarakani. Alishatwambia kabisa kwamba haimaanishi wizi wala rushwa kuwa na mali zaidi ya mshahara tunaokulipa sisi tuliokuajiri.

Basi kwa haya, na mengine mfano wake, ndipo wengine tunaona kwamba Mkapa hastahili kabisa kujifariji kwamba aliiongoza nchi hii kwa amani na mshikamano. Ni bora tu kwamba amekwenda. Ni bora tu kwamba yeye si tena kiongozi wetu, maana hakutukinai sisi kama raia wake. Ni bora tu kwamba anamalizia umri wake huko aliko na hivyo alivyo.

Lakini asitutafiri kutukumbusha kilio matangani, hali anajuwa kuwa msiba aliotuwachia umetushinda kukimaliza kilio chake hadi leo. Naasifanye hivyo, maana nasi tutainuka tuseme: “Oneni, there stands a looser!”

Saa ya Ukombozi ni hii December 16, 2006

Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.
add a comment
Na Mohammed Khelef Ghassani

HISTORIA inaonesha kuwa harakati za kijamii kujikomboa kutoka minyororo ya idhilali na dhulma zina mtandao na wigo mpana. Watawala wetu huwa hawapendi kulisikia neno ‘kujikomboa’ likitajwa katika siasa za sasa hivi kwa madai kuwa wakati wa Mwafrika kujikomboa umeshapita, maana hatawaliwi tena na mkoloni.

Huko ni kujipumbaza, maana tafsiri hasa za utawala wa kikoloni na ukombozi zimeepukana kabisa na mipaka ya kiwakati, kijiografia au ya kirangi kwa mtawala na mtawaliwa. Ama iwe jamii inapambana kujipapatuwa kutoka mikononi mwa mtawala wa kigeni au mtawala mzawa, mweupe au mweusi, sasa au zamani, Afrika au Ulaya, kote huko ni kujikombowa na harakati hizo ni ukombozi. (Soma An Economic Strategy for the Second Liberation of Africa, Babu, A. M: 1994).
Wakati wowote jamii inapokuwa chini ya utawala wa kimazonge, na kujitambuwa hivyo, hunyanyuka na kutafuta ukombozi wake____ iwe kisiasa, kiuchumi, kitamaduni au vyenginevyo. Harakati hizi zina nguvu na kasi kubwa ya kuzagaa na kusambaa mithili ya moto nyikani au maji kutoka mlimani. Mkururo wa matukio katika historia ni shahidi wa hayo. Mshairi mmoja, akifananisha nguvu ya harakati na ile ya maji, aliwahi kuandika:
Wayazuwiyaye mai, yasenende na ndiyaye.
Huoni hiyo si rai, kuyafanya yas’eneye?
Zuia uzuwiavyo, kila tobo yazibiye
Illa mai yashukavyo, i kubwa mno kasiye
Nawe sikiza yajavyo, isikize ngurumoye
(Angalia Malenga wa Uswahilini, uk. 18: Mdungi, A., 2001).

Ni kasi hii isiyozuilika ndiyo ambayo humuathiri kila mtu na kila kitu katika jamii iliyokumbwa na wimbi la harakati za mabadiliko. Huzifanya nyenzo na silaha za kufikia lengo kuwa nyingi. Ndio kama hivyo yalivyo maji yatiririkayo kwa kasi kutoka mlimani, yanazagaa mote na yanapenya kila mahali, na vitu vyote vilivopo juu ya mlima___ magogo, majani, udongo, mawe___ husombwasombwa na kuwa sehemu ya maporomoko.

Hapa petu, hivyo ndivyo ilivyokuwa wakati wa mapambano ya kudai uhuru kutoka kwa watawala wa kigeni, kuanzia mwishoni mwa miaka ya ‘40 hadi mwanzoni mwa miaka ya ’60. Wakati huo jamii ilitaka kujikomboa kutoka mikononi mwa watawala wa kigeni.
Watu walitaka wapate uhuru wa kujitawala na kujiamulia mambo yao wenyewe. Harakati za ukombozi zilijipenyeza kila mahali na zikaleta athari yake. Familia, miji, vijiji, viwanja vya michezo, elimu, sanaa, dini na, alimradi, kila mahali pakawa ni sehemu na ni taasisi ya ukombozi.
Ndiyo, kila taasisi ikafanya kazi yake vizuri katika mapambanao. Yalikuwa ni mapambano ambayo watawala wa kigeni walishindwa kuyahimili, ikawapasa kuondoka ilhali wakiwa na hamu ya kubakia. Walishindwa kubakia kwa kuwa kila mahali walipogeuka, palikuwa na mwito ule ule tu: “Ondokeni hatuwataki, tunataka kujitawala wenyewe!”
Kila mahali. Wakisoma magazeti, wanakuta hilo. Wakitembea njiani, wanasikia hilo. Wakipita mitaani, kuta za majumba zimechorwa hilo. Pakiitishwa mikutano ya hadhara, dharura au faragha, wanasikia hilo. Hata pakiimbwa nyimbo, wanasikia hilo hilo. Popote, momote na kokote, sauti ni moja tu: “Fungasheni na ondokeni, ondokeni!” Yakawashinda!
Hatimaye, matukio manne yaliyofuatana yakawa ndiyo athari iliyobakia kwa harakati zile za ukombozi kwa Watanganyika na Wazanzibari: Uhuru wa Tanganyika wa 1961, Uhuru wa Zanzibar wa 1963, Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa 1964.
Mambo haya manne, licha ya tafauti ya maoni iliyopo juu ushiriki au utoshiriki wa wananchi kwayo, hayawezi kuwachwa bila ya kuhusishwa na harakati za ukombozi zilizoendeshwa na raia.
Sasa ni miaka mingi tokea kizazi kilichopita kiendeshe harakati hizo na kufanikiwa kupata waliyoyapata, kubwa zaidi likiwa ni huko kujivua makuchani mwa mtawala wa kigeni. Hao walikuwa ni wazazi wetu. Nakumbuka nyimbo tuliyokuwa tukiimba skuli: ‘Sisi sote tumegomboka kwa ndugu zetu walopotea’. Ndiyo, wao ndio waliotukomboa!
Lakini kumbe kuondoshwa kwa mtawala mgeni haikuwa mwisho wa harakati za kujikomboa kisiasa na kiuchumi. Raia waliojikusuru huko nyuma kuikomboa nchi hii walisahauliwa siku moja tu baada ya ukombozi kupatikana. Wao na sisi vizazi vyao tumekuwa tukirithishana mashaka, tabu, idhilali na mateso.
Na watawala wapya ambao___ kinyume na wale wageni waliokuwapo wakati wa wazee wetu____ ni wazawa, wanarithishana vyeo, uluwa, mali na israfu. Yale yale aliyoyafanya mtawala mgeni, ndiyo ayafanyayo sasa mtawala mwenyeji. Al-watan kabisa! Ni kwa sababu hiyo, hivi sasa, karibuni nusu karne nzima tokea watawala wa kigeni kuondoka, harakati nyengine za kujikomboa zinazagaa kwa kasi ile ile ya mporomoko wa maji kutoka mlimani.
Vizazi vya wale raia waliowaondosha watawala wa kigeni vinajihisi kuwa thamani ya mapambano ya wazazi wao imepotoshwa na kudharauliwa. Wanaona kuwa damu ya wazazi wao imebezwa na kusalitiwa (Fungate ya Uhuru, uk. 5, Khatib, M. S, 1985).
Sasa nao wanataka mabadiliko. Na kama walivyofanya wazazi wao katika harakati za kujikomboa, nao wanazisambaza harakati hizi katika kila pembe na katika kila uwanja. Ni vile vile tu, hapana jipya.
Ukifungua gazeti, ukiangalia televisheni, ukisikiliza nyimbo, ukihudhuria mkutano, ukikaa kijiweni na wash’kaji au barazani na wazee, ukienda uwanjani kuangalia mechi, ama kwenye mhadhara wa kidini, mote humo kauli ni moja tu, ya mabadiliko.
Kasi ya harakati ina nguvu za ajabu, na kwa kweli haizuiliki. Ikifungiwa mlango huu, basi hujifungulia yenyewe milango mingine. Mtawala akiwazuia watu wasifanye mkutano kwa kuwa katika mkutano huo atapingwa, basi watampinga kwa kutumia chombo chengine____ gazeti, televisheni au redio, na sasa kuna mitandao. Mtawala akikifunga chombo cha habari, atapingwa kupitia michezo. Na hata wakizuiliwa hapo, watatoboa kwengine tu.
Katika wakati kama huu, kila pahala na kila mtu, ama kama mmoja mmoja au katika ujumla wao, ni taasisi nzima na kamili ya harakati. Sijuwi watawala wetu watavifungia vingapi na watazuwia wangapi, ikiwa hata ndani ya tabaka la watawala wenyewe, munajengeka ghoba la harakati? (Fuatilia kuibuka kwa chama kipya cha SAFINA hapa Zanzibar).
Namna kasi na nguvu hii ya harakati za ukombozi ilivyozagaa na kuenea kila sehemu, ni sawa na vile nyumba inavyokuwa imekumbwa na hitilafu za umeme kutoka katika laini kubwa ya kusambazia umeme. Kila kitu na kila sehemu katika nyumba hiyo huwa yenyewe ni umeme. Ukigusa dirisha, shoti. Ukigusa mlango, shoti. Ukigusa kiambaza, shoti!
Wakati natayarisha makala hii, nilisikia nyimbo moja mpya ikiimbwa na mwimbaji maarufu wa muziki wa kizazi kipya Joseph Haule (Profesa J). Nyimbo hii inaitwa Siyo Mzee. Hapa sikusudii kufanya uhakiki wa kifasihi, lakini kutokana na maudhui yake, nimeonelea kuwa huu ni mfano halisi wa jinsi kasi ya harakati za ukombozi inavyosambaa kila mahali na kwa kila mtu. Hata katika kumbi za starehe, ambako huko nyuma usingelitarajia kukuta kitu zaidi ya ulimbwende na kulewa starehe za maisha, nako pia kuna shoti! Sijuwi vifungiwe vingapi?
Kwa wale wanaofuatilia muziki huu, ambao ni maarufu zaidi miongoni mwa vijana, wanajuwa kuwa huko nyuma mwimbaji huyu huyu aliwahi kuimba nyimbo aliyoiita Ndiyo Mzee. Ile ilikuwa ni kejeli kwa raia waliolevywa na kasumba za kitawala kiasi ya kwamba huamini kila wanaloambiwa kwa hishima na taadhima. Ilikuwa ni nyimbo iliyowataka wananchi wajihakiki na wajitathmini wenyewe na wakati huo huo kuwaambia watawala kuwa mbinu yao imeshajuilikana, nayo ni hii ya kuwafanya watu wawaitikie Ndiyo Mzee tu kila siku.
Lakini Siyo Mzee ni kinyume. Hili ni suto kwa watawala. Inawaonesha kuwa ile Arubaini yao ndiyo imewadia. Kwa kweli, hii ni nyimbo ya harakati za ukombozi. Inachora taswira ya unafiki wa wanasiasa walio katika tabaka la utawala. Hao ndio wale wanaopanda majukwaani kila baada ya miaka mitano kuwaomba kura wananchi na kuwaahidi mambo milioni, lakini wasitekeleze hata moja.
Hao ndio wale wanaoponda maraha kwa mapesa ya walipa kodi wa nchi hii: wakulima na wafanyakazi, na kisha kuwatupa. Kwao wao watu hawa, thamani ya raia ipo katika kuwapigia wao kura tu. Wakati wote wa upigaji kura, wao na raia huwa dam’ dam’, lakini baada ya hapo, wanakuwa mbali mbali mfano wa mbingu na ardhi. Wasaliti wakubwa!
Kutoka Ndiyo Mzee hadi Siyo Mzee, Joseph Haule anaonesha kuwa jamii imebadilika sana na kwamba sasa ni saa ya ukombozi. Katika Ndiyo Mzee wananchi walikuwa mbumbumbu, lakini katika Siyo Mzee wananchi wameshakarambuka.
Pale mwanzo raia walikuwa wamezugwa na maneno ya kiongozi wao, tuseme walikuwa na nidhamu ya woga, lakini sasa raia hawa hawa wamekwishang’amua kuwa kiongozi wao anawadanganya. Sasa hawako tayari kumkubalia mbabaishaji huyu. Wanamwita katika kikao cha dharura na kumuuliza kuhusu zile ahadi alizowaahidi wakati wa kampeni.
Kwa mfano, katika Ndiyo Mzee, aliwaahidi wapiga kura wake kuwa angeliwapatia askari polisi vifaa vya kutosha, zikiwemo helikopta kila askari na yake, kusudi waweze kupambana na ujambazi ulioenea. Sasa anapoulizwa ziko wapi zile helikopta, kiongozi mbabaishaji anajibu:

Nafikiria kuanzisha kwanza chuo cha marubani
Vyenginevyo mutapata ajali nyingi hewani
Baskeli hamujuwi kuendesha, helikopta mutaendeshaje?
Kila mtu aendeshe yake, huko angani itakuwaje?

Anapoulizwa na wakulima ile ahadi yake ya kuwapatia matrekta imefikia wapi, kiongozi huyo muongo anajibu:

Wakulima mngeendelea kwa kutumia jembe la mkono
Serikali haina hela, bajeti imefika kikomo
Naona kilimo cha mkono kinaendelea vizuri
Jamani kazeni mikono, endeleeni kukaza msuli!

Katika jumla ya ahadi alizozitowa katika Ndiyo Mzee, ni kuwa angelisambaza mabomba yanayotowa maji na maziwa nchi nzima (wakati sasa hata hayo ya maji tu hakuna). Anapokumbushiwa hili, anakuwa mkali:

Jamani naomba muulize maswali ya kiutu uzima
Mabomba kutoa maji na maziwa haiwezekani
Mulininukuu vibaya, nasisitiza haiwezekani!

Lakini ahadi kubwa kuliko zote aliyowahi kuitoa katika Ndiyo Mzee ni kwamba ikiwa ingelitokezea hali ya maisha kuwa ngumu, basi yeye angelikuwa tayari kugawana na wananchi kile anachokipata. Hiki kilikuwa ni kijembe cha mwisho kiashiriacho namna watawala wetu walivyo wanafiki wa kupindukia. Naye anapouliziwa hilo, anang’aka kwa ukali:

Eeh! Kugawana vya kwangu hilo suala litakuwa gumu
Familia inanitazama, ebo! nina majukumu
Imeandikwa: kila mtu atabeba msalaba wake
Kila mbuzi ale kwenye urefu wa kamba yake

Kikao hiki cha dharura kinamalizikia kwa vurugu. Wanachi wenye hasira kwa kudanganywa na kufanywa watoto na mtu waliyemchaguwa kwa kura zao wenyewe, wanachachamaa. Sasa kila alisemalo mtawala huyu, wao haawakubalianai nalo:

Wananchi tuko pamoja? ‘Siyo mzee’
Watanzania tumeelewana kule? ‘Siyo mzee’
Washika dau na wapiga kura pale? ‘Siyo mzee’
Enh!? ‘Siyo mzee’
Eti!? ‘Siyo mzee’
Wakulima tuko pamoja pale? ‘Siyo mzee’
Wanafunzi tumeelewana kule? ‘Siyo mzee’
Mabaamedi na mapolisi pale? Siyo mzee
Enh!? ‘Siyo mze’e
Eti!? ‘Siyo mzee’.

Na kama ilivyo kawaida ya watawala wetu wanapoona kuwa hasira ya umma inawajia usoni pao, hutumia jeshi la polisi kuikandamiza. Mwisho wa nyimbo hii, kunachorwa picha hiyo hiyo. Mwenyekiti wa kikao cha dharura anawaomba maafande wawasaidie kuwanusuru na ghadhabu ya umma!

Nilipomaliza kuisikiliza nyimbo hii nilikumbuka yale maneno maarufu: Saa ya Ukombozi imewadia. Lakini kwa hapa petu sio tena suala la kuwadia, kwa kuwa hapo mwanzo saa hii hii pia iliwahi kufika, isipokuwa sasa ni kujirejea tu. Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa: Saa ya Ukombozi imerejea!

Makala hii ilichapishwa kwa mara ya mwanzo katika gazeti la Dira Zanzibar, mwaka 2003

Maalim Shamsi, hoja sio tena Zanzibar kumezwa, ni kumezuliwa! December 16, 2006

Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.
add a comment
Na Mohammed Ghassani

HOJA kwamba Tanganyika inatumia Muungano wa Tanzania kuimeza Zanzibar si mpya hata kidogo. Ni kongwe na ina mashiko. Ilianza kujengwa zamani, tokea 1964. Tokea wakati huo hadi leo, hoja hii imekuwa ikitetewa na kuchambuliwa kwa dalili na mifano ya kutosha kiasi ya kwamba imeshazoeleka mno vichwani mwetu.

Muokote Mzanzibari yeyote leo hii, ama kutoka pale Dada Njoo- Darajani, Kizimkazi- Mkunguni, Mapinduzi- Mkoani au Maziwa Ng’ombe- Micheweni, na umuulize ni ipi nafasi ya Zanzibar katika Muungano huu, atakujibu: ‘kutawaliwa’ au atakupa neno lolote mfano wa hilo___ kumezwa, kuburuzwa, na kadhalika.
Kwa hivyo, hoja hii imefahamika vya kutosha na imejengeka vichwani mwa watu. Walioitoa, wamefanikiwa. Imekuwa kama mbegu iliyopandwa: imechipuwa, imekuwa na sasa inamea!
Na mashiko ya hoja hii hayapo katika umaarufu wake tu, yaani sio ile inayoitwa katika Falsafa Argumentum ad Populum, bali yapo katika ule ukweli inayouwasilisha. Yaliyotahadharishwa na hoja hii miaka 40 iliyopita, ndiyo yanayotokezea leo.
Kwa bahati mbaya sana ni kwamba kile ambacho bado hakijafanyika, tokea wakati huo hadi sasa, ni dhamira ya kweli ya kuifanyia kazi hoja hii. Na hii ni kutokana na mapuuza na dharau za watawala wetu.
Ni mapuuza, maana wanaona kuwa hoja hii itakuwa ikiibuka na kuzama yenyewe kwa yenyewe na hatimaye itakufa kifo cha kawaida (natural death) tu. Na ni dharau, maana wanaamini kuwa hata kama hoja hii itaendelea kudumu, Wazanzibari wenyewe ni wachache kulinganisha na hao waliounganishwa nao na, basi, hawatakuwa na nguvu za kuweza kulazimisha vyenginevyo visivyokuwa hivi vilivyo sasa. ‘Waache Wazenji waseme tu, maji ya moto hayaunguzi nyumba!’
Hilo ni koseo. Kwanza, katika jambo kama hili, Wazanzibari si maji, bali ni cheche za moto. Hakuna asiyejuwa kuwa Zanzibar ni kituo cha usambazaji___ usambazaji wa kila kitu. Historia inaonesha kuwa itikadi, dini, biashara na hata misimamo mbalimbali inayoathiri maisha ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, ni vitu vilivyoanzia hapa na kusambazwa ndani ya Bara la Afrika kupitia Tanganyika. Kwa hivyo, uwezekano wa zumari kupulizwa tena hapa, na wa Maziwa Makuu wakaicheza, bado ungalipo. Lazima watu watanabahi hilo!
Lakini, pili, ni koseo kwa kuwa jambo kubwa kama hili linalohusu khatima ya nchi na uwananchi wa wananchi wake, halifunikiki kombe kiasi hicho. Haliwezi kupuuziwa na kudharauliwa namna hii. Hili ni jambo la watu na hii, Zanzibar, ni nchi yenye watu wake. Basi ni wazi kuwa hoja hii itakwenda ikijirudia hadi moja lijuilikane___ ama khatima ya kuwa au ukomo wa kufana!
Kwa hivyo, si kitu cha kushangaza kwamba leo hii Wawakilishi wetu katika Baraza wanaitaka serikali iifanyie kazi hoja hii. Lakini cha kushangaza ni kwamba Waziri Kiongozi, ‘Msomi’ Shamsi Vuai Nahodha, ndio kwanza anawataka wawakilishi hao wajenge hoja kuhusiana na matatizo ya Muungano na sio kutoa malalamiko tu kuwa upande mmoja (Tanganyika) unaumeza mwengine (Zanzibar).
Akina mie tunajiuliza: “Hivi wahishimiwa wetu wajenge hoja ipi tena?” Kwamba, tuonavyo sisi na ambavyo ndivyo vilivyo, ni kuwa hiyo hoja tayari imeshajengeka kwa premises na conclusion zake?
Ushahidi kuwa hoja hiyo ilijengwa na kujengeka ni haya matukio ambayo yamekuwa yakiendelea kutokea tangu Aprili 1964 hadi sasa. Kutokea mambo 11 ya Muungano hadi 22, yaani ongezeko la asilimia mia moja, na yote yako dhidi ya Zanzibar kama nchi huru, ni uchambuzi na ithibati kwamba hoja hii ni madhubuti (sound argument).
Hapa ifahamike kuwa matukio haya, kama yalivyokuwa yakipigiwa mifano na wahishimiwa Wawakilishi wetu mule Barazani, ni uchambuzi na ithibati tu kwa hoja iliyokwishajengwa zamani mno. Yenyewe si hoja inayokusudiwa hasa, kama alivyoyachukulia Msomi Maalim Shamsi.
Wawakilishi wetu waliposema, kwa mfano, kuwa uchumi na biashara ya Zanzibar hivi sasa ni vitu vinavyoendeshwa kwa maamuzi kutokea Bara, hawakuwa wakijenga hoja mpya. Walikuwa wanatoa moja kati ya shuhuda nyingi zinazothibitisha hoja kongwe kwamba Zanzibar, kama nchi huru, basi katika Muungano huu haina lake jambo___ imekufa dungu msooni. Ni nchi yenye uhuru lakini siyo huru!
Changamoto iliyopo mbele ya msomi na mwalimu wetu huyu, kwa hivyo, akiwa kama kiongozi wa shughuli za serikali Barazani na pia akiwa na dhamana kubwa katika serikali anayoiongoza, sio kuibomoa hoja hii ya Zanzibar kumezwa na Tanganyika, maana haibomoki wala haivunjiki, bali ni kujenga hoja ya kuimezua Zanzibar___ kama kweli ni mjenzi wa hoja____ kwamba tayari Zanzibar yake imeshamezwa!
Na wala asidanganyike kwamba umezuwaji wa Zanzibar umo katika kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Fedha au kupewa asilimia 4.5 ya mgao wake wa misaada na serikali ya Muungano tu. Hivyo visimdanganye kwa kuwa vyenyewe ni vijimambo vidogo vidogo, ambavyo vinafanywa sasa ili kuuviza huo mchakato wa umezuwaji, wanaouona kuwa umeanza.
Umezwaji wa Zanzibar haukuanzia katika vijimambo hivi___ vyenyewe ni matokezeo tu ya kumezwa huko____ na, basi, umezuwaji wake hauwezi kuanzia kwavyo. Suluhu ya Zanzibar katika Muungano haimo katika Tume ya Fedha wala katika hiyo 4.5% ya mgao, bali imo katika siasa inayouzunguka na kuuendesha Muungano wenyewe. Mwenye siasa hizi ndimo mulimo na tatizo lenyewe.
Hapa nazungumzia siasa kwa maana yake halisi, yaani nguvu na maamuzi. Hali ya kuwa na nguvu na uwezo wa kuzitumia nguvu hizo katika kufanya na kuyasimamia maamuzi, huko ndiko kufanya siasa. Na hiyo ndiyo siasa.
Kwa maana hiyo ya siasa, Tanganyika, kwa jina la Muungano imeitawala Zanzibar. Inaifanyia maamuzi na inatumia nguvu zake kuona kuwa maamuzi hayo yanatimizwa na yanatimia. Hilo halijali ikiwa ama maamuzi hayo yanaendana au hayaendani na hali halisi ya Zanzibar kijiografia, kisiasa, kiuchumi au kiutamaduni. Linachojali ni kuendana kwake na matashi ya Tanganyika tu.
Sitii chumvi na wala sikathirishi maneno kusema kuwa mipaka na thamani ya uhuru wa Zanzibar imo ndani ya mipaka ya matashi ya Tanganyika, kwa jina na kwa baraka za Muungano. Nje ya hapo au kinyume cha hivyo, hapana Muungano____ kwa tafsiri hii ya Muungano tulionao. Hivyo ndivyo siasa za Muungano zilivyo, na hapo ndipo penye uhalali wa hoja hii ya kumezwa kwa Zanzibar na Tanganyika.
Kwamba Zanzibar haina nguvu za kufanya maamuzi yake yenyewe wala uwezo wa kuyasimamia maamuzi hayo. Na kama haina nguvu katika maamuzi yake, maana yake ni kusema kuwa imemezwa, imetawaliwa.
Zanzibar haiwezi kujitungia sera za kuinua uchumi wake kama Zanzibar na kutaraji kufanikiwa kama Zanzibar, maana baada ya yote nguvu za utekelezaji wa sera hizo lazima ziende sambamba na maslahi ya Tanganyika, kwa jina la Muungano. Kwa mfano, haiwezi kujiundia mfumo wake wa kodi kando ya huu wa Muungano kwa kuwa haina nguvu hizo. Zanzibar haina nguvu kama nchi, kwa kuwa imeamuliwa iwe ni kijisehemu tu cha jinchi!
Hapo ndipo hata ile shaka kuwa pana azma ya kuundwa kwa serikali moja ya Tanzania na kuiua kabisa serikali ya Zanzibar inapopata uhalali wake. Waache akina msomi na mwalimu wetu wakatae, ati kwa kuwa katiba inasema wazi ‘kutakuwa na serikali mbili, ya Zanzibar na Tanzania.’ Kwao wao, wanataka kila mtu akiamini kile kilichomo katika katiba, hata kama anachokishuhudia katika uhalisia ni kitu tafauti.
Ni kweli, panapohusika katiba iliyopo sasa, serikali moja haionekani ndani yake. Lakini panapohusika uhalisia, serikali moja inaonekana kila mahali. Haihitaji kwenda kwenye maabara ya kisayansi kulitafiti hilo. Uangalie tu utendaji kazi wa serikali zetu mbili, kisha fanya tathmini hata ya kiwango cha chini kabisa (the least-effort-evaluation), na nina hakika utafikia hitimisho (conclusion) la kuwepo kwa serikali moja.
Hakuna usomi hata mmoja ulimwenguni utakaotafautiana na zile ziitwazo basic facts kwa kuzingatia theoretical facts. Hapa nakusudia kusema kuwa kilichomo katika katiba zetu ni ukweli wa kinadharia tu (theoretical), ambao mara nyingi huthibitishwa vyenginevyo na ukweli halisi (basic). Kwani ni mara ngapi hata hao viongozi wakubwa wa serikali huvunja katiba za nchi kwa matashi yao? Tupige mifano mingapi kulithibitisha hilo?
Sijuwi ni nadharia gani ya kisayansi, ama iwe Applied Science au iwe Social Science, inayokiuka misingi ya ukweli halisi. Msomi na mwalimu wetu huyu, Mhe. Shamsi, sijuwi kaegemea ipi? Kwa maoni yangu yasiyo na hata chembe ya usomi____ kwa kuwa mimi si msomi___ ni kuwa hata kama hakitajwi popote katika katiba, tuna kiwango kimoja tu cha serikali, na serikali hiyo ndiyo yenye huo userikali wote mikononi mwake. Kwangu, sio kuwa serikali moja inakuja, bali tayari (kimatendo) imeshakuwepo.
Labda, Msomi Shamsi, alikuwa aulizwe kwa nini pameundwa serikali moja bila ya Baraza la Wawakilishi kujulishwa na sio kuambiwa kuwa pana khofu ya kuundwa kwa serikali moja. Hapo angelielewa!
Serikali, kwa maana ya chombo cha utawala chenye maamuzi ya juu kuhusu khatima ya taifa, ni ya Muungano. Khatima ya Zanzibar inaamuliwa Dodoma. Nani aongoze, vipi aongoze, kipi kiwe na kipi kisiwe hapa Zanzibar ni kutokana na amri, maagizo na maelekezo kutoka huko kwenye serikali yenye userikali.
Kwa hivyo, kuambiwa kuwa tuna serikali mbili, huo ni u-wili mtakatifu wa vitabuni mwetu tu. Wa kinadharia tu. Kwenye uhalisia, kuna serikali moja tu inayotenda na kutawala. Kuna u-moja wa milele!
Siasa hii ya mkubwa kummeza mdogo ndiyo iliyouzunguka Muugano huu na ndiyo waliyoikhofia Wazanzibari tokea zamani. Huu Muungano haujaanza kukosolewa leo. Kwa bahati mbaya, huko mwanzo utawala ulikuwa ni wa mkono wa chuma zaidi kuliko hivi sasa. Wengi walizizungumzia khofu zao hizi vibuyuni, na wale wachache waliothubutu kuzisema wazi, waliishia pabaya.
Sasa ni zama mpya. (Shukrani kwa uhuru zaidi wa kujieleza, na ole kwa wanaoonekana kutaka kuturudisha kule kule kwa kutiwa shemere na bakora mbili mbili mgongoni. Inshallah, huko hatutarudi!) Sasa ni wakati wa umma kutumikiwa na sio kutumikia. Sasa umma unapokuwa hauridhishwi na jambo fulani, hata kama jambo hilo linapendwa mno na watawala wao, hulisema kwa sauti na nguvu zote. Sasa ni zama za watawala kuakisika kwa matakwa ya umma na sio umma kuakisika kwa matakwa ya watawala.
Matakwa ya Zanzibar ya sasa ni kuwa na nguvu zaidi za kufanya maamuzi na uwezo wa kuyasimamia maamuzi hayo. Ni kuwa na uwezo wa kujipangia mustaqbal wake na kuhakikisha kuwa inaufikia. Kwa mfano, Vision 2020 haiwezi kutekelezeka katika hali ya sasa ya Muungano. Lazima hali hii ibadilike kwa haraka.
Hii haimaanishi, na wala haitamaanisha hata kidogo, kutoka nje ya Muungano na Tanganyika, lakini itamaanisha kutokuwa mfano wa koloni la Tanganyika. Maana, kuwa katika muungano ni kitu kimoja na kuwa chini ya ukoloni ni kitu chengine. Na lazima tukubaliane kwamba kumekuwa na mambo mengi sana yanayodhihirisha kuwa Zanzibar imetawaliwa na Tanganyika kuliko kuiita nchi huru iliyo katika muungano na nchi nyengine huru.
Nani atayapeleka matakwa haya mbele na kuhakikisha kuwa yanatimia? Bila ya shaka ni Wazanzibari wenyewe. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuona kuwa anaifanyia jambo la kheri nchi yake kwa kutoa mchango wake katika kuimezua. Mwenye kalamu aandike, mwenye chaki naasomeshe na mwenye nafasi ya kuingia vikaoni, naanzishe mdahalo na, au, aendeleze ule uliokwishaanzishwa.
Sote natuelewe kuwa hilo la siasa za Muungano ndilo tatizo letu la pamoja. Na hili nawashajiisha hata ndugu zetu wa Tanganyika waliangalie kwa muktadha huo huo. Kwamba sisi hatuna tatizo la kuungana nao, bali siasa za kuungana huko ndizo zinazotutatiza. Kwa pamoja, tunaweza, kwa haraka na kwa ufanisi kabisa, kuzirekebisha siasa hizo bila ya kuuathiri Muungano wenyewe.
Makhsusi hapa naelekeza kauli hii kwa wenzetu wote walio katika chama kilichokamata dola hivi sasa. Wao, kwa siku nyingi, wameuchukulia Muungano kuwa ni suala nyeti kuweza kuzungumzika. Ndio maana, kuliibua suala hili vikaoni mwao kulihitaji kwanza kuwa mpinzani wa CCM na serikali zake. Sasa nawaache woga wao wa ‘kukatwa vichwa’!
Kwamba sasa imeshabainika kuwa kinachohitajika katika kulizungumzia hili ni kuwa Mzanzibari au mwenye kuipendelea kheri Zanzibar tu, na si zaidi wala pungufu ya hilo. Hii ndiyo maana waliolichangia hili Barazani mara hii hawakuwa wapinzani tu, bali hata CCM nao. Kwamba kuwa mwana-CCM ni kitu kimoja na kuwa mzalendo kwa nchi yako ni kitu chengine.
Kwa hivyo, kwa Msomi wetu Maalim Shamsi, na wengine wote waliomo serikalini na chamani, Barazani, ama iwe watawala au wapinzani, sisi Wazanzibari tunachokihitaji kutoka kwenu ni Zanzibar iliyo na nguvu zaidi, iliyo bora zaidi na makini zaidi. Tunahitaji kuimezua Zanzibar kutoka hali iliyopo hivi sasa.
Narudia tena, hatuhitaji hata kidogo kuvunja Muungano huu, lakini pia hatutaki gharama za kuudumisha Muungano huu ziwe ni kuipopotowa Zanzibar yetu. Itendeeni mema Zanzibar, nchi yenu, mkumbukwe na mkalipwe kwa hayo. Nasema tena kwamba tukishirikiana sote, twaweza kuimezua nchi yetu!
__________________________________________________________
Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Dira katika toleo na tarehe ambayo mwandishi haikumbuki.

Spika Kificho waficha nini? December 16, 2006

Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.
add a comment
Na Mohammed Ghassani
KATIKA siasa, tunaambiwa kuwa ufanisi wa utawala hupatikana kwa kutegemea uongozi na usimamizi madhubuti wa vyombo vinne vikubwa. Kila kimoja kati ya vyombo hivyo hutarajiwa kuwa na uhuru usioingiliwa na chenzake.
Lakini uhuru huo pekee hautoshi kukihakikishia chombo hicho kuwa kinatimiza jukumu lake la kuufanya utawala wa umma kuwa utumishi uliotukuka. Lazima pia kila chombo kiwe na nguvu za kutosha kisheria ili kukizuia chombo chengine kisichupe mpaka wake. Uwepo, mjengeko na ufanyaji kazi wa vyombo hivi huitwa Unne Mtakatifu!
Vyombo vyenyewe ni hivi: chombo cha kuunda sheria, kanuni na taratibu za kuongozana (rule making), cha kuzifanyia kazi (rule implementation), cha kuzitafsiri na kuzipa maana (rule adjudication) na chombo cha kuzichambua, kuzifuatilia na kuzihusisha sheria, kanuni na taratibu hizo na maisha ya raia (rule analysis).
Hiki cha mwisho ndio kwanza kimeingizwa siku za karibuni katika Sayansi ya Siasa. Si kwa kuwa ni kipya, isipokuwa mchango wake katika utawala haukuwa ukitambuliwa hapo zamani.
Leo natuzungumzie uongozi na usimamizi wa hiki cha mwanzo hapa petu, yaani Baraza la Wawakilishi (rule making organ). Msisitizo wetu hasa upo katika nafasi ya Spika wake, Mhe. Pandu Ameir Kificho, katika kujenga utawala bora na kuifanya kazi yake kuutumikia umma kuwa kweli utumishi uliotukuka.
Kutokana na umuhimu na ulazima wa mhimili anaouongoza, spika anakuwa na nafasi kubwa zaidi katika demokrasia ya uwakilishi (representative democracy), ambayo ndiyo tunayojidai kuwa nayo hapa, maana watu wanaouunda wanatokana moja kwa moja na umma.
Mhe. Kificho anaongoza chombo kinachounda sheria ‘kwa jina la umma’. Maana yake ni kuwa kila kinachofanywa na Baraza la Wawakilishi hutambuliwa kuwa kimefanywa na raia wa nchi hii kwa kuwa wao ndio waliowapeleka wajumbe wao barazani kuwawakilisha katika maamuzi ya kuendesha nchi yao. Tunaweza kusema, kwa nafasi yake ya uspika, yeye ndiye anayeuongoza umma wa Zanzibar katika chombo chao hiki cha kuundia sheria.
Kwa hivyo, kinadharia, hata kama hakupigiwa kura za moja kwa moja jimboni, bado naye anawajibika moja kwa moja kwa umma, kwa kuwa utumishi wake umetokana na unahusiana sana na umma huo. Kwamba hata hao waliompigia kura yeye, kwanza walipigiwa kura na umma.
Kwake yeye ndiko kuliko na makutano ya raia na serikali yao kuzungumzia ustawi wa maisha yao na mustaqbal wa nchi yao. Kupitia kwa wawakilishi wao, raia hutumia vikao hivi kuangalia wapi na wapi serikali imetenda kama ilivyowaahidi wakati wa kuomba dhamana ya kuwatawala, na wapi na wapi imetenda sivyo kwa mujibu wa makubaliano yao katika kuombana na kupeana kwao kura.
Ni kutokana na hilo, ndio maana kunakuwa na maswali, hoja, ushauri na changamoto kwa serikali huku ikitakiwa na umma iwajibike kutekeleza dhamana na ahadi zake. Hivyo ndivyo ilivyo.
Kwa hivyo basi, katika hali yoyote ile spika si sehemu ya serikali inayoulizwa maswali, ikajengewa hoja au ikapewa ushauri na changamoto. Spika ni mwangalizi na msimamizi tu wa vikao hivi baina ya serikali, inayowakilishwa na mawaziri, na umma, unaowakilishwa na wawakilishi wao.
Maswali, hoja, ushauri na changamoto huwa havielekezwi kwake yeye, bali kwa serikali. Spika haijibii, haitetei wala haifichii kitu serikali, zaidi ya kuhakikisha kuwa sheria na kanuni za Baraza zinafuatwa katika kila kikao. Hivyo ndivyo inavyotakiwa iwe.
Si stahili, na haifai hata kidogo, kwa spika kujaribu kuikingia kifua serikali kwa hali yoyote ile. Ni sawa kwamba yeye ndiye anayepaswa kuweka nidhamu ya Baraza, kwa kuwa yeye ndiye kiongozi wake. Lakini kuweka huko nidhamu hakuna uwiano wowote na kuinusuru serikali na maswali, hoja au changamoto litokalo kwa wawakilishi wa watu, litokalo kwa umma.
Hapa ni baina ya umma na serikali tu. Wala sio baina ya umma, kwa upande mmoja, na serikali na spika, kwa upande wa pili. Hivyo haitakiwi iwe.
Pamekuwa na matukio mawili matatu ambayo yanamuonesha Mhe. Kificho akicheza nafasi mbili anapokuwa Barazani; moja kama Spika, kwa maana ya msimamizi wa chombo cha uundiaji sheria, na ya pili kama ‘mtetezi’ wa Baraza la Mawaziri.
Ingawa hii ya pili haichezi kwa kujibu maswali au hoja zinazotolewa kwa mawaziri wa serikali, lakini hufanya hivyo kwa kuyazimua maswali, au kuzikwepesha hoja zinazoelekezwa kwao. Hiyo haipendezi, haivutii na inakirihisha. Inatafsirika kuwa Mhe. Kificho anawakingia kifua mawaziri hao kila pale anapoona kuwa kuna hatari ya kukwamishwa na kuwajibishwa na sauti ya wawakilishi wa watu___ sauti ya umma.
Tukio la karibuni zaidi lilitokea wiki iliyopita. Inakumbukwa kuwa si zamani sana tokea Mhe. Hafidh Ali Tahir, mwakilishi wa watu wa jimbo la Rahaleo na ambaye yasemwa kuwa kitaaluma ni mwanakhabari, atake gazeti hili la Dira lifungiwe. Hilo lilikuwa limetanguliwa na kauli ya Mhe. Salim Juma Othman, Waziri katika ofisi ya Waziri Kiongozi anayeshughulikia khabari, kwamba serikali inakusudia kulishitaki Dira katika Baraza la Habari kwa kukiuka kwake maadili ya uandishi.
Suala la kulifungia Dira linapingana, bila ya shaka, na dhana nzima ya utanuzi wa sekta binafsi. Sasa kwa kuwa aliyewahi kulizusha suala hili ni Waziri Salim katika mazungumzo na waandishi wa khabari huko Pemba na kufuatiwa na Mwakilishi Hafidh katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, pakaonesha kuwa hapa pana shaka na shukuki.
Kama tulivyo sisi raia tulio nje ya Baraza, na ambao tunaliangalia Dira sio tu kama gazeti, bali pia kama taasisi ya umma, hata Mhe. Abbas Juma Muhunzi, mwakilishi wa watu wa jimbo la Chambani, naye akawa anataka kujuwa kulikoni. Serikali imesimama wapi na Dira?
Kwamba huko nyuma Waziri Salim alisema kuwa serikali italishitaki gazeti hili, kisha akazuka na Mhe. Hafidh akataka gazeti lifungiwe, tena leo katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, Waziri huyo huyo anazungumzia utanuzi wa sekta binafsi. Mhe. Muhunzi akataka kujuwa serikali imelichukulia vipi ombi la Mhe. Hafidh na ni kwa kiasi gani inalihusisha jambo hilo na utanuzi wa sekta binafsi? Hilo ndilo lililokuwa swali lililohitaji jawabu.
Unajuwa nini kilitokea? Mhe. Kificho akasema kuwa hilo la Dira si swali, kwa hivyo Waziri alitakiwa kujibu tu utanuzi wa sekta binafsi.
Afanaalek! Hivi kama la Dira si swali, huo uhalali wa utanuzi wa sekta binafsi kuwa swali ni upi? Wananchi huku nje walikuwa na sababu na hamu ya kuijuwa kauli ya serikali kuhusiana na Dira hivi sasa. Na hiyo ni kwa sababu zilizotangulia kutajwa huko nyuma.
Kwanza, waliona kuwa uwezekano wa kulishitaki Dira kwenye Baraza la Habari ni finyu sana kwa kuwa khabari si jambo la Muungano, na baraza hilo ni chombo kinachofanya kazi kwa sura ya Muungano. Kwa kuwa hapo, serikali ingelishindwa, basi uwezekano ni kwamba, badala yake, ingelitumia njia nyengine kujenga hoja ya kulifungia.
Pengine ingeliwashawishi watu wake walio nje ya serikali kutoa shinikizo hilo kupitia maandamano au njia yoyote ile na, au, hata kwa kupitia Mwakilishi kuwasilisha hoja binafsi na kupitishwa Barazani. Sasa, hadi hapo watu wakataka kuijuwa nafasi ya Dira, gazeti lao, iko wapi!
Sababu ya pili ni ule uwiano uliopo baina ya hatua za kuliandama gazeti hili___ kitu ambacho hivi sasa kimezoeleka____ na dhana nzima ya kutanua sekta binafsi katika khabari. Ama ikiwa andamo hilo linatokana na serikali, wawakilishi, au watu wa kawaida, Dira ni chombo halali kwa mujibu wa sheria, basi ni kwa vipi serikali inakilinda kama ilivyoapa kulinda na kusimamia sheria za nchi hii?
Maana kulinda na kusimamia sheria ni pamoja na vile vilivyopo kwa mujibu wa sheria hizo. Mwakilishi wa watu alitaka serikali iseme ina msimamo gani juu ya hilo. Kwa maneno mingine, rule making ilitaka kujuwa vipi rule implementation inaitendea rule analysis?
Lakini, kwa Mhe. Kificho, hili lilikuwa ni swali linaloujengea hoja na kuupa changamoto uadilifu wa serikali iliyokamia kusimamisha utawala wa sheria. Na kwa kuwa Spika ni ‘mtetezi wa serikali’ barazani, basi akaikingia kifua: “Swali ni utanuzi wa sekta binafsi”. Kwa hivyo, Waziri akatakiwa kujibu tu serikali inajishugulishaje na utanuzi wa sekta binafsi katika khabari. Akabororowa bwerere, papai kwa kijiko!
Mwenye kuzingatia anaweza kujiuliza: hivi utanuzi huu wa sekta binafsi in relation to what____ kwa kuuhusisha na nini? Kwamba chimbuko la swali halikuwa utanuzi wa sekta binafsi, na hilo Mhe. Kificho analijuwa kuliko ninavyolijuwa mimi. Anajuwa kuwa chimbuko lake lilikuwa ni uhusiano wa utanuzi huo na kauli za wahishimiwa Salim na Hafidh juu ya kufungiwa kwa Dira. Hapo, na hapo tu, ndipo umma unapotaka ujibiwe.
Kwa nini Mhe. Spika Kificho afanye hivi? Anaficha kitu gani hasa, kisijuilikane? Anamficha nani, asijuwe? Anamfichia nani, asifahamike? Kwa kufanya hivi, Mhe. Spika anatujengea dhana nyingi vichwani mwetu na kutufanya tuhoji hata uadilifu wake yeye binafsi, akiwa kama kiongozi wa chombo cha umma. Tuhoji huo utumishi wake wa umma uliotukuka.
Ni kana kwamba anajenga picha kuwa serikali iliyopo madarakani haina dhamira nzuri na utawala wa sheria, na hivyo analificha hilo lisijuilikane. Ni kana kwamba anatuficha sisi raia tuliowapeleka wawakilishi wetu barazani kutuundia sheria na kuangalia utendaji kazi wa watawala tuliowapa dhamana ya kutuongoza, tusijuwe kile kilichopo nyuma ya pazia. Ni kana kwamba anawafichia mawaziri ‘wake’ na kuwasitiri wasibwagwe kwa hoja.
Yumkini, Mhe. Kificho ana khofu zake zinazomfanya afiche, hata kama hazina uhalali. Pengine, sababu moja ni kuwa amezoea kuongoza vikao vyenye wajumbe kutoka upande mmoja tu wa kimawazo na, au, kichama, hivyo hana uzoefu wa migongano ya hoja vikaoni. Huwa anadhani vile watu wakigongana kihoja, huenda wakamalizia kwa kuvunja kanuni za Baraza. Hivyo, ili kulinusuru hilo, huamua kuingilia kati.
Au, pengine, Mhe. Spika huamua kuingilia kati kwa kuwa hawa mawaziri wanaopewa changamoto ni mawaziri kutoka chama chake. Kwa hivyo, anaona kuwa wakikwamishwa wao, ndio kama kimekwamishwa chama chake. Kwamba ikiwa mawaziri hawa wanaonekana kuwa na udhaifu mkubwa kama huo, basi itachukuliwa kuwa hivyo ndivyo ilivyo serikali, na vivyo chama kilichoiunda. Naye, Spika, akiwa mmoja kati ya watu muhimu katika chama, basi ndivyo alivyo!
Lakini, kama nilivyotangulia kusema, khofu hizi hazina uhalali. Spika anatakiwa kuwa jasiri na muadilifu. Awe jasiri kwa kuwa wanaojengeana na kuvunjiana hoja ni watu wazima, tena wastaarabu. Hakuna hasara yoyote kwa mgongano wao wa hoja. Bali, kinyume chake, kuna manufaa mengi yatakayopatikana kupitia mijadala ya aina hii.
Na awe muadilifu kwa kuwa yeye anaongoza mhimili muhimu wa utawala. Lazima ajijengee utumishi unaohishimika. Kama nilivyosema huko nyuma, kinadharia huyu ni sehemu ya watu wanaowakilishwa barazani, na kiutendaji angelitakiwa kusimama baina ya pande hizi mbili, yaani serikali inayotawala na umma unaotawaliwa. Serikali inawakilishwa humu Barazani na mawaziri wake kama vile umma unavyowakilishwa na wawakilishi wao. Hiyo ndiyo mizania iliyopo!
Yeye ni refa tu na anatakiwa kuufanya mchezo huu kuwa fair play. Haipendezi, haikhalisi na inachefua mno kumuona refa anapuliza kipenga na wakati huo huo anapiga shuti kuuondosha mpira kutoka eneo la goli la timu moja. Sasa yeye atakuwa nani? Muamuzi au mchezaji? Akifanya hivyo, si bora akawacha kipenga na kuvaa jezi?
_____________________________________________________________
Dira, Na. 33, Julai 16-24, 2003

Watawala na raia ni kama lila na fila December 16, 2006

Posted by Mohammed Khelef Ghassani in Uncategorized.
add a comment
Na Mohammed Ghassani

BAINA yetu na watawala wetu pana kizingiti cha kimawasiliano (commucational barrier). Nakusudia kusema kwamba si sisi raia wala wao viongozi wetu mwenye uwezo wa kuingia katika akili na kuisoma fikra ya mwenzake. Na kwa hivyo hawatuelewani. Huenda, ikawa kwa kuogopa kuonekana watovu wa nidhamu, basi tuko tunaojifanya kuelewa na kukifurahikia kila kinachosemwa na mtawala wetu, hivyo tukapiga makofi na kurukaruka. Na vivyo, kwa kukhofu kuonekana kuwa haungwi mkono, mtawala naye hujifanya kuyajuwa sana maisha yetu. Hivyo sivyo hali halisi ilivyo. Ukweli ni kuwa pana tatizo kubwa la kimawasiliano.

Inawezekana kabisa kwamba ushiriki wa watu katika mikusanyiko yetu hautokani hata kidogo na mvuto wa mtawala kwao. Watu wanaweza kushiriki katika mkutano wa kiongozi fulani, si kwa kuvutiwa na namna anavyozungumza, bali kwa kuwa pana vishawishi vyengine vilivyo muhimu na bora zaidi na tafauti kwao. Walevi wanaweza kufuata pombe, vijana wa kiume wakafuata wasichana (hasa ikiwa wasichana hao ni hawa wanaovaa mibano na mipasuo), wazee wakafuata kahawa. Au, kutokana na hali yetu ya maisha ilivyo ngumu, wengi wanaweza kuvutiwa na mlo: pilau, haluwa, n.k.
Hapa tanbihi kwa viongozi wetu wa kisiasa ni kwamba wanapojiona wamewaburuta watu wengi katika mikusanyiko yao, wasilewe sifa. Hawapaswi kudhani kuwa watu wote hao wanawapenda na wana imani nao. Lazima wajihakiki na waone ikiwa kweli wao___ wakiwa kama upande mmoja wa mawasiliano___ ni wawasilianaji wazuri na ikiwa kweli kile wakiwasilishacho (ujumbe) katika mikutano yao, ndicho hasa kinachowavuta watu karibu yao___ wakiwa kama upande wa pili wa mawasiliano haya.
Uzoefu unaonesha kwamba wanasiasa wachovu wana kawaida ya kuyadharau matatizo yanayotokana na mawasiliano na ambayo huyaathiri moja kwa moja mahusiano yaliyopo baina yao na wafuasi wao. Huwa wanakosa uwezo na umakini wa kimawasiliano na, hivyo, kushindwa kuzizingatia hisia na fikra za watu wao.
Matokeo yake ni kuharibika kwa mahusiano baina yao. Wanapofikia hapo, wanasiasa hawa huanza kuchukuwa hatua za kikatili kulazimisha kuwepo kwa mahusiano. Hatua hizo husababisha kuwepo kwa mahusiano hasi baina yao. Na hata yanapokuja hayo yanayoonekana kuwa mahusiano chanya, basi huwa ni ya kutungwa tu. Hayo hayawasaidii chochote watawala, labda kuwaharibia zaidi.
Hili ni tatizo la kihistoria katika siasa za kutawaliana, lakini kuwa kwake la kihistoria hakulihalalishi. Kiuongozi na kisiasa, tatizo hili lina gharama kubwa sana, nami nadhani kuwa viongozi wetu wanastahili kusaidiwa kujuwa kwa nini pawe na tafauti kubwa za kimawasiliano baina ya watawala na watawaliwa.
Sababu ni nyingi, mojawapo ni hii ya kutokuchimbukia kwao pahala pamoja, yaani kuwa na viongozi wasiotoka migongoni mwa raia wanaowaongoza. Hapa nakusudia kusema kuwa hawa ni viongozi wasiotokana na maisha wanayoyaishi watu wao walio wengi.
Viongozi hawa huwa aidha wamezaliwa katika pepo za dunia na, au, kwa wale waliotokea katika ufukara, wameshayasahau maisha hayo. Sasa wamekuwa hawajuwi chochote kuhusu mambo yetu sisi tuliozaliwa na kukulia katika maisha ya tabu na dhiki. Misamiati, shida na haja zetu si vitu vinavyoeleweka vichwani mwa viongozi hawa. Hawatujuwi.
Malkia mmoja wa Ufaransa aliwahi kumuuliza mtumishi wake baada ya kuuona umma ukiandamana mbele ya kasri lake: “Kwani wale wanataka nini hasa?” Akaambiwa kuwa wanataka mkate, basi yeye akauliza “kwa nini wasidai keki?”
Malkia hakujuwa kuwa kwa waandamanaji wale, keki si kitu cha kawaida kama vile kilivyo kwake yeye. Wale ni raia waliokuwa na maisha ya dhiki sana kiasi ya kwamba mkate ndio msamiati mkubwa katika maisha yao. Matokeo yake, ufalme wa mumewe ukapinduliwa na raia wanaodai mkate. Mkate tu!
Hivi ndivyo pia walivyo watawala wetu. Hawana uelewa juu ya maisha yetu, watawaliwa. Matokeo yake ni kuwa viongozi hawa wanakuwa wazuri katika majukwaa ya kimataifa, lakini sio katika jukwaa la nyumbani.
Wanazungumza kila lahaja ya Kiingereza, tena vizuri, lakini Kiswahili walichozaliwa nacho kinawapa tabu. Wanapokaa majukwaani hutuvunganyavunganya, la mwanzo wakaliweka mwisho na la mwisho wakaliweka mwanzo. Wanakosa hata misamiati ya kujieleza wao wenyewe mbele yetu.
Wanaujuwa na wanauheshimu sana utandawazi, ndio maana kila siku wanazungumzia umuhimu wa nchi hii kuwamo na kubakia katika mchezo huo wa kilimwengu ulioasisiwa na kusimamiwa na mataifa makubwa. Lakini, kwa bahati mbaya, wanashindwa kuujuwa umuhimu wa nchi hii kudumu katika Muafaka ambao umeasisiwa na kusimamiwa na watu wa nchi hii wenyewe. Ndio maana wanapata uthubutu wa kuuponda, kuukebehi na kuudharau. Sijuwi huo utandawazi wao utatanda uwazi upi, ikiwa kesho na keshokutwa nchi hii itajaa machafuko yatakayotokana na kuvunjwa kwa Muafaka!?
Wanaijuwa sana historia ya Ulaya na Mapinduzi ya Viwanda na awamu zake zilizoanzia 1750, ndio maana wanayazungumzia kistaarabu na kiuchumi. Lakini hawajuwi chochote kuhusu historia na Mapinduzi ya Zanzibar na awamu zake yaliyodumu kwa miaka 40 tu, na ndio maana wanayazungumzia zaidi kikabila na kijazba.
Wanaweza kuziona kwa urahisi sana athari za ugaidi kwa ulimwengu na maslahi ya mataifa makubwa, lakini ni shida kwao kuziona athari za ukandamizaji ndani ya nchi. Wanaijuwa globalization na athari zake, lakini hawajuwi chochote kuhusu udugunaizesheni na athari zake. Hawaujuwi wala hauwapitikii vichwani mwao.
Wanazijuwa zaidi pudding, hamburger na pizza kwa kuwa ndizo zilizowalea na ndizo walizozizowea. Lakini hawajuwi kitu kuhusu shelisheli, biye, togonya na mtoriro; vyakula vilivyotulea na tunavyoshindia sisi raia wanaoutuongoza. Kwa viongozi wetu, hivi si vyakula vinavyofikirika kuliwa na binadamu.
Wanayajuwa zaidi mabenzi yanayoendeshwa kwa kasi lakini yasiyowaumiza abiria wake hata kama barabara ni za mashimo. Lakini hawajuwi chochote kuhusu bavu za mbwa tunazopanda sisi raia tulio wengi. Hawajuwi kuwa humo watu hubanana na mizigo yao ya makozi na muhogo, na hata wakifika safari yao, wako taabani kwa kudundwadundwa mashimoni. Hawaujuwi usafiri huu.
Wanaujuwa usafiri wa Boeing wanaopanda wakapewa chai na vyakula vizuri vinavyotolewa na wahudumu warembo na watanashati, mara tatu kabla hawajafika safari ya robo siku. Hawaujuwi usafiri wa majahazi tunayoyapanda sisi na njaa tokea asubuhi ya siku moja hadi usiku wa siku ya pili.
Hawaujuwi wala hawaujali upepo huu wa Kusi ambao huangamiza mamia ya roho za raia wao wanaotumia usafiri huo. Ndio maana wanashindwa hata kwenda kuwapa mkono wa pole walioondokewa na ndugu na jamaa zao!
Kwa hivyo, chanzo ni huku kutoka na kuishi dunia tafauti kati yetu sisi raia na hao wanaoitwa kuwa ni viongozi wetu. Unaweza kumsikia kiongozi anahutubia katika mkutano wa hadhara huko kwetu kijijini, huku anazungumzia ubinafsishaji, utandawazi, ugaidi, kupunguziwa madeni, nafasi ya kodi katika ukuwaji wa uchumi, na vitu vyengine kama hivyo.
Bila ya shaka, si vibaya kuvizungumzia vitu hivi, lakini suali ni wapi, wakati gani na kwa nani? Busara ya tendo ndilo ni kutendwa pahala ndipo na wakati ndio. Likiepuka mipaka hiyo, tendo hilo huwa halina chembe ya busara, na huwa hasara tupu!
Karibuni Rais Amani Abeid Karume alikuwa akizungumza na wana-CCM wa mikoa mitatu ya Unguja katika kijiji cha Mtende, kusini ya kisiwa cha Unguja. Yale yale tunayoyazungumzia hapa ya ukosefu wa uwiano baina ya kile kilichomo katika fikra za mtawala na za watawaliwa, ndiyo yaliyodhihirika. Pamoja na mengine, Rais alitutaka vijana wa Zanzibar tusikubali hata siku moja kupokonywa uhuru wetu ulioletwa na Mapinduzi ya 1964, maana uhuru una utamu wake. Sadakta kabisa!
Si wakati tena huu wa kuzungumzia uhalali na uharamu wa Uhuru wa 1963 na Mapinduzi ya 1964, lakini itoshe kukubaliana kuwa wazee wetu walipigania uhuru wa nchi hii. Hapo sote tunakubaliana, na ndio maana nikasadikisha maneno ya Rais kututaka vijana tuutambuwe utamu wa uhuru.
Lakini nina hakika kuwa baina yake Rais na sisi vijana wake, pana tafauti kubwa sana ya kuupata uhuru huo. Niseme kuwa ‘uhuru’ wake si ‘uhuru’ wetu. Wake yeye una kila sababu ya kulindwa na kutukuzwa, wa kwetu ni hasara. Wetu ni uhuru-njaa!
Kwamba uhuru uliopo Mazizini sio uhuru uliopo Mtende, na wala haufanani kabisa. Wa Mazizini ni uhuru kwa maana yake hasa___ ni uwezo wa kuamua, kuchagua na nguvu za kupata. Ni uhuru wa kuamka asubuhi na kukuta kila kitu kipo tayari kwa ajili yake. Bafuni kuna maji ya kukoga katika mabeseni makubwa makubwa na mifereji inayotowa kila aina ya maji___ ya moto, vuguvugu, au baridi kwa mujibu wa hali ya hewa na mahitaji ya muogaji.
Mazizini kuna uhuru wa kuwa na umeme kila wakati. Hata TANESCO wafanye tajriba yao ya kuizimia umeme Unguja nzima, basi huko majenereta yanajiwasha yenyewe. Huko ndiko kwenye uhuru wa kula chakula unachokitaka na kwa wakati unaoutaka mwenyewe.
Kuna uhuru wa kupata maji safi na salama, wa kuwa na makazi ya kuridhisha, wa kuvaa nguo za kupendeza. Kuna uhuru wa kuumwa na kupata matibabu mazuri na ya kuridhisha, na mara nyingi nje ya nchi. Huo ndio uhuru wa kulindwa na kumfanya mtu awe ‘mzalendo’. Uhuru wa aina hiyo ukikhatarishwa, lazima aliyenao atokwe na machozi na apigane kwa kucha na meno kuurejesha. Kwamba huo ni uhuru-shibe.
Lakini huo sio uhuru tulionao sisi vijana wake tuliojitia kwenye magari kumfuata yeye kutoka Sogea na Mikunguni. Huku, asubuhi ukiamka, lazima kwanza uwe na shilingi mia ya kununua dumu la maji pale Mwembe Beni, maana mifereji yetu haitoki maji kwa karne sasa.
Ukikosa mia ya kununulia maji, basi itabidi uende kazini na tongo zako, ikiwa hiyo kazi unayo. Ikiwa kazi huna, kama tulivyo wengi wetu, basi utaishia maskani kumsubiri wa ‘kumpiga kirungu’. Tunatakiwa tuulinde na tuutetee uhuru huu, sio kuupinga na kuuondowa?
Utamwambiaje kijana wa Pandani kuwa huu ndio uhuru uliopiganiwa na wazee wake na hivyo aulinde? Uhuru wa kuamka asubuhi na kukimbilia Msaani kwenda kukunguzuwa shina la muhogo, ndiyo chai inywewe nyumbani. Na muhogo wenyewe ni hilo hogo tu. Halina nazi, halina kitoweo. Huu ni uhuru-njaa na basi hauwezi kuwa wa kung’ang’aniwa na vijana wako, mtukufu Rais. Utamwambiaje kijana wako wa Msuka kwamba yuko huru na ajifakharishe, ilhali ndio kwanza anarudi kumzika ndugu yake barobaro zima? Unajuwa alikufa kwa nini?
Alianguka mkarafuu, akaumia vibaya. Hospitali ya Wete wakasema hawana uwezo wa kumtibu hapo, lazima apelekwe Mkoani. Mkoani akaambiwa hadi Mnazi Mmoja, nako akaambiwa hadi KCMC, Moshi. Akafa hajapata matibabu. Huo ndio uhuru wa kujivunia, wa kuumwa bila matibabu?
Kwa nini asijisifu kwa ule ‘uhuru’ wa Mazizini, ambao kijana akiumwa hupanda ndege hadi kwa Mtakatifu Thomas, London, hata kama maradhi yake yangeliwezekana kutibiwa Mnazi Mmoja tu?
Nadhani umefika wakati wa viongozi wetu kujifunza lugha ya kuwasiliana na raia ili kuyafanya mahusiano baina ya watawala na watawaliwa kuwa makini na ya kweli zaidi.
Vyenginevyo, kuna uwezekano wa kiongozi kuwaona kila siku raia wanajaa mikutanoni kwake, naye akadhani kuwa wanamfuata na wanavutiwa naye, na kumbe wanafuata mambo yao: pombe, wanawake, ngoma. Na siku ya siku ikafika, akajikuta wale wale waliokuwa wakiitikia “Ndiyo mzee”, sasa wanasema “Sio mzee”
Katika Communication Works (McGraw-Hill Companies, Inc., 1999), Michael Gamble na Teri Kwal Gamble wanasema kuwa, katika wote, wanasiasa ni watu wanaotegemea zaidi mawasiliano kujijenga na kulinda nafasi zao za kisiasa. Na ili kuendelea kuwa hai kisiasa, basi lazima mwanasiasa aweze kuyajibu ndivyo maswali haya matatu:
La kwanza ni kwa vipi na kwa nini anayaona mambo kama anavyoyaona na raia wanayaona mambo kama wanavyoyaona? Pili, ana uwezo gani wa kusikiliza na kuratibu ujumbe anaoupokea? Na, tatu, anaifahamuje nafasi ya mazingira___ kiuchumi, kisiasa na kiitikadi___ katika kujenga fikra ya watu? Sijuwi ikiwa Mhishimiwa Rais ana majibu kwa maswali haya, na kama anayo, sijuwi ni yapi!
_______________________________________________________________________________Dira, Dira, Na. 36, Agosti 8-14, 2003